2015-10-05 11:46:00

Rais Kikwete apongezwa kwa kuinua sekta ya biashara nchini Tanzania!


Wafanyabiashara wa Tanzania wamemwagia sifa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, kwa kuinua uchumi wa Tanzania katika sekta mbalimbali katika miaka 10 ya uongozi wake, kupitia hatua zake mbalimbali alizozichukua katika kipindi hicho cha ustawi wa kasi zaidi kuliko wakati mwingine katika historia ya Tanzania. Wafanyabiashara hao pia wameipongeza Serikali yake kwa kukubaliwa kupata awamu ya pili ya mabilioni kwa mabilioni ya fedha za misaada za Millennium Challenge Coprporation (MCC) ya Marekani na pia kwa kufanikiwa kwenye kigezo cha Serikali yake kuchukua hatua za kwelikweli kupambana na rushwa. Tanzania itapata karibu sh. trilioni moja katika awamu hiyo.

Sifa hizo za wafanyabiashara zilimwaga hapo Oktoba 2, 2015, wakati wa Chakula cha Usiku ambacho wafanyabiashara hao walimwandalia Rais Kikwete kupitia Taasisi yao yaTanzania Private Sector Foundation (TPSF) kwenye Hoteli ya Serena mjini Dar es Salaam. Pongezi hizo za Rais Kikwete ziliogozwa na Mwenyekiti wa TPSF, Bwana Reginald Mengi, ambaye amemshukuru Rais kwa mafanikio yake katika ujenzi wa miundombinu ya barabara, viwanja vya ndege na reli; mawasiliano, kuboresha mazingira ya kufanyia biashara na kulinda utulivu na amani nchini.

“Napenda nikupongeze Mheshimiwa Rais hasa kwa mambo mawili ya karibuni. Moja ni mafanikio ya Serikali yako kupata awamu ya pili ya mabilioni ya fedha za MCC baada ya kuwa Tanzania imeonyesha dhamira thabiti ya kukabiliana na rushwa,” alisema Mengi na kuongeza: “Pili, napenda kukupongeza kwa kuchaguliwa kwako kuwa miongoni mwa watu mashuhuri duniani watakaotafuta njia za kufuta kabisa ugonjwa wa malaria duniani ukiwa kwenye kundi moja na matajiri wakubwa sana duniani”. Siyo kupunguza bali kuufuta ugonjwa huo unaoua watu wetu wengi. Tunajua umeshiriki sana katika mitandao ya kukabiliana na ugonjwa huo kama vile ALMA, Malaria No More, lakini hii ya kujaribu kufuta kabisa ugonjwa huo ni kubwa sana.” Baraza la Kilimo Tanzania (ACT) lilimshukuru Rais Kikwete kwa ulezi wake wa shughuli za kilimo nchini nakusema kuwa anaondoka madarakani wakati dalili za mageuzi makubwa katika sekta hiyo zimeanza kujitokeza wazi wazi nchini.

Chama cha Wana-Mabenki Tanzania (TBA) kimesema kuwa mafanikio katika shughuli za kibenki yanajionyesha wazi wazi kutokana na sera nzuri za miaka 10 ya uongozi wa Rais Kikwete. “Takwimu hazidanganyi Mikopo ya kibiashara nchini imeongezeka kutoka bilioni 1,600 mwaka 2005 hadi kufikia bilioni 14,000 kwa sasa. Matawi ya mabenki nchini yameongezeka kutoka 400 hadi 600 kwasasa na watumishi katika sekta hiyo wameongezeka kutoka 9,000 hadi kufikia 15,000 na sasa nchini zipo benki zaidi ya 52,” alisema mwakilishi wa TBA

Nacho Chama cha Utalii Tanzania kimesema kuwa mafanikio katika sekta hiyo ni dhahiri kabisa kiasi cha kwamba sekta hiyo sasa inaongoza katika kuiingizia Tanzania fedha za kigeni. Alisema mwakilishi wake: “Idadi ya watalii wanaotembelea Tanzania imeongezeka kutoka watalii 612,754 mwaka 2005 hadi kufika watalii 1,138,000 mwaka jana. Hili ni ongezeko la zaidi ya asilimia 80. Tanzania sasa inapata kiasi cha dola za Marekani bilioni mbili kutokana na utalii zikilinganishwa na dola milioni 747.2 mwaka 2005. Hili ni ongezeko la asilimia 163. Ajira zimeongezeka kutoka 500,000 mwaka 2005 hadi kufikia 1,200,000 kwasasa. Tuseme nini zaidi yahapo?”

Chama cha Wafanyabiashara Wanawake katika Tanzania nacho kimetoa pongezi na sifa nyingi kwa mafanikio ya miaka 10 ya uongozi wa Rais Kikwete katika kuwezesha wanawake nchini. Mwenyekiti wake, Bi. Anna Matinde alisema: “Umeanzisha Benki ya Wanawake ambayo ni kimbilio la wanawake wajasiriamali, umeteua akinamama wengi katika nafasi za uongozi, umetupa Spika wa Bunge wa kwanza mwanamke, umetuachia Katiba Inayopendekeza 50-50. Umetuwezesha sana Mhe. Rais.”

Mwenyekiti wa Chama cha Madini Tanzania, Balozi Ami Mpungwe alisema kuwa Rais Kikwete anaondoka madarakani akiwa ameanzisha michakato ya kutekelezwa kwa miradi mikubwa ya madini Tanzania ambayo itabadilisha kabisa sura ya Tanzania. “Mhe. Rais umekuwa mdau wa madini kwa miaka mingi- tokea ulipoingia Serikalini mwaka 1988. Kwasababu hiyo unaijua sana sekta hii na ndiyo maana umeanzisha michakato ya miradi mikubwa ya madini – mradi wa madini ya nickel wa Kabanga, Ngara, mradi wa urani wa Mantra, mradi wa graphite, mradi wa uchimbaji chuma na makaa ya mawe kule Liganga na Mchuchuma. Yote haya yatabadilisha sana sura ya nchi yetu na maisha ya wananchi wake.”

Rais wa Chama cha TCCIA amesema kuwa shughuli za biashara kikiwemo kilimo na uuzaji nje mazao zimeongezeka sana katika miaka 10 ya uongozi wa Rais Kikwete “Mauzo yetu ya nje ya mazao ya kilimo sasa yamefikia dola za Marekani bilioni tano kutoka bilioni 1.6 mwaka 2005, mapato ya bidhaa za nje kuvuka Tanzania kuingia nchi jirani yamepanda kutoka dola za Marekani bilioni 1.2 mwaka 2005 hadi kufikia dola bilioni tisa kwa sasa. Mauzo yetu katika nchi za Jumuia ya Afrika Mashariki yamefikia thamani ya dola za Marekani milioni 569 kutoka dola milioni 162 mwaka 2005, mauzo yetu katika nchi za SADC yamepanda kutoka dola milioni 445 hadi kufikia dola bilioni 1.2. Umeinua sana shughuli za kilimo.”

Makundi hayo mbalimbali, likiwemo Baraza la Taifa la Biashara Tanzania (TNBC) yamempa zawadi mbalimbali na hati za kutambua mchango wa Rais Kikwete katika uongozi wa Tanzania.

Na mwandishi maalum.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.