2015-08-07 09:34:00

Barua ya Papa kwa wakimbizi wa Jordan; yadai mshikamano na umoja


Baba  Mtakatifu Francisko, amepeleka ujumbe wa mshikamano kwa wakimbizi, ambamo kwa nguvu pia anaihimiza  jumuiya ya kimataifa, kukabiliana kwa nguvu zote na vipeo vya uhalifu wa haki za binadamu unao endelea Mashariki ya Kati.


Baba Mtakatifu ametuma barua hiyo kwa  Askofu  Mkuu Maroun Lahham wa Jerusalem  ambaye pia ni Vika wa Yordani ,  akionyesha mshikamano wake kwa mamia ya maelfu ya wakimbizi wa Iraki wanaoishi Yordani waliokimbia madhulumu na mauaji  akiwataja  kuwa ni wafia dini wa leo.

Kwa mwaliko wa Askofu Mkuu Lahmam na Patriaki wa Jerusalme Mashariki. Askofu Mkuu Fouwad Toual, Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu la Italia, Askofu Mkuu Nunzio Galantino, kwa wakati huu anatembelea Yordan, kwa lengo la kushiriki katika kumbukumbu ya kupita mwaka mmoja tangu kuwasili kwa wakimbizi wa Iraki nchini Yordani. Katika tukio hili, Askofu Mkuu Galantino, atashiriki katika  matukio mbalimbali yaliyoandaliwa kwa ajili ya kumbukumbu hii.

Ujumbe Baba Mtakatifu kwa wakimbizi wa Yordani , umeanza na maneno ya kuwatia matumaini ndugu hawa walioonewa na kuziishi hali za  vurugu hadi kulazimika  kuachana na nyumba zao na nchi yao.

Papa pia amekemea vikali uwepo wa dhuluma mateso na mauaji ya kinyama yasioweza elezeka  yanayofanya na watu wasiovumilia wengine, ushabiki unaoathiri , ambao haiwezekani kunyamaliwa au kupuuzwa au kukaliwa kimya na jumuiya ya kimataifa.

Papa amewataja watu hao wanaonewa na kuuawa kwa sababu ya imani yao , kuwa ni mashahidi wafia dini wa  leo, wanyonge na wanaobaguliwa kwa sababu ya uaminifu wao kwa Injili.  Aliendelea kukumbusha jinsi Kanisa lisivyo weza kusahau au kuwatelekeza wafuasi wake, hata wale walio uhamishoni kwa sababu ya imani yao. Papa amewashukuru wakimbizi wote kwa uthabiti wa imani na ushahidi wao.

Papa pia katika ujumbe wake hakusahau kuwataja wale wanaosaidia mamia ya maelfu ya wakimbizi  akisema,  utumishi wao unatangaza ufufuo wa Kristo," na  msaada wa ni mwanga wa matumaini wakati wa uwepo wa  giza.  Amewaombea wingi wa baraka za Bwana maana ndiye mtoaji pekee wa zawadi nyingi .

Ujumbe wa Papa , umeonyesha hamu yake ya kuona duniani nzima inajali kwa makini  na kwa kina zaidi, mateso ya watu hao  na hivyo kuwa tayari kushiriki katika hatua zote za kukomesha uso wa mateso yanayofanyika, na kushikamana na Wakristo na jumuiya zingine za kidini hasa zenye waumini wachache wanaodhulumu haki yao ya kuishi kwa uhuru na amani .

Papa kwa mara nyingine, ametoa ombi lake kwa Jumuiya ya Kimataifa, akiitaka isikae  kimya mbele ya jinamizi hili la uso wa uhalifu usiokubalika, au  kupuuzwa maana  ni kitisho kwa  haki za binadamu na huzuia utajiri wa mshikamano kati ya watu, tamaduni na dini. 
Papa Francis alihitimisha kwa kuomba sala na maombi kwa ajili yao , na kuwapa Baraka zake za Kitume na kuwakabidhi chini ya  ulinzi wa kimama a Bikira Maria.








All the contents on this site are copyrighted ©.