2015-08-10 09:38:00

Papa asema bila upendo kwa jirani, imani peke yake haitoshi


Unaweza kuwa na imani kubwa hata kutenda miujiza, lakini kama moyo hauko tayari kumpenda jirani,  upendo ambao ni Mungu mwenyewe , imani  iliyopo ni bure. Papa Francisko  alieleza na kutoa sababu kwamba imani kubwa isiyokuwa na upendo thabiti kwa wengine , imani hiyo katika majaribu madogo madogo, hunyauka  na kutoweka mara kama maua, Papa Francisko alieleza Jumapili wakati wa sala ya Malaika wa Bwana, mbele ya mahujaji wengi waliokusanyika katika Uwanja wa Kanisa Kuu la Petro, akiutaza upendo wao kwa Mungu uliowavuta kuja kusikiliza Neno la Mungu  licha ya  joto kali  lililokuwepo.

Akitoa tafakari juu ya Somo la Jumapili la Injili, ambamo watu walishtushwa na maneno ya Yesu alimo sema yeye ni mkate halisi kutoka mbinguni, na kwamba hakuna anayeweza kwenda kwa Mungu Baba, isipokuwa kupitia kwake,  Papa Francisko , alifafanua  kwa kuainisha na mienendo ya imani, hasa mahusiano mtu binafsi na  watu wengine na utu wa Yesu,na katika uthabiti wa uhusiano wa Baba, Mwana na Roho Mtakatifu.

Kwa mtazamo huo Papa alisema , haitoshi kusikiliza habari za Yesu au kusoma Biblia au kushuhudia miujiza na kusema una imani thabiti na Mungu,  kwa kuwa watu wengi hufanya hivyo, humkaribia Yesu lakini  kumbe imani yao ni mbali na upendo wa Yesu, unaomutaka muumini kuwa kama yeye, kujishusha na kuwa mnyenyekevu kwa ajili ya kumtumikia mwingine. Kukubali kuvua ukuu na kutumikia kama Yeye, kuwa na imani kwamba, Yesu ndiye Mwana wa Mungu, Mkate utokao kwa Baba kwa ajili ya wokovu wa binadamu. Wengi  huisoma Biblia, lakini hupuuza hilo na hivyo imani yao inakuwa ni bure, kama somo la Injili lilivyoleza.  Papa, alitaja hawaamini kwa sababu,wamemfungia nje Roho wa Mungu.

Aliendelea kusema, iwapo moyo utabaki umefungwa,mwanga wa  imani ambaye ni Roho Mtakatifu hauwezi kuingia ndani mwake .Aliongeza kuwa  Mungu Baba daima hutuvuta kuelekea kwa Yesu, na sisi tunachotakiwa ni kuifungua mioyo yetu kumruhusu akae ndani yetu, na kuwa karibu naye na kusadiki mafundisho yake. Kumbe imani inakuwa ni kama mbegu iliyopandwa ndani ya  moyo na kuchanua kwa kuamini kwamba Yesu ametoka kwa Baba wa Mbingu na kuja kukaa nasi, kwa nia wazi, moyo wazi, bila  dhambi. Tunatakiwa kuitambua sura yake kwamba ametoka kwa Mungu na kwa maneno yake, namatendo yake, na  Neno la Mungu linalofunuliwa kwetu kwa nguvu za  Roho Mtakatifu, na hivyo kutuwezesha sisi kuishi kwa mahusiano yenye upendo thabiti wenye kumdhihirisha Yesu kuwa Mwana aliyetoka kwa Mungu Baba, na nasi tunapokea  kama zawadi kwa karama ya imani.

Kwa kuishi na imani hii, Papa alisema tunaweza kuelewa maana ya maneno ya Yesu: "Mimi ni mkate hai ulioshuka kutoka mbinguni. Mtu yeyote akila mkate huu ataishi milele na mkate nitakaompa ni mwili wangu kwa maisha ya ulimwengu "(Yn 06:51)":

Papa aliendelea , katika Yesu, katika 'mwili' wake - yaani, katika ubinadamu wake halisi, ina maana ya  upendo wote wa Mungu umeshuka kwa binadamu na unaendelea kudumishwa na Roho Mtakatifu. Wale ambao basi wenyewe wamevutiwa na upendo huu, hufanya hija yao ya maisha kuelekea kwa Yesu wakitembea katika njia ya  imani thabiti kwa ajili ya kupokea kutoka kwake uzima huo wa milele.

Na kwa namna ya kipekee, kwa kila anayeishi na imani hii, Papa Francisko anasema  kuwa , Bikira wa Nazareti, Maria,  binadamu wa kwanza, aliyemwamini  Mungu,  kwa kukubali kuupokea mwili wa Yesu, anakuwa ni mfano hai wa imani wa kujifunza kutoka kwake. Mama Maria ni  mfano hai wa furaha na katika kutoa  shukrani kwa zawadi hii ya imani. Zawadi hiyo isiyo 'binafsi', lakini ni zawadi inayo tolewa kwa  wote, wenye kusadiki na kuipokea , zawadi ya kuwa wamoja katika upendo wa Mungu katika maisha haya ya ulimwengu.  








All the contents on this site are copyrighted ©.