2015-10-09 11:22:00

Msikubali kukumbatia utamaduni wa kifo!


Tangu mwanzo wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia, Mababa wa Sinodi wamelaani vikali tabia ya baadhi ya nchi wafadhali zinazotoa shinikizo kwa nchi changa kubadili kanuni maadili na utu wemwa kwa kuridhia ndoa za watu wa jinsia moja, kifo laini au utoaji wa mimba kama sehemu ya masharti ya kupata msaada wa kiuchumi. Mwelekeo huu ni hatari katika maisha na utume wa ndoa na familia.

Katika mahojiano maalum na Radio Vatican Mama Thèrèse Nyrabukeye, mlezi wa Chama cha Familia nchini Rwanda ambaye pia ni mgeni mwalikwa kwenye maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu anakiri kwamba, pengine wananchi wengi Barani Afrika bado wanatambua na kuheshimu mpango wa Mungu katika kazi ya uumbaji unaowashirikisha bwana na bibi, ambao kimsingi wanaunda familia na matunda ya muungano huu wa upendo ni watoto ambao ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Mwelekeo huu unaojikita katika kanuni maadili na utu wema, pole pole hata Barani Afrika unaanza kuingiliwa na mashinikizo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii yanayojikita katika utamaduni wa kifo, unaowalazimisha watu kukubali sera na mikakati ambayo wakati mwingine yanasigana na kanuni maadili, utu wema, mila, desturi na mapokeo bora ya Kiafrika. Maisha ya mtu ni matakatifu yanapaswa kulindwa, kudumishwa na kuendelezwa kwa kukumbatia Injili ya uhai kama anavyohimiza Mtakatifu Yohane Paulo II.

Hii ni changamoto kwa wanandoa kuhakikisha kwamba, wanasimama kidete kulinda, kutetea na kushuhudia Injili ya familia inayoambata Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Waamini na watu wenye mapenzi mema anasema Mama Nyrabukeye wasikubali kutumbukizwa katika utamaduni wa kifo kwa kisingizio cha “uzazi salama”, haki msingi za binadamu; uhuru wa mtu binafsi au usawa wa kijinsia. Wananchi wasipokuwa makini, baada ya muda si mrefu watajikuta wametumbukizwa katika ukoloni mamboleo na utamaduni wa kifo; mambo ambayo kwa hakika ni majanga kwa ustawi na maendeleo ya familia.

Kanisa hadi sasa limekuwa mstari wa mbele kulinda na kutetea utu, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ni matumaini ya Mama Nyrabukeye kwamba, Kanisa litaendelea kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu; maisha na mafao ya wengi bila kuogopa! Hii ni dhamana pia ya watu wote wenye mapenzi mema, kwani haya ni mapambano ya wote na wala si kwa ajili ya Wakristo peke yao, kwani misingi ya maisha ya ndoa na familia ikiisha bomolewa, jamii nzima itaathirika.

Familia zinahitaji huduma na uangalizi makini, wakati wa raha na shida, ili ziweze kuwa ni mashuhuda wa Injili ya familia. Ili kufikia lengo hili anasema Mama Nyrabukeye, kuna haja kwa wanandoa watarajiwa kupatiwa katekesi makini na endelevu pamoja na Kanisa kuhakikisha kwamba, lina andaa mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji kwa wanandoa na familia, kwani hawa ndio wanaojenga Kanisa dogo la nyumbani na msingi wa maendeleo ya kijamii. Kanisa lina dhamana na wajibu mkubwa katika kuzitegemeza familia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.