2015-10-05 11:08:00

Changamoto katika maisha ya ndoa na familia!


Jumapili iliyopita tulitafakarishwa kuhusu ukuu wa Mungu na uwezo wake. Tafakari ya Neno la Mungu jumapili ya leo inatuongoza kuona jinsi Mwenyezi Mungu alivyotushirikisha ukuu na uwezo huo sisi wanadamu, lakini pia itusaidie kuona kama kweli tumetumia vizuri dhamana hii aliyotukabidhi. Tunaadhimisha Jumapili ya 27 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa, sanjari na uzinduzi wa Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia inayoongozwa na kauli mbiu “wito na utume wa Familia ndani ya Kanisa na Ulimwengu mamboleo.

Kwa taarifa yako tu! Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake wakati wa ufunguzi rasmi wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu amekazia umuhimu wa Mama Kanisa kusimama kidete kulinda, kutetea pamoja na kushuhudia tunu msingi za maisha ya ndoa na famia kwa kutambua kwamba, binadamu ana madonda makubwa yanayohitaji kugangwa kwa njia ya toba na huruma ya Mungu. Katika ulimwengu mambo leo, watu wengi ni wakavu. Ikumbukwe kwamba, Mwenyezi Mungu amemuumba mwanadamu ili kumshikirisha furaha na upendo wa dhati. Ndoa si jambo la kufikirika anasema Baba Mtakatifu Francisko! Binadamu hana budi kuambata upendo wa kweli kwa kutambua kwamba, ndoa si jambo la mpito!

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika Familia ya Mungu kuwapokea wanandoa waliojeruhiwa kwa moyo wa upendo na huruma, kwani Kanisa ni uwanja wa mapambano, mahali ambapo wale waliojeruhiwa wanapata tiba, ikiwa kama Kanisa litayaacha malango yake yakiwa wazi, ili wale wanaotaka faraja waonje faraja hiyo kutoka kwa Kristo mwenyewe. Kanisa linapaswa kuwa ni daraja linalowaunganisha watu na kamwe lisiwe ni kikwazo wala kizuizi cha watu wanaokimbilia huruma na msaada wa Mungu katika shida na mahangaiko yao ya ndani. Sasa unaweza kuendelea na tafakari kwa Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya 27 ya Mwaka B wa Kanisa.

Katika Injili,Wayahudi wanaweka mbele ya Yesu swali – je ni halali mume amwache mkewe? Mk. 10:2. Jibu la Yesu ni tofauti kabisa na mawazo yao. Yesu anaangalia historia yote na lengo la mpango wa Mungu wa uumbaji halafu anatoa jibu. Basi alichounganisha Mungu, mwanadamu asikitenganishe – Mk. 9:10. Katika mtazamo huu, Wayahudi waliona ndoa kama kitu cha kawaida sana. Tunasoma hivi katika -  Kumb. 24:1-2. Pakiwa na mtu aliyemchukua mke na kuitimiza ndoa naye, lakini mke yule hampendezi machoni pake, kwa vile ameona kitu kisichofaa, basi amwandikie hati ya talaka akampe mkononi mwake, na kumtoa katika nyumba yake. Naye mke akiondoka nyumbani kwake, akienda kwingine akawa mke wa mune mwingine. Mkazo wa kutoa au sababu ya kutoa talaka ulikuwa ni kwenye kitu kisichofaa.

Hata kati yao Wayahudi kulikuwa na ushindani mkubwa kuhusu ufahamu huo – hicho kitu kisichofaa ni kitu gani. Zilikuwepo shule tatu katika Uyahudi zinazoshindana kutoa majibu. Shule iliyoshikilia msimamo mkali ya Rabbi Shammai walisema hicho kitu ni uzinzi. Shule yenye mawazo huru ya kati ya Rabbi Hillel ilisema kitu hicho ni aina yo yote ya kero aliyosababisha mwanamke na shule yenye mawazo huru zaidi ya Rabbi Aqida ilisema siyo lazima mwanamke awe na kosa lo lote, lakini mwanaume akijisikia hamtaki tena huyo mwanamke basi ilitosha kumpa talaka. Swali lililowekwa mbele ya Yesu likawa mtego kwani angeunga mkono upande mmoja, basi angeingia kwenye mtafaruku mkubwa na pande nyingine.

Hata hivyo hii sheria ya Musa inakataliwa na Yesu huku akisema Mungu aliivumilia tu. Yesu anasema ni kwa sababu ya ugumu wa mioyo yao. Yesu hailaumu sheria ya Musa ila anaweka mbele yao ile sheria ya asili na mpango wa Mungu wa uumbaji. Anatumia nafasi hiyo kukumbusha mpango wa Mungu ulivyokuwa. Pia haongei tu kuhusu sheria ila anaongeza uelewa mpya wa swala la neema – Mk. 10:9, kwamba wanaaswa kubaki waaminifu na kuwa watambue uwepo wa zana zinazowasaidia kubaki hivyo, yaani neema. Kwamba katika huu mpango wa uumbaji inapatikana pia nguvu kwa njia ya roho mtakatifu inayogusa maisha ya mwanadamu. Na hii inakuwa ni neema ya kisakramenti. Tunasoma toka Efeso – Efe. 5:31-32 – kwa hiyo mume atawaacha baba na mama na kuambatana na mke wake. Nao wawili watakuwa mwili mmoja. Fumbo hili ni kubwa, lakini nasema haya juu ya Kristo na kanisa. Na hii dhana ya sakramenti inaenda zaidi ya ile kusema sasa naweza kuwa huru kufanya lo lote juu au dhidi ya mke wangu. Ni zaidi ya hilo. Ndoa sasa inakuwa ni njia ya kuunganika zaidi na Kristo kwa njia ya upendo kwa mwingine, njia halisi ya ukamilifu/utakatifu.

