2015-10-06 10:22:00

Kanisa linahamasishwa kuwa ni shuhuda wa huruma ya Mungu katika ukweli!


Baada ya Baba Mtakatifu Francisko kuzindua maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu, Kardinali Peter Erdo, mwezeshaji mkuu alitoa tafakari ya utangulizi iliyogawanyika katika sehemu kuu tatu: changamoto, wito na utume wa familia. Hii ni tafakari elekezi inayofumbatwa katika huruma ya Mungu kwa wanandoa wanaoishi katika mazingira magumu ya kifamilia, lakini katika ukweli. Ni mwaliko kwa Kanisa kuendelea kushikamana na familia maskini sanjari na kusimama kidete kulinda maisha tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake, hadi mauti inapomfika kadiri ya mpango wa Mungu.

Familia zinakabiliana na changamoto nyingi zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu mamboleo, kati ya changamoto hizi ni: uhamiaji, ukosefu wa haki msingi za kijamii, ujira kiduchu usiokidhi mahitaji msingi ya familia; nyanyaso na ukatili dhidi ya wanawake; mazingira magumu ya kazi; utoaji mimba kwa shuruti; mimba za chupa, idadi ndogo ya watoto wanaozaliwa; hamu ya kupata mtoto kwa gharama yoyote ile na madhara yake.

Mambo yote haya yanapelekea taasisi ya familia kuwa dhaifu, kiasi kwamba, baadhi ya watu wanakuwa wagumu kufanya maamuzi machungu katika maisha. Baadhi ya wanandoa wanaonesha utashi wa kuwa na haki zao binafsi, hali inayopelekea ubinafsi wa kutupwa, kiasi cha kushindwa kutambua mipaka kati ya ndoa na familia. Jamii ambayo kwa sasa inajikita katika suala la ulaji inashindwa kutambua tofauti kati ya tendo la ndoa na dhamana ya uumbaji ambayo wanandoa wamekabidhiwa, kiasi cha kugeuza maisha ya binadamu kuwa kama bidhaa.

Kardinali Erdo anaendea kukaza kwa kusema, ndoa na familia ni mambo ambayo yana mwambata mwanadamu katika hija ya maisha yake na hivyo kusaidia katika mchakato wa kurithisha tunu msingi za maisha ya kijamii na kwamba, ndoa inasimikwa katika udumifu ambao kimsingi ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na wala si mzigo kama wanavyodai baadhi ya watu.

Kutokana na ukweli huu, Kanisa linapenda kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, kielelezo cha Jumuiya inayojikita katika maisha yanayofumbata upendo. Familia kama Kanisa la nyumbani linajikita katika msingi wa Sakramenti ya Ndoa, mahali ambapo, wanafamilia wanajifunza kujikita katika kutafuta na kudumisha mafao ya wengi.

Kardinali Erdo anasema kwamba, kuna haja kwa Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, anatoa majiundo makini ya awali na endelevu kwa wanandoa watarajiwa, kwa kugusa mambo msingi katika maisha yao: kiroho, kimwili na Kikanisa. Wakleri waandaliwe vyema ili waweze kuwasaidia wanandoa katika makuzi yao, hususan waweze kuwa makini kuwasaidia wanandoa wanaoishi katika mazingira magumu ya kifamilia, daima wakijitahidi kuwasaidia waamini hao kwa kuzingatia huruma na haki. Hii ni changamoto kubwa kwa Wakleri na wahudumu wa Neno la Mungu, wanaopaswa kuanza kutafuta mfumo mpya wa Katekesi na shuhuda kwa kuonesha uaminifu na ukweli mfunuliwa kutoka kwa Kristo.

Dhamana ya familia ni pamoja na kuendelea kushirikiana na taasisi nyingine, hasa katika maeneo ambayo dhana na uelewa wa familia haushibani wala kuendana na Mafundisho ya Kanisa au mpango wa Mungu katika maisha ya binadamu. Lengo ni kusaidia kuonesha umuhimu wa familia katika jamii. Familia za Kikristo anakaza kusema Kardinali Erdo, zinapaswa kuonesha mshikamano wa dhati kwa familia maskini, familia zisizokuwa na fursa ya ajira; zinazokabiliwa na magonjwa au ambazo zimejikuta zikifilisika kwa kutumbukia katika mchezo wa kamali. Familia za Kikristo ziwe mstari wa mbele kuzisaidia familia zinazoishi katika vita na machafuko ya kisiasa, kijamii na kidini.

