2015-08-02 13:58:00

Mwenye nguvu amenitendea makuu na jina lake ni takatifu!


Kila mwaka ifikapo tarehe 15 Agosti, Mama Kanisa anaadhimisha Siku kuu ya Bikira Maria Kupalizwa mbinguni mwili na roho. Hii ni siku kuu inayounganisha sherehe zote za Bikira Maria kadi ya Mapokeo ya Kanisa Katoliki. Leo katika Liturujia ya Neno la Mungu, tunapenda kuimba utenzi wa sifa na shukrani kwa Bikira Maria aliyepalizwa mbinguni. Lakini kwanza kabisa kabla ya kuzama katika fundisho hili kuu la imani, pata mchapo!

Katika mashindano ya ngumi, mshindi na aliyeshindwa wote wawili wanachakazana vibaya sana. Lakini pengine mshindi anaonekana kupigika zaidi kuliko aliyeshindwa. Vilevile ukimwangalia maiti aliyelala jenezini unapata picha kama ya mtu aliyepigwa sumbwi la nock-out. Zaidi tena ukiuangalia ulimwengu wetu huu, utajiona kama vile upo kwenye uwanja wa ngumi pindi mchezo wa masumbwi ukiendelea kati ya nguvu za kifo (zenye uzito mzito) zikichapana na nguvu za uzima (zenye uzito mwepesi). Ukiyaangalia masumbwi yanayorushwa na nguvu za kifo ni mazito na ya mfululizo yanamnyeshea ndugu uzima kama mvua za masika.

Ama kweli uzima anashughulikiwa kuanzia siku anapoingia ulingoni yaani anapozaliwa duniani. Masumbwi yanayorushwa na kifo ni ya aina nyingi sana ikiwa ni pamoja na masumbwi ya chuki, masumbwi ya upweke, masumbwi ya uhaini, masumbwi ya wivu, masumbwi ya kudhulumiana kiuchumi, kijamii, kisiasa, masumbwi ya woga, masumbwi ya magonjwa mbalimbali nk. Masumbwi mengine kama yale ya ugonjwa yanaweza kukuangusha chini na ukaugulia kitandani muda mrefu. Mbaya zaidi wakati mwingine nguvu ya mauti inaamua kumrukia uzima kwa nguvu zote na kumtupa chini hadi uzima anashindwa kuinua tena, kama inavyosema zaburi “mwenye kulala hivi hainuki tena.”

Hapo ndipo kifo kinatamba lakini bila kushangiliwa kwa sababu watazamaji wote na mashabiki wa uzima wanabaki wanalia tu bila kujitetea kwani “dua la kuku halimpati mwewe.” Ukimwuliza mama kuku “kulikoni ananyang’anywa vifaranga vyake na mwewe huku anaona.” Jibu lake ni jepesi tu: “Nimezidiwa nguvu.” Kadhalika uzima unapomwuliza mwumbaji wake: “Je, mwumbaji wetu uko wapi kuutetea uzima uliouumba unapopigwa masumbwi au labda unafurahia kuangalia jinsi kiumbe chako kinavyopigika na kifo na azma yake ni nini?”

Ndugu yangu, leo Kanisa Katoliki popote duniani tunasherehekea Sikukuu ya Bikira Maria kupalizwa mbinguni. Katika Kanisa fundisho hilo la Maria la kupalizwa mbinguni linaitwa “Dogma” yaani fundisho sadikifu kama ilivyo sikukuu ya Bikira Maria Immakulata au Mkingiwa Dhambi ya Asili (08 Desemba); Bikira Maria Mama wa Mungu (01 Januari) na Kupashwa habari ya kuzaliwa kwa Bwana (25 Machi). Dogma hii ilitangazwa rasmi tarehe moja mwezi Novemba, mwaka 1950 na Baba Mtakatifu Pius XII. Dogma yoyote ile ni tamko linalotafsiri ukweli wa Neno la Mungu lililo katika Biblia. Kwa vyovyote, dogma hiyo ni lugha ya kibinadamu ambayo inategemea sana mabadiliko ya hali halisi ya maisha ya jamii.

Kwa hiyo dogma ni tafsiri ya maisha mbayo inabidi irandane na ukweli wa maisha. Dogma ya Bikira Maria kupalizwa mbinguni imewekwa hivi kwamba iweze kuigusa jamii yetu ya leo. Kwa maana hali ya maisha na matendo ya Mama huyu Maria yanalingana na hali halisi ya mazingira yetu ya sasa. Ukweli huo hauna upinzani, kwani Maria alikuwa mtu kama sisi, alizaliwa kama watu wengine huko Galilea. Akiwa sawa kama watu wengine, mama huyu mwenye uhai alipambana pia na makashkash ya maisha, yaani masumbwi ya nguvu za kifo. Kama vile magonjwa, matatizo ya ndoa kama vile kifo cha mume wake aliyemwacha mjane. Halafu kesi ya Yesu mtoto wake, kesi iliyompelekea kuuawa msalabani na mama kubaki kama gumba na watu wa baki  tu. Katika ulingo ule wa masumbwi, Maria alipigika hasa na hakuweza kurudisha wala kukwepa sumbwi hata moja.

