2015-10-10 09:59:00

Yaliyojiri katika tafakari za Mababa wa Sinodi kwenye Makundi!


Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia wameendelea kusikiliza taarifa zilizotolewa kutoka kwenye makundi madogo madogo ambayo kwa mwaka huu yamepewa kipaumbele cha pekee ili kuonesha umoja na utofauti unaoambata utume na maisha ya Kanisa. Wamesikiliza na kutafakari kuhusu changamoto za familia, kwa kukazia zaidi matumaini badala ya kuonesha hali ya kukata tamaa. Mababa wa Sinodi wamepembua na kubainisha utakatifu na uzuri wa maisha ya ndoa na familia licha ya matatizo na changamoto zinazoendelea kujitokeza.

Sakramenti ya Ndoa kadiri ya mpango wa Mungu, inasimikwa katika upendo kamili kati ya bwana na bibi na matunda ya muungano huu thabiti ni watoto ambao kimsingi ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayopaswa kutunzwa na kuelimishwa barabara. Familia ni shule ya ubinadamu, mafungamano ya kijamii na chachu ya ustawi na maendeleo ya jamii. Mababa wa Sinodi wameorodhesha litania ya matatizo na changamoto zinazoikumba familia ya binadamu na hatimaye, kuyaangalia matatizo yote haya katika mwanga wa imani na uso wa huruma unaooneshwa na Kristo Yesu.

Mababa wa Sinodi wanasema, Kanisa halina budi kuibuka kidedea kwa kuzipatia familia imani na matumaini bila kubeza wana kufumbia macho matatizo na changamoto ambazo zinaendelea kuziandama familia ndani ya Kanisa na katika ulimwengu mamboleo. Huu ni mwaliko wa kujenga na kuimarisha mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji kwa familia, ili kuziwezesha familia kupata majiundo makini na endelevu kuhusu imani inayoungamwa na Mama Kanisa; Imani inayoadhimishwa katika Sakramenti za Kanisa; Imani ambayo ni dira na mwelekeo wa maisha ya waamini yanayofumbata Amri za Mungu. Hii ndiyo imani inayosaliwa na waamini kama sehemu ya hija ya maisha yao ya kila siku.

Mababa wa Sinodi wanakiri kwamba, pengine, Kanisa halikuweka mkazo zaidi katika majiundo ya waamini: kiroho na kimwili na matokeo yake ni watu kukengeuka na kutopea katika dhambi na mmong’onyoko wa maadili na utu wema. Kanisa linapaswa kuwa ni mhudumu wa Familia ya Mungu na wala si mmiliki wake. Baadhi ya Mababa wa Sinodi wanakiri kwamba, lugha iliyotumika katika Hati ya kutendea kazi inajifungamanisha mno na matatizo na changamoto za familia Barani Ulaya na hivyo kukosa mwelekeo wa Kanisa la kiulimwengu. Ni lugha ambayo haina mvuto na walengwa wake hawakutajwa bayana. Ni matumaini ya Mababa wa Sinodi kwamba, hati ya mwisho itakuwa hai, wazi na inayoeleweka na waamini wengi zaidi.

Mababa wa Sinodi wanalitaka Kanisa kuwa na mpango mkakati  kwa ajili ya kuwaelimisha na kuwasaidia wahamiaji na wageni; mpango ambao unapaswa kutekelezwa na Kanisa mahalia wanakotoka wahamiaji na wageni pamoja na Kanisa hisani, linalotoa hifadhi kwa wakimbizi na wahamiaji, kwa kukumbuka kwamba, ndani ya Kanisa hakuna mgeni! Mababa wa Sinodi wanakaza kusema, kuna haja ya kupembua kwa kina na mapana changamoto zinazojitokeza katika ulimwengu wa wahamiaji na wakimbizi, haki na wajibu wa watu hawa.

Wazee na watu wenye umri mkubwa ni rasilimali na maktaba rejea ya maisha ya kijamii, kumbe, wanapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa na Jamii husika. Tunu, karama na mapaji ya watu hawa yakuzwe na kupewa na nafasi katika ustawi na maendeleo ya jamii husika. Wazee na walemavu wapewe tunza makini. Kanuni maadili katika sayansi ya binadamu ni mambo ambayo yanapaswa kusisitiziwa ili kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu.

Kanisa lioneshe mifano ya watakatifu wanaopaswa kuigwa kwa kuenzi tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; utakatifu wa ndoa, pamoja na kuainisha vifungu vya Maandiko Matakatifu, ili viweze kuwa ni kikolezo kwa waamini katika maisha yao. Maendeleo ya sayansi na teknolojia yanaathari zake katika malezi na makuzi ya vijana kuhusiana na masuala ya ndoa na familia. Kumbe, kuna haja ya kukazia maadili ya kibayolojia pamoja na  umuhimu wa kutunza na kuenzi useja katika maisha ya waamini.

Mababa wa Sinodi wameridhishwa na majadiliano yanayofanyika katika makundi madogo madogo. Licha ya tofauti zao, lakini wote kwa pamoja wanaunganishwa na Ukatoliki unaofumbatwa katika umoja wa Kanisa. Marekebisho yaliyofanywa kwenye muswada wa kwanza wa hati ya kutendea kazi ni makubwa na kwamba, si kila wazo linaweza kukubaliwa, ndiyo maana kuna haja ya kukuza na kudumisha utamaduni wa kusikilizana, kuheshimiana na kuthaminiana, kwa ajili ya mafao, ustawi na maendeleo ya familia ya binadamu. Kwa mtazamo huu, hakuna atakayeshinda wala kushindwa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.