2015-09-11 15:58:00

Serikali ya Tanzania imezindua mradi wa Ujenzi wa kituo cha magonjwa ya moyo


Serikali imezindua mradi wa ujenzi wa kituo cha ubora wa sayansi ya magonjwa na mishipa ya moyo  nchini Tanzania kitakachokuwa na uwezo wa kutoa huduma za kitabibu na kitafiti kwenye magonjwa hayo kwa nchi zote za ukanda wa Afrika mashariki.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika jijini Dar es Salaam Septemba 10, Mkurugenzi wa Elimu ya juu nchini, Profesa Sylivia Temu, alisema mradi huo unaotekelezwa na serikali kwa ushirikiano na Benki ya Maendeleo Afrika, ni mojawapo ya miradi minne ya afya inayotekelezwa kwenye ukanda wa Afrika Mashariki ikilenga kutatua changamoto mbalimbali za kiafya.

Vile alisema kila nchi ya Afrika inayo miradi ya aina yake kwenye sekta hiyo muhimu , na kwa upande wa Tanzania wamejikita katika kukabiliana na magonjwa ya moyo , mradi huo utakuwa chini ya uangalizi wa Chuo kukuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili (Muhas), ambao utakwenda sambamba na ujenzi wa Kampasi mpya ya Chuo Kikuu hicho , kilichoko eneo la Mlonganzila  jijini Dar Es Salaaam.

 Profesa Temu akiongea pia kwa niaba ya Waziri wa Elimu a Mafunzo ya Ufundi Dk Shukuru Kawamba ,aliongeza kwamba mradi huo utasaidia kupunguza vifo vitokanavyo na magonjwa ya moyo nchini, na kupunguz gharama zinazolikabili taifa kwa sasa kutokana na kusafirisha nje idadi kubwa ya wagonjwa wa moyo kupata matibabu.

 Lakini pia kupitia kituo hiki kitakacho kuwa kikubwa kabisa hapa Afrika Mashariki, wanatarajia kwamba tafiti nyingi za masuala ya kiafya hasa kwenye eneo hili la magonjwa ya moyo zitakuwa zikifanyika  nchini Tanzania na pia kupitia Muhas, watazalisha wataalam wengi wa magonjwa hayo kwa manufaa ya vyuo vingine ndani na nje ya nchi, aliongeza.

Kwa upande wa Makamu Mkuu wa Muhas, Profesa Ephata Kaaya, alisema chuo chake kimejipanga kutekeleza mradi huo mkubwa utakaotekelezwa kwa awamu mbili, awamu ya kwanza utahusisha mafunzo pamoja na maandalizi ya vifaa huku awamu ya pili ikuhusisha ujenzi kamili wa kituo hicho alisema.

Meneja Miradi ya Jamii kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika, Hamis Simba, alizitaja baadhi ya sababu zilizosababisha benki hiyo kufadhili mradi ho kuwa ni pamoja  na kuvutiwa na mikakati ya Tanzania na nchi za Afrika Mashariki kwa ujumla katika kukabiliana na magonjwa ya moyo.

Na Shirika la Utafiti wa Magongwa na Tiba barani Afrika (Amref), limezindua zahanati zilizofanyiwa ukarabati kupitia mradi wa Afya ya uzazi ni haki ya vijana tuitetee' katika Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam Tanzania

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Amref, Meneja wa Mradi huo na mtaalamu wa afya ya uzazi na afya ya watoto, Dk. Beatus Sambili, alisema mradi huo ulianzishwa kwa ajili ya kuwakusanya vijana na kuwapatia elimu juu ya namna ya kupambana na magonjwa ya ngono, maambukizi ya Virusi vya Ukimwi, matumizi ya dawa za kulevya na mimba za utotoni. 

Mbali na uzinduzi wa zahanati hizo, pia  Amref imekabidhi vifaa mbalimbali vitakavyotumiwa na zahanati hizo.Baadhi ya vifaa hivyo ni viti, benchi la kukalia wagonjwa lililotengenezwa kwa plastiki, televisheni, deki, ving'amuzi, meza za ofisini na mbao za matangazo. Aidha, alisema mradi huo ulianzishwa kwa kuzilenga Manispaa za Kinondoni na Ilala kwa Jiji la Dar es Salaam na Manispaa ya Iringa kwa Nyanda za Juu Kusini.

 Alizitaja Zahanati zilizonufaika na huduma hiyo kuwa ni Kiwalani, Vingunguti, Mongo la Ndege na kituo na Pugu Kajiungeni. Wakizungumzia mradi huo, Waganga Wafadhili  wa Zahanati zilizofanyiwa ukarabati na Amref, walisema watatumia fursa hiyo kupambana na changamoto zilizokuwa zikiwakabili katika utoaji wa elimu na huduma mbalimbali kwa vijana kutokana na upungufu wa vifaa.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.