Baba mtakatifu Benedikto XVI katika waraka wake “Deus Caritas Est –  Mungu ni Upendo – N0. 60” anasema muungano huu wa ndoa ni alama ya ukamilifu na ukomavu siyo kwa mtazamo wa kikristo tu, lakini pia katika mtazamo wa kawaida wa kibinadamu.

Ndugu zangu, dhana ya familia na watoto ina maana kubwa na pana sana katika maisha ya mwafrika.   Lakini pamoja na uelewa huu,  dhana ya ndoa na familia iko katika mahangaiko makubwa katika ulimwengu wetu wa leo na kwa namna ya pekee katika familia zetu. Pengine mwenendo wa maisha na hali halisi zinazidi uwezo wetu wa kuishi kadiri ya mapenzi yake mwenyezi Mungu. Jambo la ajabu na ambalo hatuna budi kulifanyia tafakari ni kuwa inaonekana tunataka familia au watoto bila kuwa na mke au kuwa na mume au kuwa na familia ya baba na mama.

Padri Lou, M.M anasimulia kutoka kitabu “Hadithi za Kiafrika” hadithi ya padre Jack aliyeishi kati wa watu maskini huko ukanda wa ziwa. Yeye alikuwa na nyumba nzuri, maji na umeme wa jua wakati wakristo wake majirani hawakuwa na vitu hivyo. Siku moja akiwa anaenda kijijini na katekista wake aliamua kumshirikisha jinsi anavyojisikia. Yeye kuishi katika hali nzuri, ya kiutajiri kati ya maskini yaani kuwa na mahitaji yote ya msingi n.k. Katekista Charles akawa anamsikiliza mpaka alipomaliza maelezo yake. Baada hapo katekista Charles akakunja uso wake kwa mshangao. Halafu akamwambia, lakini padre, wewe ni maskini zaidi kati yetu hapa kijijini. Huku padre Jack akiwa anashangaa kwa neno hilo, katekista akamwambia, huna wajukuu.

Bahati mbaya sana wakati wetu huu dhana ya ndoa na familia imekumbwa na mahangaiko, utengano na mafarakano na shida zinapotokea huwa hakuna juhudi za pekee sana kurekebisa hali hiyo. Haya yote hutokea pale ambapo mwanadamu anaposahau lengo la uumbaji alilotujalia Mungu.  Hata zile tunu za familia katika mila na desturi za kiafrika zimepoteza thamani yake. Mtume Paulo anatoa mchango mkubwa juu ya namna ya kurekebishana kikristo pale inapotokea mifarakano katika familia. Juu ya namna ya kurekebisha hali hii, kukarabati kile kilichoharibika. Katika Efe. 4:26-27 – kasirikianeni lakini msitende dhambi. Jua lisizame kabla hasira yenu haujatulia. Msimpe shetani nafasi, Kol. 3:13 – mvumiliane na msameheane na kama mmoja ana lalamiko dhidi ya mwenzake, basi kama Bwana alivyowasemeheni, nanyi mfanye vivyo hivyo ; Gal. 6:2 – mchukuliane mizigo. Hivyo mtatimiza sheria ya Kristo.

Hatuna budi kukumbuka kuwa fundisho la Yesu na uelewa wake juu ya mwanadamu ni tofauti kabisa na uelewa wetu. Anamtazama mwanamke kama mtu mzima, kiumbe cha Mungu. Wayahudi wanamwangalia mwanamke kama kitu au mali ya mwanaume. Kama kitu cha kutumia na kutupa. Na pili Yesu hajishughulishi kufundisha sheria dunia ila anangalia maadili zaidi. Wanamwuliza kilicho halali kisheria na yeye anawapa jibu ya kile kilicho kizuri zaidi kimaadili, kile cha kutafuta katika maisha. Mtume Paulo anatukumbusha katika – 1 Kor. 10:23-24 – vyote ni halali, lakini si vyote vifaavyo. Vyote ni halali, lakini si vyote vilivyo mfano mwema. Mtu asitafute faida  yake mwenyewe, bali ya mwenzake.

Baba mtakatifu Paulo wa VI anasema tukitaka amani hatuna budi kuipatia roho na roho ya amani ni upendo na kwetu sisi wakristo hii roho hutoka kwa Mungu ambaye ni upendo na hujionesha kwetu tukipendana kati yetu.

Tumsifu Yesu Kristo. Pd. Reginald Mrosso, C.PP.S.

Kanda ya Tanzania.








All the contents on this site are copyrighted ©.