Kwa namna ya pekee kabisa, Kanisa linahamasishwa kuwa karibu zaidi na familia ambazo zimejeruhiwa, kwa kuzionjesha huruma na ukarimu pamoja na kuzisaidia kutambua ukweli wa maisha ya ndoa na familia. Kilele cha hali ya juu kabisa cha huruma ni kusema ukweli katika upendo, kwani upendo wa kweli unaunganisha, unabadilisha, unainua na kutoa mwaliko wa toba na wongofu wa ndani.

Kardinali Erdo anasema kwamba, huruma inajikita katika wongofu kwa mdhambi kutambua mapungufu yake, jambo linalohitaji majiundo makini, ili kutambua mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu hususan kwa wanandoa waliotengana na kuamua kuoa au kuoana tena. Majimbo yatenge vituo vya kuwasikiliza wanandoa wanaokabiliana na changamoto katika maisha na utume wao. Huu uwe ni mwanzo wa hija ya msamaha na upatanisho pale inapowezekana. Kwa wale waliooa na kuachika na baadaye wakaamua kuoa au kuolewa wanapaswa kusaidiwa kwa kuzama katika mikakati ya kichungaji inayobainisha kweli za maisha ya ndoa kadiri ya Mafundisho ya Kanisa sanjari na huruma inayotolewa na Mwenyezi Mungu kwa msamaha wa dhambi, unaojikita katika toba na wongofu wa ndani.

Kardinali Erdo anasema kwa wanandoa wanaotamani kupokea Ekaristi Takatifu wanapaswa kufuata hija ya toba itakayowawezesha kupokea Sakramenti ya Upatanisho, bila kusababisha makwazo. Sakramenti ya Kitubio inaweza kutolewa kwa wale wanaotaka kufanya mabadiliko ya kweli katika maisha kwa kuzingatia kanuni maadili, utu wema na wajibu wa wahusika; mambo yanayohitaji majiundo makini ya dhamiri ya wahusika.

Kanisa linahamasishwa kuwa na mbinu mkakati makini kwa ajili ya kuwasaidia mashoga; kwa kuonesha heshima bila kuwabagua, lakini watambue kwamba, ndoa za watu wa jinsia moja si sehemu ya mpango wa Mungu kwa binadamu katika maisha ya ndoa na familia. Kanisa halitakubali shinikizo kutoka katika mashirika ya kimataifa kama sehemu ya masharti ya msaada wa kiuchumi hususan kwa nchi changa zaidi duniani.

Kardinali Peter Erdo katika tafakari yake elekezi anakazia kwa namna ya pekee Injili ya uhai inayopaswa kulindwa, kutetewa na kudumishwa tangu pale mtoto anapotungwa mimba hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Kanisa linapinga kwa nguvu zote vitendo vya utoaji mimba na kifo laini kwa kukumbatia Injili ya uhai. Ni mwaliko kwa Kanisa kuendelea kutoa huduma kwa watoto wanaotelekezwa na wazazi wao; kwa kuwasaidia wanawake wanatoa mimba na familia zihakikishe kwamba, zinaendelea kuwahudumia wagonjwa wao. Kanisa litaendelea kuwahudumia wagonjwa: kiroho na kimwili.

Kardinali Erdo anawahamasisha waamini kuwasaidia watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi kama kielelezo cha mshikamano wa upendo unaofumbata Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Kanisa linaendelea kuwataka wanandoa kuwajibika barabara kwa kuzingatia mpango wa uzazi kwa njia ya asili. Kanisa linapaswa kila wakati kuwa ni kielelezo cha huruma ya Mungu kwa waja wake na kumbe, wazazi ni wahusika wa kwanza wanaowajibika kutoa malezi makini kwa watoto wao. Wawe makini kuangalia elimu inayotolewa kwa watoto wanapokuwa shuleni.

Kardinali Peter Erdo anahitimisha tafakari elekezi kwa kulitaka Kanisa kutubu na kuongoka, ili liweze kuwa hai kama mtu binafsi na kama jumuiya ya waamini. Tayari kushuhudia huruma ya Mungu kwa binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.