2015-08-19 10:55:00

Nchi maskini hupambana na vikwazo zaidi katika huduma za afya


 Wahudumu wa afya vijiji, wametajwa kuwa msingi wa afya bora vijijini. HIlo limetamkwa katika taarifa ya matokeo ya utafiti uliofanywa na  Chuo Kikuu cha Witwatersrand Afrika Kusini,  juu ya umuhimu wa wahudumu wa afya vijijini.  Matokeo yameonyesha kuwa, jamii inayoishi katika mazingira magumu katika nchi maskini na nchi za kipato cha kati,  ndiyo inakabiliwa na vikwazo vingi katika huduma za afya. Aidha kwamba, uhafifu wa huduma za afya  katika jamii maskini hushamirishwa zaidi na ukosefu wa upatikanaji wa usafiri, maji safi,  usafi wa mazingira na lishe.  Na hivyo kwa matatizo haya , huduma za afya huhitaji mpango makini zaidi ili ziweze kukabiliana na mchanganyiko tata wa changamoto hizo.

Nonhalanhla Nxulalo, anabaini kwamba, njia moja ya kupunguza matatizo hayo ni kwa kutumia wahudumu wa afya vijijini, hasa katika eneo la  Afrika, Kusini mwa Sahara na hasa Afrika Kusini, ambako wahudumu wa afya hufanikisha sehemu kubwa ya  jukumu muhimu katika kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa jamii maskini vijijini. Wahudumu hao hujenga uhusiano kati ya mfumo wa afya na jamii. Wao pia wana uwezo wa kuboresha upatikanaji wa sekta nyingine mbali licha ya afya,  na hivyo hujenga fursa katika ufanikishaji wa ustawi wa  jamii na makazi.

Mwandishi anapongeza juhudi za wahudumu wa Afya  Afrika Kusini, ambao ni zaidi ya 65,000, ambao licha ya kutoa huduma za afya katika jamii maskini pia ni chanzo cha utoaji wa taarifa za afya; huendesha shughuli za kukuza afya na ufahamu juu ya magonjwa;hutambua na kuhudumia maradhi madogo madogo na kuainisha magonjwa sugu kwa matibabu zaidi. Huunganisha jamii na vitendea kazi  na huduma;huendesha shughuli zinazotakiwa katika maeneo kama vile matibabu au ushauri nasaha au  msaada kwa  maradhi ya hatari ya kuambukiza haraka kama TB na VVU, malaria,pamojana  ukarabati katika maradhi mengine hatari kama shinikizo la damu na kisukari.

Hata hivyo, utafiti unaonyesha, pamoja na kazi kubwa zinazofanywa na wahudumu wa afya vijijini katika kuchangia uboreshaji wa huduma za afya, miradi mingi ya afya vijijini wanayo paswa kuiendeleza, hushindwa kuendelea kutokana na matatizo mbalimbali,  ikiwemo uhaba wa fedha,  mifumo dhaifu ya afya toka serikali za mitaa na serikali kuu , elimu duni ya wahudumu, ukosefu wa nyaraka rasmi kama vile vyeti vya kuzaliwa au hati ya utambulisho pia mishahara duni. . 








All the contents on this site are copyrighted ©.