2015-10-09 07:51:00

Dumisheni ulinzi na usalama, ili rasilimali ya Taifa iwe ni kwa mafao ya wengi!


Watanzania wanapoelekea kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika hapo tarehe 25 Oktoba 2015, hivi karibuni, Jukwaa la Wakristo Tanzania liliwataka wadau mbali mbali kuhakikisha kwamba, haki, amani, usalama na utulivu vinadumishwa ili watanzania waweze kutumia vyema haki yao ya kuchagua viongozi wanaowataka kwa ajili ya mustakabali wa maendeleo ya watanzania wengi. Badala ya kutumia lugha za kejeli, matusi na vitisho, wagombea uchaguzi na wapambe wao watumie muda huo kwa ajili ya kunadi sera na vipaumbele vyao.

Jukwaa la Wakristo Tanzania linaendelea kuwahimiza watanzania kuhakikisha kwamba, wanaendelea kuiombea Tanzania ili iweze kuwa kweli ni taifa linalojengwa katika misingi ya uhuru, haki na amani na kwamba, viongozi wa dini wataendelea kuwa ni sauti ya kinabii katika kukuza na kudumisha misingi ya uhuru, haki na amani wakati n amara baada ya uchaguzi mkuu nchini Tanzania.

Hivi karibuni, Askofu mkuu Paul Ruzoka, Mwenyekiti wa Tume ya haki, amani, uchumi na mazingira ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, akizungumzia kuhusu utafiti uliofanywa kwenye sekta ya viwanda nchini Tanzania, alikaza kusema, haiwezekani Tanzania kutoa kipaumbele cha kwanza kwa ajili ya kuwalinda wawekezaji wakubwa kwenye machimbo ya madini kwa ajili ya faida yao binafsi. Serikali haina budi kuhakikisha kwamba, mapato yanayotokana na madini yanawanufaisha watanzania wengi na kwamba, wananchi mahalia wanapaswa kufaidika na rasilimali inayowazunguka.

Askofu mkuu Ruzoka anabainisha kwamba, utafiti uliofanywa kwenye Wilaya za Kilwa, Tarime na Geita unaonesha jinsi ambavyo ukuaji wa uchumi katika maeneo haya unavyotegemea kwa kiasi kikubwa sekta ya madini. Kumbe, kuna haja ya kuwekeza zaidi na zaidi katika medani mbali mbali za maisha ili kuboresha ustawi na maendeleo ya wananchi mahalia.

Askofu mkuu Ruzoka anaishauri Tanzania kutumia fedha inayopatikana kutokana na rasilimali mbali mbali zilizoko nchini Tanzania kwa ajili ya kugharimia maboresho ya maisha ya watanzania wengi. Rasilimali ya nchi, usalama wa raia na mali zao, uhuru, haki na amani ni mambo yanayopaswa kusimamiwa kikamilifu bila mzaha. Kumbe, vyombo vya ulinzi na usalama havina budi kuhakikisha kwamba, uchaguzi unafanyika katika mazingira ya haki na amani bila upendeleo, ili rasilimali iliyoko Tanzania iweze kuwa ni kwa mafao na ustawi wa watanzania wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.