2015-08-13 08:49:00

Papa asema kipindi cha mapumziko ni muhimu na wala si uvivu


Kipindi cha mapumziko baada ya kazi,  ni zawadi ya  thamani ambayo Mungu alifanya kwa familia ya binadamu", ambayo haipaswi kupita au kupuuzwa katika mipango ya utendaji wa familia na mtu binafsi . Ni maelezo ya Papa aliyoyatoa siku ya Jumatano wakati wa katekesi yake kwa mahujaji na wageni waliokuwa wamekusanyika katika Ukumbi wa Paulo VI,mjini Vatican. Papa Francisko alitoa  wito kwa familia kuiishi kama inavyotakiwa Siku ya Mapumziko ya Jumapili, kwa kushiriki katika Ibada ya Ekaristi inayobadili kila wakati wa maisha, hata wakati wa uchungu. Katika Katekesi hii, Papa aliwakumbatia wakimbizi Wakristo kumi waliowasili tokea kituo cha Wakimbizi cha Lampedusa Italia baada ya kutoroka vurugu nchini Nigeria na kuuishi miezi sita ya kazi ya kulazimishwa nchini Libya. 

Papa akitafakari umuhimu wa mapumziko ya baada yakazi, alisema, mapumziko yaliwekwa na Mungu mwenyewe,kama nafasi ya kutafakari uzuri wa kile kilichofanyika au kuumbwa kama Mwenyezi Mungu mwenyewe alivyofanya baada ya kuiumba dunia na vyote vilivyomo. Na hivyo mapumziko inakuwa  nafasi nyingi wazi ya kufikiria pia  jinsi ya kusonga mbele kwa mafanikio zaidi katika kazi. 

Papa alieleza kwa kuangalisha katika kitambu cha Mwanzo, aya zinazozungumzia jinsi Mungu alivyoumba dunia na vilivyomo vyot, na jinsi baada ya kuviumba vyote alipata siku ya kupumzika  y akutafakari yote yaliyofanyika. Hivyo siku mapumziko ilibuniwa na Mungu mwenyewe na akaibariki na kuitakatifusha. Kwa hiyo mwanzo wa kuwa na mapumziko ni upendo na hamu ya Mungu. Papa Francisko aliendelea kukumbusha umati wa watu, kwamba, kubarikiwa kwa siku ya saba kunatufundisha umuhimu wa kuwa na muda wa kutafakari na kufurahia kazi zile zilizofanyika katika muda wa siku sita za wiki.Na si tu katika  maana ya kitaaluma lakini pia kwa maana ya kila utendaji wa wanaume na wanawake hata katika maisha ya familia, kwa namna nyingine inaweza kusemeka kuwa jinsi tulivyoshirikishana katika kazi ya ubunifu wa Mungu.

Kwa hiyo kupumzika si kama uvivu au  kujibweteka, lakini ni wakati mzuri wa kutazama kwanza ya yote yaliyofanyika kwa upendo na kutathimini kazi kwa makini zaidi. Na ndivyo ilivyo hata kw amaisha ya familia , ya  bibi na bwana harusi,baada ya kazi kubwa walizozifanya wakati wa uchumba, hufunga ndoa na kuingia katika kipindi cha mapumziko, kipindi cha kutafakari maisha yao mapya, hii ni jambo jema. Kwa wazazi baba na mama, mapunziko ni muda wa kuangalia watoto au wajukuujinsi wanavyokua na jinsi ya kuunda mfumo wao wa maisha ya baadaye. Kipindi chamapumziko ni wakati wa kutazama kwa makini yanayotakiwa kufanyika ndani ya nyumba zetu, katika kujenga urafiki zaidi na wengine na  jamii inayotuzunguka, na kufikiria juu ya mazuri zaidi. 

Aidha Papa alionyesha kusikitika kwamba , bahati mbaya kumejengeka tabia na mwelekeo wa matumizi mabaya ya siku ya Mapumziko. Wengi huitumia kama siku ya kufuja maisha na mali, wakiyaweka maisha hatarini. Badala ya kuwa katika hali za utulivu wa kutafakari kazi za siku sita, siku ya mapumziko inakuwa ni siku yenye vurugu zaidi kijamii.Wengine wakitafuta kujineemesha zaidi na siku ya mapumziko iliyowekwa na Mungu.  Siku ya mapumziko, hasa zaidi Jumapili ni siku iliyowekwa kwa ajili ya tafakari na si ya kufanya tena kazi za uzalishaji mali. 

Baba Mtakatifu Francisko, alileleza hili katika mwendelezo wa mada juu ya Familia , akiwataka wote waliokuwa wakimsikiliza kutafakari pamoja nae   mambo makuu matatuyasiyoweza kwepeka katika maisha ya familia nayo ni :Mapumziko, Kazi na  Sala.

Na mwisho wa katekesi yake alisalimia mahujaji na wageni kwa lugha mbalimbali, akiwataja wanaozumguza lugha ya Kiingerezahasa kutoka Malta, Zimbabwe, Philippines na Trinidad na Tobago. Aliwatakia wote baraka zake za kitume na  huruma ya Bwana.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.