2015-10-11 16:29:00

Papa ahuzunishwa na shambulio la kigaidi Ankra Uturuki kuwa ni unyama usiokubalika


Jumapili hii baada ya tafakari fupi  ya Neno la Mungu na sala ya Malaika wa Bwana ,  Mkuu wa Kanisa la Ulimwengu, Papa  Francisko,  aliionyesha huzuni yake kufuatia shambulio la Kigaidi lililofanyika mjini Ankra Uturuki, akisema shambulio hilo ni unyama usioelezeka.  Papa alieleza hilo mbele ya maelfu ya mahujaji na wageni waliofika kusali pamoja naye sala  ya Malaika wa Bwana katika Uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro hapa Vatican.

Papa ameyaita mauaji haya kuwa ni ya kutisha  kwa watu wote walio staraabika na wenye kujali maisha ya wengine.  Amesema haya ni majonzi makubwa yanayoumiza wengi.  Ni Maumivu makubwa kwa sababu, waathirika ni watu wa kawaida wasiokuwa na hatia wala wasioweza kujitetea kwa  nguvu za silaha kali, bali huonyesha madai yao kupitia maandamano ya kawaida ya amani.  Papa alieleza na kuziombea tena kwa Bwana wa huruma na upendo, roho za marehemu ,akiomba pia faraja za matumaini kwa wanaoteseka  na majeraha  na pia kwa familia zao . Papa aliwaomba wote waliofika kumsikiliza katika uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro, wote kwa pamoja kukaa katika ukimya mfupi wa sala, kuwaombea kafara wa tukio hilo.

Jumamosi majira ya Mchana , kwa niaba ya Papa Francisko,  Kardinali Parolin, alipeleka salaam za rambi rambi za Papa kwa njia ya Telegram,  kwa Rais wa Jahuri ya Uturuki  Rais Recep Tayyip Erdoğan, kufuatia janga la mlipuko uliotokea mjini Ankra na kusababisha maisha ya watu kuangamia.

Baba Mtakatifu Francisko alionekana kuhuzunishwa na taarifa za tukio hili, na kuonyesha mshikamano wake dhati kwa wale walioathirika na janga hili.  Na alilaani vikali kitendo hiki akisema ni unyama wa hali ya juu, huku akionyesha ukaribu wake wa kiroho kwa familia zote zinazo guswa na huzuni hii, na kwa ajili ya usalama kwa wale wote waliojitokeza kusaidia majeruhi na kuziombea roho za marehemu wote huruma  Mwenyezi.
 








All the contents on this site are copyrighted ©.