2015-08-15 14:03:00

Kupalizwa kwa Bikira Maria mbinguni kunakumbusha hatima ya maisha ya binadamu


(Vatican Radio) Katika Sikukuu ya Maadhimisho ya kukumbuka tukio la Bikira Maria kupalizwa mbinguni mwili na Roho, ambayo ni tarehe 15 Agosti, Baba Mtakatifu Francisco nyakati za sala ya adhuhuri, aliongoza sala ya Malaika wa Bwana, katika uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Wachambuzi wanasema,  Papa Francisco amekuwa ni Papa wa kwanza katika kipindi cha miaka 60 iliyopita, kuongoza sala ya Malaika wa Bwana katika uwanja huu wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro,wakati wa  Sikukuu  ya maadhimisho ya Bikira Maria kupalizwa mbinguni mwili na roho. Kumbukumbu za kihistoria zinaonyesha, Papa Pius XII, aliongoza sala hiyo katika sikukuu hii  katika uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro miaka sitini iliyopita.

Jumamosi hii, Papa Francisco alivunja ukimya huo, kwa  kuwahutubia mamia ya maelfu ya waamini waliokusanyika katika uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu kwa ajili ya sala ya Malaika wa Bwana. Papa Francisko katika hotuba yake fupi, alitafakari somo la Injili, na Sikukuu ya kupalizwa Bikira Maria mbinguni, akisema inakumbusha hatima ya maisha ya binadamu.Na kwamba, Maria pamoja na kutambua uwezo wa nguvu za vishawishi, vurugu, kiburi, fahari na majivuno ya matajiri, Yeye aliamini neno la Bwana, na kulitangaza kwamba, Mungu kamwe hatawaacha watu wake, maskini na wanyenyekevu.Bali atawapa wale wanaomwamini msaada makini wa huruma yake,  wakati akiwateremsha wenye mamlaka kutoka katika viti vyao vya enzi, na kutawanyika wenye moyo wa majivuno na  kiburi.

Papa Francisco aliendelea kutafakari juu ya Wimbo Mkuu wa Maria, “ Magnificat”, akisema, wimbo huo, unatuwezesha kutazama kwa makini na kuona kwamba huruma ya Mungu ndiyo nguvu yamaisha ya Maria. Mungu asingeweza kuruhusu Maria, kumzaa Bwana wa maisha kutoka katika tumbo lililojaa kiburi cha dhambi.

Papa kwa makini alirejea katika utakatifu wa Maria akianisha na stahili  aliyopewa ya kupalizwa mbinguni mwili na roho, akisema, si Maria peke yake aliyepewa hadhi hii, lakini inakuwa ni stahili kwa kila anayeguswa na kuiamini siri hii, ambayo hukumbusha nini kinatokea katika hatima ya maisha ya mtu. Papa ameonya uwepo wa  binadamu duniani si kwa ajili ya kuzurura kipumbavu, lakini maisha ni hija inayoelekea kwa nyumbani kwa Baba, anayemsubiri kila binadamu kwa upendo mkuu. Na kwamba, wakati wa kupita katika maisha haya, Mungu huonyesha ishara ya uhakika,  matumaini na faraja kupitia kwa Mbarikiwa Bikira Maria ,aliyejaa neema, Mwenyeheri aliyebarikiwa kwa sababu aliamini  Neno la Bwana.

Hivyo Papa amewasisitiza waamini wote wa Kanisa kwamba, kama washarika aminifu wa Kanisa pia wanapata stahili ya kushiriki katika utukufu wa Mama Yetu, na hivyo ni kumshukuru Mungu, kwa kuwa pia waanamini katika sadaka ya Kristo aliyoitoa juu ya msalaba na, kwa njia ya Ubatizo, pia huingizwa katika siri hii ya wokovu.

Baba Mtakatifu baada ya tafakari yake katika wakati huu wa sala ya Malaika wa Bwana, alitoa salaam kwa mahujaji na wageni waliotoka pande mbalimbali za jiji la Roma na duniani kote. Aliwaalika wote wapate nafasi ya kutembelea sanamu ya Mama Yesu wa Salus Populi Romani, Mama Mlinzi wa watu wa jiji la Roma, sanamu iliyowekwa katika Kanisa Kuu la Maria Mkuu katikati ya Jiji Roma.








All the contents on this site are copyrighted ©.