Jumapili akiwa ziarani Cuba, Baba Mtakatifu Francisco baada kutembelea jengo la Ikulu ya Cuba, kwa muda mfupi alisimama katika Kanisa la Moyo Mtakatifu wa Yesu , lililodhaminishwa kwa Wajesuit. Na mara alikwenda katika Kanisa Kuu la Mjini Havana, la Mtakatifu Maria Asiyekuwa na doa, kwa ajili ya Ibada ya masifu ya jioni, ambako alisali sala hiyo akiwa pamoja na Maaskofu, Mapadre, Watawa na Waseminaristi.
Baba Mtakatifu katika homilia yake alionyesha kuguswa na hotuba ya kumpokea katika Kanisa hilo , iliyotolewa na Kardinali Ortega , ambaye alizungumzia juu ya umaskini wa Kanisa la Cuba na pia Papa alisikiliza ushuhuda wa mtawa mmoja, juu ya kuishi na wagonjwa wasiojiweza na wagonjwa wa akili.
Mahali hapo Papa alishukuru, si tu kudra na huruma ya Mungu lakini pia alikumbuka maisha ya baadhi ya wazee miongoni mwao, wenye kujua yote katika uzoefu wao wa maisha kwamba "huruma zake Mungu ni za milele, na uaminifu wake ni wa karne zote". Papa alieleza na kutoa mwaliko kwa wote kumshukuru Mungu kwa ajili ya hilo.
Aidha Papa kwa namna ya kipekee alitoa shukurani kwa ajili uwepo wa Roho katika utajiri wa karama mbalimbali tofauti za wamisionari , waliofika katika nchi hiyo, watu waliozamia na kubobea na kuwa wananchi Wacuba miongoni mwa Wacuba, ishara inayoonyesha kwamba huruma ya Mungu ni ya milele.
Papa alieleza na kuendelea kutoa tafakari kwa somo la Injili akisema Injili ilikuwa inamwonyesha Yesu akiwa katika mazungumzo na Baba yake . Na hivyo linaashirika muumini kuzamisha kina cha moyo wa urafiki katika sala, kama mazungumzo ya baba na mwana.
Papa alikumbusha wote jinsi saa ya Yesu ilipofika, aliomba kwa ajili ya wanafunzi wake , wali waliokuwa naye na wale wanaokuwa bado kufika , kama ilivyoandikwa katika Injili ya Yoh.17:20. Na kwamba katika wakati huo muhimu, Yesu aliunda mfumo wa maisha ya wanafunzi wake wote, kuwa ni mfumo wa sala na maombi kwa Mungu juu mbinguni . Yesu aliifahamu vyema mioyo ya wanafunzi wake , na alimwomba baba yake awadumishe katika umoja naye..
Na hivyoYesu aliomba kwa Baba yake , awaokoe wafuasi wake dhidi ya roho ya kutengana, roho ya kupapalika wakati wanapokabiliwa matatizo na mashaka, moyo wa kutafuta faraja katika mambo ya mpito na yaliyo tofauti na maadili na wengine na yenye kujenga moyo wa kujitenga. Papa alieleza na kukemea moyo wa namna hiyo ndani ya kanisa akisema, moyo kama huo ndani , huweka makunyazi katika uso mzuri wa Kanisa. Hali hizo huongoza katika mfumo wa kujitenga , na uchovu, kwa huzuni polepole, hupandikiza chuki, na malalamiko ya mara kwa mara, yenye kuleta uchovu . Hayo siyo mapenzi ya Mungu kwa ajili yetu, wala si maisha yanayoongozwa na Roho Mtakatifu (Evangelii Gaudium, 2), kwa wale walioalikwa naye, alisisitiza.
Ndiyo maana Yesu anasali ili kwamba , maisha ya huzuni na kujitenga yasijengeke katika mioyo ya wafuasi wake. Yesu anaomba na anatualika tena kuomba, kwa sababu anajua kuwa baadhi ya mambo yanaweza tu kuwa uzoefu wa maisha kama zawadi.
Papa aliendelea kuzungumzia juu ya umoja akisema ni neema iliyo juu yetu yenye kufanikishwa na Roho Mtakatifu. Hivyo sisi tunapaswa kuiomba neema hii kwa ajili ya mabadiliko chanya katika maisha, mabadiliko yanayofanikishwa na Roho Mtakatifu kama zawadi kwetu.
Papa alifafanua na kuweka bayana kwamba, umoja, mara nyingi huchanganywa na kufanana au kua sare katika utendaji, hisia na maneno. Lakini umoja haina maana ya kuwa sare katika kila jambo, bali ina maana ya kuwa na upendo mmoja kwa mwingine bila kujali tofauti zilizopo katika hisia na itikadi za mwingine. Na umoja mara nyingi huwekwa hatarini pale sisi tunapojaribu kuwaona watu wengine kuwa tofauti na sisi na hivyo kuwatenga au kuwabagua. Kumbe umoja ni zawadi, na si jambo la kulazimisha kwa nguvu au kwa amri, lakini hujengwa na upendo wa kukaribiana na kukutana kama binadamu. Papa alieleza na kutoa mwaliko kwao wote , kumwomba Mungu hamu zaidi ya kukaribiana, mmoja kwa mingine. Kuwa majirani daima, licha ya kutofautiana katika baadhi ya mambo, hiyo ni sehemu ya maisha.
Na aliwalenga moja kwa moja Maaskofu, Mapadre na wahudumu wa Kanisa akiwataka wawe karibu na waamini. Wawe viongozi walio wazi na wenye kujali hoja na matatizo ya wengine. Papa ameitaja migogoro na kutoelewana katika Kanisa, wakati mwingine huhitajika kwa ajili ya kuonyesha uhai wa kanisa na uwepo wa Roho Mtakatifu kwamba yu hai na anafanya kazi zake . Papa alieleza na kukemea jamii ya "ndiyo ndiyo " au ile daima yenye kusema "hapana kwa kila jambo"!.
Papa alikamilisha maelezo yake na ombi kwa Yesu, ambaye daima huruma yake kamwe haifadhaishi, lakini daima huwa na uwezo wa kurejesha furaha yetu. Na hili ni jambo muhimu na la thamani kwa maisha ya watu wa Cuba.
All the contents on this site are copyrighted ©. |