2015-10-06 07:21:00

Jikiteni katika mchakato wa upatanisho haki na amani!


Kardinali Philippe Nakellentuba Ouèdraogo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Ouagadougou, Burkina Faso anaungana na Askofu mkuu Piergiorgio Bertoli, Balozi wa Vatican nchini Burkina Faso kuwataka wananchi wa Burkina Faso kushikamana kwa dhati kukuza na kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa unaofumbatwa katika dhana ya upatanisho. Changamoto hii inatolewa na viongozi wa Kanisa Jumapili iliyopita, tarehe 4 Oktoba 2015 katika ibada ya Misa takatifu iliyoadhimishwa kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa de Yagma, baada ya jaribio la kutaka kuipindua Serikali ya Burkina Faso kushindikana hivi karibuni na muasisi wa jaribio hili Gilbert Diendèrè kushikishwa adabu.

Kardinali Ouèdraogo anaitaka Familia ya Mungu nchini Bukrina Faso kujikita katika mchakato wa upatanisho unaofumbatwa katika misingi ya haki, ili kupata amani ya kudumu inayopata chimbuko lake katika mioyo ya watu. Hii ndiyo changamoto pia inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya maandalizi na hatimaye, maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu. Anawataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutubu na kubadili maisha yao; ni wakati muafaka wa kusikiliza kilio cha watu wanaodhulumiwa na kunyimwa haki zao, tayari kukikimbilia na kuambata huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka kwa waja wake.

Baba Mtakatifu Francisko anasema haki na huruma ni sawa na chanda na pete na kwamba, hiki ni kilele cha mapendo yanayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Haki iwawezeshe watu kufuata sheria sanjari na kujikikabidhi kwa imani na matumaini katika utekelezaji wa mapenzi ya Mungu. Mwenyezi Mungu anataka rehema na wala si sadaka na watu wasifuate sheria kwa mazoea tu! Ikumbukwe kwamba, huruma haipingani na haki, bali inaonesha msimamo wa Mungu dhidi ya mdhambi anayechangamotishwa kutubu na kumwongokea Mungu, kwa kuacha njia zake mbaya.

Kwa namna ya pekee, Askofu mkuu Bertoldi anaitaka Familia ya Mungu nchini Burkina Faso kuwa na imani katika mfumo wa sheria na haki pamoja na kuendelea kushirikiana kwa dhati, ili kufanikisha mchakato wa uchaguzi mkuu uliokuwa unatarajiwa kufanyika nchini humo hapo tarehe 11 Oktoba 2015 na kuhairishwa baada ya jaribio la kutaka kuipindua Serikali ya mpito kushindikana. Uchaguzi huu kwa sasa unatarajiwa pengine kufanyika mwezi Desemba, 2015. Itakumbukwa kwamba, Burkina faso tangu kunako mwaka 2014 imetumbukia katika machafuko ya kisiasa baada ya Rais Blaise Compaorè kubwaga manyanga!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.