2015-10-10 07:39:00

Familia na huruma ya Mungu ni chanda na pete!


Kardinali Lluis Martinez Sistach, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Barcellona anasema, maadhimisho ya Sinodi maalum ya Maaskofu kuhusu familia yaliyofanyika kunako mwaka 2014 yalikuwa ni maandalizi makubwa yaliyoliwezesha Kanisa kujipanga barabara ili kukabiliana na changamoto za ushuhuda na utangazaji wa Injili ya Familia kwa watu wa mataifa.

Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya familia yaliyofunguliwa mjini Vatican kuanzia tarehe 4 hadi tarehe 25 Oktoba 2015, yanaongozwa na kauli mbiu “Wito na utume wa familia ndani ya Kanisa na ulimwengu mamboleo” yanagusa kwa namna ya pekee kabisa dhamana, wajibu, changamoto na vikwazo vinavyoendelea kujitokeza katika utume wa familia sehemu mbali mbali za dunia.

Ni matukio ambayo kwa kiasi kikubwa anasema Kardinali Lluis Martinez Sistach kwamba, yameishirikisha Familia ya Mungu kwa kiasi kikubwa, changamoto na maamuzi yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko na kutekelezwa na Sekretarieti ya Sinodi za Maaskofu chini ya usimamizi wa Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu. Wadau mbali mbali wameshirikisha maoni yao, ili kuliwezesha Kanisa hatimaye, kuibua mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji kwa ajili ya utume wa familia.

Hati ya kutendea kazi ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya familia, “Instrumentum Laboris” inaonesha utashi wa Mama Kanisa wa kutaka kuwawezesha waamini kusimama kidete kulinda, kutetea na kushuhudia Injili ya familia. Lengo ni kuimarisha kanuni na tunu msingi za maisha ya ndoa na familia dhidi ya mwelekeo wa sasa unaojikita katika tabia ya ukanimungu na kumong’onyoka kwa tunu msingi za maisha ya ndoa, familia na utu wema.

Kardinali Sistach anasema, kuna umati mkubwa wa watu unaoishi kwenye miji mikuu, lakini kwa vbahati mbaya ni kundi linalokabiliana na upweke hasi unaoweza kulitumbukiza katika utamaduni wa kifo na hali ya kukata na kujikatia tamaa. Ni watu wanaoishi katika mazingira magumu, hata kama baadhi ya watu wanadhani kwamba, wale wanaoishi miji mikuu, wako eti “matawi ya juu”, lakini huko kuna shida na magumu yake.

Mawasiliano ni haba, watu wanapishana utadhani Merikebu baharini; gharama ya maisha inazidi kupanda kila siku, wakati hali ya maisha inaendelea kuporomoka kutokana na hali ngumu ya maisha inayosababishwa na myumbo wa uchumi kitaifa na kimataifa. Watu wanaishi kwa wasi wasi kwa kuhofia usalama wa maisha yao kutokana na vitendo vya kihuni na uvunjaji wa sheria kuongezeka maradufu katika miaka ya hivi karibuni. Watu wanaendelea kukosa imani kwa serikali na vyombo vya sheria kutokana na kukithiri kwa rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma.

Kardinali Sistach anakaza kusema, dini na familia ni taasisi ambazo zinaendelea kuathirika vibaya kutokana na tabia ya ukanimungu, mawazo mepesi mepesi, kukengeuka kwa watu pamoja na kuporomoka kwa kanuni maadili na utu wema. Familia mijini ni sawa na bandari salama, ni mahali ambapo watu wanapaswa kujisikia kwamba, wanapendwa, wanaheshimiwa na kuthaminiwa si kutokana na kile ambacho wamebahatika kumiliki, lakini kwa sababu wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Hapa ni mahali ambapo mtu anapata utambulisho wake katika jamii, hasa pale anapokabiliana na athari za myumbo wa uchumi kwa kukosa fursa za ajira; familia inakuwa ni kimbilio salama la wengi, kwa kugawana hata kile kidogo kinachopatikana! Kwa Wakristo, familia ni shule ya kwanza ya imani, maadili na utu wema. Ni mahali ambapo watoto wanapaswa kurithishwa tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu, kitamaduni, kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko unaotolewa na wazazi pamoja na walezi.

Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanakaza kusema, familia ni Kanisa dogo la nyumbani, ni shule ya haki, amani na utakatifu wa maisha. Familia inajipambanua kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watu wake wakati wa raha na majonzi. Kumbe, dhamana kubwa ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya familia ni kuwawesha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kushuhudia tunu msingi za Injili ya Familia kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mguso katika maisha.

Familia zioneshe uaminifu kwa Neno la Mungu na Mafundisho ya Kanisa kuhusiana na Sakramenti ya Ndoa pamoja na tunu msingi za maisha ya kifamilia. Hapa, Kanisa linahamasishwa kuhakikisha kwamba, linakuwa karibu sana na wanandoa katika hija ya maisha yao ya kila siku, ili kweli waweze kuwa ni mashuhuda amini wa Kristo. Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia inapaswa kuwa kweli ni muhtasari wa Sala ya Familia ya Mungu kwa kuambata tunu msingi za maisha ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Waamini wanahamasishwa kuendelea kusali kwa ajili ya kuombea mafanikio katika maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia.

Kardinali Lluis Martinez Sistach anasema, Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia inapaswa kuunganisha mambo makuu mawili: Uaminifu na huruma ya Mungu. Hii inatokana na ukweli kwamba, mara baada ya kuadhimisha Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya familia, Baba Mtakatifu, tarehe 8 Desemba 2015 atazindua rasmi maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, unaoongozwa na kauli mbiu “Iweni na huruma kama Baba yenu wa mbinguni”.

Hapa, Kanisa linapenda kuonesha kwamba, ni Mama na Mwalimu; mambo msingi yaliyopatiwa kipaumbele cha pekee kabisa katika maisha na utume wa Mtakatifu Yohane wa XXIII. Kanisa liongozwe na kweli za Kiinjili kwa kuwaonjesha watu huruma na upendo wa Mungu. Mwenyeheri Paulo VI alihitimsiha maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kwa kuwataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa kweli ni Wasamaria wema. Kanisa halina budi kuangalia madonda na mipasuko inayoendelea kujitokeza katika maisha na utume wa familia nyakati hizi. Kuna kundi kubwa la wanandoa ambao wameachika na kuamua kuoa au kuolewa tena. Hawa wanapaswa kusaidiwa ili waweze kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Waamini hawa waendelee kujisikia kuwa ni sehemu ya Kanisa na kwamba bado hawajatengwa wala kusahauliwa na Kanisa.

Kardinali Sistach anakaza kusema, Kanisa linapaswa kuwashirikisha watu ukweli unaoambata huruma na upendo wa Mungu unaojidhihirisha katika toba, wongofu na msamaha wa kweli. Hii ni changamoto ya kusoma na kutafakari tena na tena Hati ya kutendea kazi, “Instrumentum Laboris” kama alivyokazia hivi karibuni Baba Mtakatifu Francisko, ili kweli Kanisa liweze kuambata uaminifu na huruma ya Mungu katika maisha na utume wake. Sinodi hii isaidie kuonesha familia huruma na upendo wa Mungu. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika Waraka wa Furaha na Matumaini, “Gaudium et Spes” wanakaza kusema: uchungu na fadhaa ya wanadamu wa nyakati hizi hususan maskini na wale wanaoteseka ni furaha na matumaini; uchungu na fadhaa ya wafuasi wa Kristo pia. Wala hakuna jambo lililo na hali halisi ya kibinadamu lisiloigusa mioyo yao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.