2015-10-08 11:39:00

Fungueni macho! Kuna watoto wanaopofuka kila dakika kwa kukosa tiba!


Jumuiya ya kimataifa, tarehe 8 Oktoba 2015 inaadhimisha Siku ya Macho Duniani, kwa kuwahamasisha wananchi kutambua kwamba, kuna kundi kubwa la watoto wanaokuwa vipofu takribani kila dakika kutokana na ukosefu wa tiba muafaka na vifaa vya macho. Taarifa ya Shirika la Afya Duniani, WHO, inaonesha kwamba, licha ya maendeleo makubwa yaliyokwisha kupatikana katika nchi zilizoendelea kuhusu tiba ya macho, lakini bado kuna kuni kubwa la watoto ambao wanakuwa vipofu kwa kutosa tiba na vifaa vya macho.

Shirika la Afya Duniani linabainisha kwamba, ikiwa kama watoto wengi wangefanyiwa uchunguzi wa macho na kupatiwa dawa kwa wakati muafaka, mchakato huu ungesaidia kupunguza idadi ya watoto wanaoendelea kuwa vipofu siku hadi siku, hususan kutoka katika nchi zinazoendelea duniani. Takwimu zinaonesha kwamba, asilimia 40% ya magonjwa ya macho kwa watoto yanatibika. Ikiwa kama asilimia 60% ya magonjwa ya macho kwa watoto hayataweza kupata tiba muafaka, wanaweza kuwa vipofu katika kipindi cha mwaka mmoja.

Kikundi cha Madaktari wa CBM kutoka Italia kinashiriki kikamilifu katika kampeni ya kusaidia kudhibiti ugonjwa wa macho katika nchini 15: kutoka Afrika, Asia na Amerika ya Kusini kwa kuwahudumia wagonjwa hawa katika Hospitali 19 na vituo vya macho. Ldengo ni kuhakikisha kwamba, Madaktari wa CBM wanatoa tiba kwa wagonjwa 13, 000 pamoja na kufanya upasuaji wa macho kwa wagonjwa 7, 000. Wanapania pia kugawa miwani ya kurekebisha macho ipatayo 6, 000. Kampeni hii inawanufaisha wananchi kutoka Kenya, Ethiopia, DRC, Sudan ya Kusini, Rwanda, Nigeria, Tanzania, Uganda, Zambia, Bolvia, Brazil, Haiti El Salvador, India na Nepal.

Padre Richard A. Mjigwa. C.PP.S,

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.