2015-10-07 10:50:00

Mababa wa Sinodi kwa sasa wanatafakari na kushikirishana mawazo!


Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia yameingia katika hatua ya kushirikishana katika vikundi vidogo vidogo, kwa kuzingatia mambo msingi yaliyokuwa yamejadiliwa kwenye maadhimisho ya awamu ya kwanza ya Sinodi maalum ya Maaskofu kuhusu familia, yaliyofanyika Oktoba, 2014. Baba Mtakatifu Francisko amewakumbusha Mababa wa Sinodi kwamba, hotuba zake rasmi ni ile ya ufunguzi na hitimisho ya Sinodi maalum ya Maaskofu iliyofanyika mwaka 2014 sanjari la Hati elekezi ya Mababa wa Sinodi.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, mafundisho tanzu ya Kanisa kuhusu Sakramenti ya ndoa na Familia hayakuguswa hata kidogo. Ikumbukwe kwamba, Mababa wa Sinodi wanaangalia changamoto za maisha ya ndoa na familia na wala tatizo wanandoa kutalakiana na kuoa au kuoana tena si msingi wa majadiliano ya Mababa wa Sinodi. Baba Mtakatifu anawataka Mababa wa Sinodi kuwa na mwelekeo mpana zaidi katika maisha na utume wa familia ndani ya Kanisa na katika Ulimwengu mamboleo.

Kwa upande wao, Mababa wa Sinodi wanalitaka Kanisa kufanya maamuzi magumu kwa kutoka kifua mbele, tayari kutekeleza utume wa Kanisa kwa watu wa nyakati hizi bila kusahau kwamba useja ni zawadi kubwa kwa watu waliowekwa wakfu, tayari kujitosa kimasomaso kutangaza Habari Njema ya Wokovu. Kanisa linakumbusha kwamba, wazee ni rasilimali muhimu katika kurithisha imani, tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu kwa vijana wa kizazi kipya. Kanisa linawapongeza wazee kwa kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa mahalia. Kinzani na misigano kati ya wazee na vijana wa kizazi kipya inapaswa kupatiwa ufumbuzi, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa.

Ni dhamana na wajibu wa Makanisa mahalia kuwapokea na kuwasaidia wanandoa wanaoteseka kutokana na shida mbali mbali, dhamana hii ni sehemu ya utume na maisha ya Kanisa. Kanisa katika sera na mikakati yake ya kichungaji lijenge madaraja ya kuwakutanisha watu na kamwe lisiwe ni sababu ya baadhi ya Wanakanisa kutengwa na kubezwa. Parokia ziwe ni mahali pa toba, wongofu na upatanisho na kwamba, wanandoa watarajiwa wanapaswa kuandaliwa barabara kutekeleza dhamana na wajibu wao katika maisha na utume wa Kanisa.

Maaskofu mahalia wawe karibu kuhakikisha kwamba, waamini wao wanapata katekesi makini kuhusu maisha ya ndoa na familia. Wanandoa wasiokubaliana na mafundisho ya Kanisa sanjari na mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu wamekuwa ni kikwazo na chanzo cha kuvunjika ndoa nyingi miongoni mwa wanandoa. Wanandoa kama hawa wanapoingia katika mgogoro wa maisha, Mapadre wanaowafahamu wawasaidie na kuwaelimisha, ili kuzuia mpasuko na madonda katika maisha ya ndoa na familia.

Mababa wa Sinodi wamekazia mafundisho tanzu ya Kanisa kuhusu Sakramenti ya Ndoa, msingi thabiti katika maisha ya Kikristo. Mababa wa Sinodi wawe na ujasiri wa kuangalia changamoto zinazowakabili wanandoa kadiri ya maeneo wanamotoka kuliko kutafuta uwezekano wa kuwa na majibu ya jumla. Hii inatokana na ukweli kwamba, Bara la Afrika kwa mfano linachangamoto zake katika maisha na utume wa ndoa kama ilivyo kwa Bara la Ulaya, Asia na kwingineko!

Ili familia iweze kutekeleza wito na utume wake, haina budi kuhakikisha kwamba, inaboresha mahusiano kati ya Bwana, Bibi na Watoto. Mahusiano ya kijamii yanayojitokeza kwa wanandoa wa kizazi kipya yanapaswa kuimarishwa zaidi, ili kuwawezesha wanandoa kutangaza Injili ya familia. Wanandoa wawe makini na kamwe wasikubali kumezwa na malimwengu kwa kukumbatia ubinafsi, uchoyo na hali ya kujitafuta wenyewe.

Mababa wa Sinodi katika tafakari zao wanalitaka Kanisa kuwa karibu zaidi na wanandoa wanaoteseka kiroho, kimwili na kisaiokolojia ili liweze kuwasaidia wasikate tamaa. Ili kufikia lengo hili kuna haja ya kuwa na mbinu mkakati madhubuti wa shughuli za kichungaji kwa ajili ya wanandoa kwa kujikita katika tafakari ya kina ya Neno la Mungu. Wanandoa wenyewe wawe mstari wa mbele kulinda, kutetea na kudumisha Sakramenti ya Ndoa, kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko.

Kanisa litambue kwamba ni Mama na Mwalimu: “Maestra et Magistra” na liwasaidie wanafamilia kutambua kwamba, wao ni wadau wakuu katika mchakato wa Uinjilishaji. Hapa familia zinapaswa kufundwa ili kweli ziweze kuwa na mwelekeo na ari ya kimissionari, tayari kutoka kimasomaso kutangaza Injili ya furaha kwa watu wa mataifa. Kanisa liwe na imani na familia pamoja na kuziwezesha, ili kushuhudia uzuri wa maisha na utume wa ndoa.

Mababa wa Sinodi wanakaza kusema, changamoto nyingine zinahitaji moyo wa mshikamano na upendo unaojikita katika imani tendaji. Kwa njia hii, Kanisa linaweza kuwasaidia wahamiaji, wakristo wanaodhulumiwa na kunyanyaswa, watu wasiokuwa na fursa za ajira, maskini na wote waliokata tamaa. Ndoa mseto zinahitaji majadiliano ya kina yanayojikita katika ukweli na uwazi miongoni mwa waamini. Kati ya changamoto mamboleo, vifo vya wakimbizi kwenye tumbo la bahari vimewagusa Mababa wengi wa Sinodi. Wasichana na wanawake wanaotekwa nyara na kudhalilishwa utu na heshima yao; wasichana wanaolazimishwa kuikana dini yao ya awali wanapaswa kukumbukwa nakusaidiwa.

Mababa wa Sinodi wanataka majadiliano yaguse kwa namna ya pekee familia bila kutenganisha mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji na mafundisho tanzu ya Kanisa. Wawe na ujasiri wa kusoma alama za nyakati ili kuangalia: fursa, matatizo na changamoto zinazoikabili familia ya mwanadamu kwa wakati huu, kwani wanandoa wanataka kuona Kanisa linawajali na kuwatia moyo hata kama halina majibu ya mkato; huruma na upendo wa Mungu uwaguse wanandoa na familia katika maisha na utume wao, ili waweze kweli kusimama kidete kutangaza na kushuhudia Injili ya Familia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.