Hebu tuiangalie sikukuu yetu katika mwanga wa masomo ya leo na katika picha ya ulingo wa masumbwi, ili tuweze kuelewa na kufaidika na dogma ya kupalizwa mbinguni. Somo la kwanza linatupeleka kwenye uwanja wa pambano la wanamasumbwi kati ya mwenye uzito mkubwa sana, yaani joka lenye vichwa saba (alama ya nguvu za kishetani yaani nguvu za kifo) likisubiri kuzichapa na mwanamke mwenye uzito mwepesi sana tena mjamzito. Hebu waangalie wapiganaji hao: Upande mmoja yuko “Mwanamke alikuwa na mimba, akilia, hali ana utungu na kuumwa katika kuzaa.” (ufunuo 12:2) .

Upande wa pili: “na tazama, joka kubwa jekundu alikuwa na vichwa saba na pembe kumi, na juu ya vichwa vyake vilemba saba. Na mkia wake wakokota theluthi ya nyota ya mbinguni na kuziangusha katika nchi.” (Ufu. 12:3). Yule mwanamke akiwa bado ulingoni anapata vitisho vikali kwamba atakapozaa tu, atamnyang’anya mtoto wake na kummeza hapohapo. “Na yule joka akasimama mbele ya yule mwanamke aliye tayari kuzaa, ili azaapo, amle mtoto wake.” (Ufu. 12:4).

Lakini Mama huyu akiwa hajui afanye nini baada ya kutishwa na kunyeshewa masumbwi anashtukia ameshinda kwa sababu Baba ya mtoto wake yaani Mungu anaingilia kati kumwokoa yeye na mtoto wake. “Naye akazaa mtoto mwanamume, yeye atakayewachunga mataifa yote kwa fimbo ya chuma. Na mtoto wake akanyakuliwa hata kwa Mungu, na kwa kiti chake cha enzi.” (Yoh. 12:5-6).

Ukweli wa mambo mapambano na ushindi huo ulishatabiliwa na aliyeumba uzima yaani Mungu pale aliposimamisha kwa muda mapambano kati ya Ibilisi na Eva “Kwa sababu umeyafanya hayo, umelaaniwa wewe kuliko wanyama wote, na kuliko hayawani wote walioko mwituni; kwa tumbo utakwenda, na mavumbi utakula siku zote za maisha yako; nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na uao wake; huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda kisigino” (Mwa 3:14-15). Kumbe ushindi dhidi ya joka, shetani au kifo unapatikana unapatikana toka kwa Mungu. Tumwombe Maria atushukurie kwa Mungu Baba. “Ee Maria tusaidie kushukuru.”

Somo la pili linamwonesha mkuu wa uzima akiingilia kati kuunusuru uzima uliopigika vikali na kulala chini wakati mauti yameshajitangazia ushindi. Paulo anamtangaza Kristo kuwa Mshindi wa mauti. Huyo anawachakaza  na kuvunja nguvu za maadui wote wanaoudhulumu uzima. Kristu amefika kuubadilisha uwanja wa masumbwi kuwa tumbo la uzazi lenye kuzaa Uzima wa milele. “Kristo amefufuka katika wafu, limbuko lao waliolala.” (Wakor. 15:20). Kadhalika kifo kinasimangwa na kudharauliwa: “Mauti imemezwa kwa kushinda. Ku wapi, ewe mauti, kushinda kwako? U wapi, ewe mauti, uchungu wako?” (Wakor. 15:54-55). Huyo Kristo ni Mwana wa Bikira Maria. Tumwombe Mama atushukurie kwa Mwanae. “Ee Maria tusaidie kushukuru”.

Injili ya leo ni shairi alilotunga mama huyu mpiganaji baada ya ushindi. Ni utenzi wa shukrani na wa kuishabikia nguvu za Mkuu wa uzima kutokana na maajabu aliyotutendewa. Nguvu za Mungu zimefanikiwa kumweka mkombozi (mtoto wa kiume) kwenye tumbo la uzazi la Bikira na nguvu zimeyafunua makaburi walimolala majeruhi, yaani Kristo mwenyewe, Maria na tulimolala sisi sisi sote. Hebu tumwache Mama Maria afurahi kwani yeye ni alama ya ushindi wa uzima dhidi ya mauti. Tumpongeze Maria kwa kukubali kuzipiga na nyoka hadi leo anastahili kupata taji la ushindi. Aidha, tumwombe Maria atusaidie kumshukuru Mungu kwa kibwagizo kifuatacho “Ee Maria tusaidie kushukuru” na tuendelee kuimba pamoja naye: “Moyo wangu wamtukuza Bwana, na roho yangu imeshangilia Mungu mkombozi wangu.”

Heri sana kwa sikukuu ya Kupalizwa Bikira Maria Mbinguni. Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.