2015-09-25 15:58:00

Papa asema utendaji wa mtu pia huonyesha tabia ya mtu mwenyewe alivyo


Mapema Ijumaa hii 25 Septemba 2015, Baba Mtakatifu alitembelea Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa yaliyoko mjini New York, na kuwahutubia wafanyakazi wote wa Ofisi hizo za Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa. Katika hotuba yake fupi, Papa aliwashukuru kwa dhati na kuonyesha furaha yake kuwa mahali hapo. Aliwatia nguvu akiwataja kwamba wote wake kwa waume, wao ni uti wa mgongo wa chombo hiki muhimu cha Kimataifa. 

Papa alitoa shukurani zake kwa wafanyakazi wote tangu kwa maofisa wa ngazi za juu watalaam hadi kwa wahudumu wa kawaida akisema, kazi zao za kila siku ni muhimu katika kuwezesha kazi za mahusiano ya  kidiplomasia, kiutamaduni, kiuchumi na kisiasa, katika juhudi za  Umoja wa Mataifa, ambazo ni muhimu sana kwa ajili ya kukutanisha matumaini na matarajio ya watu wote wanaounda familia ya binadamu. Na alitambua juhudi na uzoefu wa wafanayakazi hao  kama Maafisa na makatibu, wahariri na wakalimani, wahudumu na wapishi, mafundi wa ukarabati na pia kama maafisa usalama.

Papa aliwashukuru wote kwa moyo wa dhati, kwa kila jambo wanalolifanya kwa manufaa ya wote na hasa kwa majitoleo yao  ambayo si tu huchangia katika ufanikishaji wa kazi za  Umoja wa Mataifa, lakini pia zenye kuwa na maana kubwa, pia  kwao wenyewe binafsi.  Papa alisema jinsi mtu anavyofanya kazi zake huonyesha pia heshima ya mtu mwenyewe alivyo.

Na kwamba wengi wao wametoka katika nchi mbalimbali duniani kote. Na hivyo wanakuwa mfano wa jinsi watu mbalibmali wanavyoweza kuungana na kuwa kitu kimoja katika utumishi kwa manufaa ya wote, na hasa kwa jinsi wanavyoonyesha ustawi wa watoto kupitia mipango mbalimbali ya elimu na lishe. Na pia  katika kujali mustakabali wa dunia na vizazi vijavyo.  

Papa alieleza na kutoa ombi kwa kila mmoja wao, akimtaka bila kujali hadhi yake, wajenge umoja na mshikamano, wakihudumiana  mmoja kwa mwingine. Kufanya kazi zao kwa ukaribu zaidi na zaidi katika hali za kuheshimiana  na umoja kati yao ili shirika hili liwe  mfano wa familia ya binadamu , yenye kuishi katika hali ya mapatano na maelewano si tu kwa ajili  ya amani lakini katika amani , kufanya kazi si tu kwa ajili ya haki lakini katika roho ya haki.

Papa alieleza na kuwahakikishia kwamba kila mmoja wao yumo ndani ya moyo wake .  Na kwamba atatolea sala zake kwa ajili yao na familia zao na akawaomba wao pia wamkumbuke katika sala zao .Na kama kuna wasioamini basi amewaomba wamtakie yaliyo mema. "Mungu awabariki wote. Asante" alimalizia Papa Francisko na kupigiwa makofi mengi . 








All the contents on this site are copyrighted ©.