2015-10-06 14:23:00

Yaliyojiri katika maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia


Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya familia yanayoongozwa na kauli mbiu wito na utume wa Familia ndani ya Kanisa na ulimwengu mamboleo, yalianza kutimua vumbi kwa mkesha wa sala uliofanywa na umati wa waamini kutoka katika Majimbo mbali mbali nchini Italia pamoja na kupata baraka ya tafakari ya kina iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko.

Jumapili, tarehe 4 Oktoba, Mababa wa Sinodi waliendelea na Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Jumatatu mchana, baadhi ya wahusika wakuu wa Sinodi, wakiongozwa na Padre Federico Lombardi, msemaji mkuu wa Vatican walipata nafasi ya kuzungumza na waandishi wa habari kutoka sehemu mbali mbali za dunia, ili kuwajuza yale yanayojiri kwa sasa.

Kardinali Peter Erdo katika tafakari yake elekezi, Jumatatu asubuhi alifafanua kwa kina na mapana hati ya kutendea kazi “Instrumetum Laboris”. Mababa wa Sinodi walipata nafasi ya kusikiliza shuhuda zilizotolewa na baadhi ya wanandoa kuhusu maisha na utume wa Familia ndani ya Kanisa na katika ulimwengu mamboleo.

Kardinali Andrè Vingt-Trois, akizungumza na waandishi wa habari amekazia umuhimu wa Sinodi kama muda uliokubalika kwa Mama Kanisa kutafakari, kusali na kushirikishana uzoefu na mang’amuzi ya shughuli za kichungaji, huku wakiwa wamungana na Baba Mtakatifu Francisko katika kipindi cha majuma matatu. Ni mkusanyiko wa Mababa wa Sinodi kutoka sehemu mbali mbali za dunia, watu wenye umri, uzoefu na mang’amuzi mbali mbali, wanaounda utajiri mkubwa wa Sinodi kwa ajili ya familia.

Huu ni muda muafaka kwa Mababa wa Sinodi kujiweka wazi mbele ya Mwenyezi Mungu ili kusikiliza kwa makini sauti ya Roho Mtakatifu kwa njia ya sala na tafakari; watakuwa wazi kwa jirani zao, ili kushirikishana utajiri unaofumbatwa katika mioyo yao. Mchakato wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu unafanyika kwa njia ya majadiliano, kwa kutambua fursa, matumaini, shida na mahangaiko yanayoendelea kuzikabili familia mbali mbali duniani.

Kwa upande wake, Kardinali Peter Erdo anakaza kusema, Mababa wa Sinodi wamepata nafasi ya kusikiliza kwa muhtasari mawazo makuu yaliyokusanywa kutoka kwa wadau mbali mbali mintarafu maisha na utume wa familia ndani ya Kanisa na katika ulimwengu mamboleo. Waamini wameshirikisha shuhuda mbali mbali ambazo zinatokana na changamoto mbali mbali wanazokabiliana nazo kutoka katika maeneo ya kazi, katika masuala ya uchumi, siasa na kibinadamu. Kuna changamoto kubwa ambazo familia kama taasisi zinakabiliana nazo katika maisha na utume wake.

Katika mwelekeo kama huu, Kanisa halina budi kuhakikisha kwamba, linajikita katika majadiliano yanayolenga kujenga jumuiya ya binadamu. Ni mwaliko kwa familia za Kikristo kuhakikisha kwamba, zinashikamana na kusaidiana kwa hali na mali, kama kielelezo cha imani tendaji. Ni jukumu la wazazi kuhakikisha kuwa wanawarithisha watoto wao imani, mila na tamaduni njema kutoka kwa Kanisa na Jamii inayowazunguka. Kanisa linawajibika kuwasaidia wanandoa wanaokabiliana na matatizo pamoja na changamoto mbali mbali za maisha kama vile ukosefu wa fursa za ajira, magonjwa na kinzani za maisha.

Askofu Bruno Forte, katibu mahuhusi wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya familia anakaza kusema, lengo la maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Familia ni kuwajengea waamini uwezo wa kutangaza na kushuhudia Injili ya familia. Familia inapaswa kuwa ni kiini cha utekelezaji wa shughuli na mikakati ya kichungaji ili kukabiliana kikamilifu na changamoto za maisha ya ndoa na familia.

Mababa wa Sinodi wakiongozwa na alama za nyakati, wazi kwa Roho Mtakatifu na mbele ya Mwenyezi Mungu, watapaswa kufanya maamuzi kwa ajili ya kuzisaidia familia zinazokabiliana na hali ngumu ya maisha. Haya ni maamuzi yanayopaswa kujikita katika ujasiri, unyenyekevu, imani na matumaini kama alivyokazia Baba Mtakatifu Francisko katika tafakari yake ya ufunguzi wa maadhimisho ya Sinodi ya familia. Mababa wa Sinodi wanapaswa kuwajibika ipasavyo pasi na kufumbia macho ukweli kuhusu wito, maisha na utume wa familia ndani ya Kanisa na katika ulimwengu mambo leo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.