2015-10-08 15:11:00

Papa ahoji: kwa nini watu waovu wanaweza onekana kuwa na mafanikio kidunia?


Homilia ya Papa , wakati wa Ibada ya Misa ya Asubuhi kwa Alhamisi hii, ilitazama kwa makini  mateso na mahangaiko mengi yanayokabili  watu wa Mungu , akitolea mfano wa  mama shujaa katika imani, mama  mwenye mme na watoto watatu , mwenye umri chini ya miaka 40 , ambaye anasumbuliwa na maradhi ya mabaya ya kansa  yaliyomweka chini kitandani. Aidha alitoa mfano mwingine akihoji  kwa  nini? Akikumbuka  uchungu na  mateso ya mama mzee , mtu wa sala na mwamini aminifu  kwa Kanisa, ambaye mtoto wake wa  kiume pekee aliuawa bila huruma na kikundi cha uhalifu cha mafia.

Kwa nini maovu haya?, sauti ya Papa Francisco ilisikika ikihoji tokea altare  ya Kanisa dogo la Mtakatifu Marta Vatican, ambamo alikitazama kwa makini kilio cha Nabii Malaki kama ilivyosikika katika somo la kwanza, akilinganisha na hali halisi za wakati huu.

Alihoji , ni mara ngapi tunaona ukweli huu, watu waovu, watu wabaya ambao wako mbali na Mungu lakini maisha yao katika mtazamo wa kidunia kwamba, yanawaendea vizuri: wakionekana kuwa na  maisha ya furaha, wana kila kitu wanachotaka, hawakosi  chochote. Kwa nini Bwana anaruhusu hilo? Ni kati ya  mlolongo wa maswali yetu yanayotafuta sababu kwa nini mtu kama huyo asiyejali uwepo wa Mungu, mtu mdhalimu, mwenye kuzua matatizo mengi kwa wengine mambo yake yote yamwendee vizuri?

Papa alisema, jibu la maswali yetu mengi, limo katika wimbo wa zaburi ya siku , inayotangaza, Heri mtu yule asiyeketi katika baraza la wadhalimu  , Mtu asiyetembea katika njia za wasio haki na wadhambi lakini mwenye kuifurahia  sheria ya Bwana ... Na aliyatumia maswali hayo yasiyokoma katika moyo wa binadamu wenye  tamaa ya kutaka hata ya kuingilia siri za mpango wa Mungu, katika uhusiano na utendaji wake  kwa binadamu, utendaji wa haki na huruma yake. Papa alirejea maandiko kutoka Kitabu cha Nabii Malaki, ambapo Bwana anawakemea watu  akisema," wewe amenikaidi katika neno, asema Bwana, na bado wauliza, tumesema nini kibaya dhidi yako?"  ' Wewe wasema, ni bure kumtumikia Mungu,na twapata faida gani kwa kushika amri zake, na kuvaa mavazi toba kwa dhambi zetu, kwa kumhofia,  Bwana wa majeshi?" Wewe mwenye kuwaona waovu na wenye kiburi kuwa ndiyo wabarikiwa?" Papa Francisko alisema kwa mtazamo wa kidunia , kweli twawaona watenda maovu kuwa ndiyo wenye mafanikio ambao hata hudiriki kumjaribu Mungu bila woga. 

Lakini Papa akaendelea kusema furaha ya watu hao ni  ya mpito, maana baada ya maisha yao hayana nafasi mbinguni maana majina yao hayakuandikwa katika kitabu cha Enzi, Papa alieleza na kusema, ni wazi kwa sasa hatuoni  matunda ya mateso ya waamini , watu  wanaoubeba msalaba wao , kama ilivyokuwa kwa Bwana Ijumaa Kuu ya Mateso , lakini furaha yake  ilionekana Usiku wa Jumamosi Takatifu Kuu,  matunda ya Mwana wa Mungu aliye sulubiwa, mateso yake, kufufuka kwa utukufu mkuu. Na ndivyo ilivyo kwa muumini aminifu ambaye furaha yake imo katika kuzitii sheria za Bwana.   Papa amewatia matumaini wote wanaoteseka na kubaki aminifu kwa Kristo kwamba,  kila jambo , litazaa matunda mazuri.  Na kwamba kwa yale yote yanayoonekana kuwa mazuri kwa wadhalimu na waovu, yatakuwa kama makapi, yatapeperushwa mbali na upepo, kwa sababu Bwana anaijua njia ya wenye haki, na  njia ya wasio itaharibiwa.
 








All the contents on this site are copyrighted ©.