2015-08-26 15:42:00

Papa ahimiza familia kutenga muda wa sala na maombi kwa Mungu


Familia ni mahali penye kuwa na upendeleo wa kipekee, katika kina cha kujifunza kutolea sala na maombi kwa Mungu,  kwa  upendo mkuu. Na maombi yaliyo bora zaidi ni yale mafupi, yasiyokuwa na maneno mengi na vitendo vingi. Wakati wa sala na maombi, kusikia hisia za kuwa karibu na Mungu au kuwa mbali naye  inategemea sana uhusiano wetu na Mungu. Ni maelezo ya Baba Mtakatifu Francisco Jumatano hii, katika mwendelezo wa mafundisho yake juu ya familia. Katika katekesi hii,  amehimiza familia, hasa  baba na mama, kutenga muda wa kutolea sala  za shukurani na maombi kwa Mungu, kwa majaliwa ya kila siku. Kama kawaida ya kila Jumatano asubuhi, maelfu ya mahujaji walimiminika katika uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro kumsikiliza Papa, na hii  ilikuwa ni Katekesi ya mia moja  kwa mahujaji na wageni tangu alipochaguliwa kuwa Khalifa wa Mtume Petro.

Papa amezungumzia umuhimu wa kutenga muda wa maombi na sala kwa kuonya kwamba, "licha ya wote kujua umuhimu wa  maombi,  wengi tuna ugumu wa kutenga muda kwa ajili ya maombi. Na  kwa kweli Wakristo wengi hulalamika juu ya kupata muda wa sala na maombi, wengi wakisema kweli ningependa kusali zaidi , lakini nakosa muda wa kufanya hivyo”. Papa ameyataja  malalamiko haya kuwa ya kweli, na  hakika. Na  akakumbusha kwamba, katika ukweli,  moyo wa binadamu daima huwa katika maombi, hata bila kujua hilo, na hasa kama moyo hauna amani. Pale moyo  unapokosa amani, hapo binadamu huona haja ya kumtafuta Mungu, kama hitaji la lazima katika kupambana na yanayo mtatiza au kumkatisha tamaa. Wakati huo binadamu hupenda kupandikiza ndani ya moyo wake upendo motomoto wa Mungu, upendo ulio hai. 

Kwa maelezo Papa, alihoji iwapo motomoto huo, unatokana na imani ya kweli kwa Mungu, kumwamini Mungu kwa moyo wote au ni imani bandia.  Papa alieleza na kusema , kweli ni vyema kuweka  tumaini kwa Mungu wakati wa matatizo,  kuwa na hisia  za kupata jawabu kutoka kwa Mungu, na kuuona wajibu wa kumtolea shukurani. Yote ni  haki. Lakini isiwe tu panapokuwa na mkwamo katika maisha.  Muda wote, nyakati za neema na nyakati za matatizo na mikwamo, ni wakati wa kukutana na Mungu katika sala na maombi. Hivya yafaa daima ,kutenga  muda wa kuzungumza na Mungu. Kupata muda wa  muda hata kidogo wa kutafakari juu ya mema anayotujalia Bwana hata bila kumwomba. Kuwa karibu na Mungu, kumshukuru na kushangalia wema na faraja zake za ajabu.  

Papa alieleza kwa kuirejea  amri kuu ya Mungu: "Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote na kwa nguvu zako zote" (Kum 6,5; taz Mlima 22:37), akisema ni lugha  ya upendo wa kina, inayoturejesha kwa Mungu.  Hapo ndipo roho ya maombi anaishi na kuanzia.

Papa anasema , moyo wa maombi ni moyo uliojaa upendo wa Mungu, chimbuko la maisha yetu. Upendo wenye kujaza  daima faraja za maisha yetu kwa upendo wake mwenyewe. Aliongeza Moyo uliojaa upendo wa Mungu huweza fanya ukimwa wa mawazo , kuwa  ishara dogo mapenzi ya kuwa na kipindi cha maombi.  Na kwamba Roho Mtakatifu hutufundisha jinsi ya  kuomba, jinsi ya kumwita Mungu Baba Yetu , na kukua katika upendo wake kila siku.

Na hivyo familia zetu zinahitaji kuiomba zawadi hii ya Roho Mtakatifu. "Kupitia sala , hata wakati wa nyakati shughuli nyingi zaidi, tunapaswa kupata muda wa kurudisha shukurani kwa Mungu, kwa majaliwa yake, na kwa kufanya hivyo, tunaweza  pata amani inayotokana na  kutambua umuhimu wa furaha ya zawadi tusizo tarajia. Papa alimalizia," kupitia maombi ya kila siku kama ilivyokuwa katika nyumba ya Martha na Mariamu, Yesu hukaribishwa kwa ukarimu".  Papa Francisko ameeleza na kuwataka wazazi wote, baba na Mama , kuwazoeza watoto wao kushiriki katika maombi. Amezihimiza  familia kutosahau kila siku kusoma hata kwa ufupi aya za Injili. Maombi huchipushwa na imani katika neno la Mungu.

 

 

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.