2015-10-06 15:03:00

Kodi isaidie kuboresha huduma kwa maskini na akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi


Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini limeitaka Serikali nchini humo kuhakikisha kwamba, maskini na akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi wanapewa nafasi ya kwanza katika mchakato wa mabadiliko ya ongezeko la thamani ya kodi nchini Afrika ya Kusini. Mapato ya kodi yalenge kuleta mabadiliko makubwa katika huduma za kijamii zinazotolewa na Serikali kwa wananchi wake.

Mchango huu ni sehemu ya tamko lililotolewa na Tume ya haki na amani ya Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini, linaloitaka Serikali pamoja na mambo mengine, kuachana na nia yake ya kutaka kuongeza VAT katika bidhaa na huduma inayotolewa nchini Afrika ya Kusini, kwani ongezeko hili litapelekea kupanda kwa bei ya bidhaa na huduma na waathirika wakuu ni maskini na watu wa kipato cha chini.

Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini linasema, kimsingi linaunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali katika maboresho ya huduma za kijamii nchini humo, lakini jambo la msingi ni kuanzisha mfumo wa kodi utakaokuwa rafiki kwa maskini na wala si kama inavyokusudia Serikali kwa wakati huu, kwani madhara yake ni makubwa kwa maskini.

Askofu Abel Gabuza wa Jimbo Katoliki Kimberley anasema gharama ya kuchangia huduma za afya, itolewe na watu wenye kipato cha juu nchini Afrika ya Kusini badala ya kuongeza gharama ya maisha kwa maskini na watu wenye kipato cha chini. Lengo pia ni kupambana na ukosefu wa uhakika wa usalama wa chakula miongoni mwa maskini, ili kudhibiti pia tatizo la utapia mlo wa kutisha kwa watoto nchini Afrika ya kusini.

Tume ya haki na amani, Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini, kwa siku za hivi karibuni, imekuwa mstari wa mbele katika kuwatetea maskini na wanyonge nchini humo. Hivi karibuni, Maaskofu waliongoza maandamano makubwa nchini Afrika ya Kusini kupinga tatizo la rushwa na ufisadi wa mali ya umma, linaloendelea kuongezeka kiasi cha kuwa sasa ni saratani ya kitaifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.