2015-08-05 09:09:00

Papa akutana na watumishi wa altareni katika uwanja wa kanisa Kuu la Mtakatifu Petro


(Vatican Radio) Papa Francisko Jumanne majira ya jioni,  alikutana na maelfu ya vijana watumishi wa altareni , kutoka mataifa mbalimbali ya Ulaya, waliokusanyika katika Uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro hapa Vatican.  Hii ilikuwa ni sehemu ya tisa ya  hija  ya Kimataifa ya vijana watumishi wa altareni kutembelea Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro.

Katika hotuba yake  Papa Francisko alitafakari juu ya madambiu ya hija ya mwaka huu, "Mimi hapa! Nitumie".  Baba Mtakatifu aliwaambia vijana, "Ni muhimu kutambua kwamba, kuwa karibu na Yesu na kujua uwepo wake katika  Ekaristi kwa njia ya huduma yao altareni, huwawezesha wao kujifunua wenyewe kwa wengine,na kusafiri pamoja katika ufanikishaji wa malengo muhimu pamoja, na katika  kupata nguvu ya kufanikisha malengo hayo.

Hija Kimataifa ya Watumishi wa Altareni, hufanyika kila baada ya miaka mitano, na huandaliwa na chama cha Kimataifa cha watumishi a Altareni cha “Coetus Internationalis Ministrantium”, pamoja na wawakilishi kutoka nchi kadhaa za Ulaya, ikiwa ni pamoja na Ujerumani, Italia, na Ufaransa, Croatia, Luxembourg, Serbia, na Slovakia. Hija hii ya kimataifa ya watumishi altareni hulenga kuwapa washiriki  uzoefu wa kipekee,  kwa ajili ya huduma yao altareni na kama msaada katika kugundua yaliyomo katika huduma za Kanisa  la Ulimwengu .

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake, aliwashukuru kwa moyo wa dhati wote walioshiriki katika hija hii  maelfu ya vijana baadhi yao wakiwa wamesindikizwa na wazazi au walezi wao, bila kujali joto kali la mwezi Agosti hapa Roma. Na alitoa shukurani za pekee kwa Askofu Nemet, Rais wa juhudi hizi , kwa maneno yake ya  mazuri ya utangulizi na salamu. Na kwa ajili ya hija hii katika mji wa Roma, mji ambapo Mitume Petro na Paulo walikuwa mashahidi.

Papa aliendelea kusema, ni  muhimu kwao kutambua kwamba,  kuwa karibu na Yesu na kumjua katika Ekaristi kwa njia ya huduma yao altareni, kutawawezesha wao kujifunua wenyewe kwa wengine, katika kusafiri pamoja, kulenga pamoja na katika kupata nguvu za kufanikisha malengo  yao. Papa alieleza, “ni  mwanzo wa kuwa na  furaha ya kweli kutokana na kutambua kwamba, licha ya kuwa wadogo na dhaifu, kwa msaada wa Yesu, wanaweza kuwa na nguvu za kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika  safari kubwa ya maisha yao  kwa kuwa pamoja na Yesu. 

Papa alieleza na kuwahimiza wote waliokuwa wakimsikiliza kuwa kama  Nabii Isaya,   alivyogundua ukweli huu na kumwomba Mungu aitakase  nia yake, kumsamehe dhambi zake, kuiponya roho yake,  kumfanya tayari kuchukua kazi muhimu ya kupeleka Neno la Mungu kwa watu wake. Katika kufanya hivyo, akawa chombo cha uwepo wa huruma ya Mungu miongoni mwa watu.  Isaya alitambua kwamba, kwa kujikabidhi mwenyewe katika mikono ya Bwana, Maisha yake yote yatabadilika. Papa alieleza na kuongeza kwa jinsi ilivyo vizuri kutambua kwamba,  imani humwenzesha mtu mwenyewe kujitambua alivyo na kumtoa nje ya kujitenga, kwa sababu hujawa na furaha ya kweli  ya katika urafiki na Yesu Kristo. Imani humuunganisha mtu kwa  wengine na kumfanya kuwa mmisionari asili!

Papa alieleza na kuwakaribishana vijana na  kutoa mwaliko kwao wote watumishi wa  altareni,  wavulana na wasichana ,akiwataka  zaidi ya yote , wakumbuke kuzungumza na Yesu katika maombi yao ya kila siku; zaidi wakijilisha na Neno la Mungu na Mwili wa Bwana, kama silaha na njia bora zaidi ya  kupata nguvu za kutoka nje, kwenda kukutana na wengine, kuwapelekea zawadi waliyoipokea kutoka kwa Bwana wanayemtumikia, na kuitoa kwa wengine kwa shauku ya furaha waliyopokea.

Papa alikamilisha hotuba yake kwa kuwashukuru wote kwa kutumikia altare ya Bwana na kwa ajili ya kuifanya huduma hii, kuwa shule halisi ya kujifunza imani, na upendo kwa jirani. Na pia aliwashukuru kwa kuanza kuitikia wito wa Bwana kama ilivyokuwa kwa Nabii Isaya , kusema "Mimi hapa. Nitumie "(Isa 6: 8).








All the contents on this site are copyrighted ©.