2015-08-02 08:27:00

Mwaka Mtakatifu: Ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani!


Mpendwa Msikilizaji wa Kipindi cha Hazina yetu, tunakusalimu kutoka katika Studio za Radio Vatican, Tumsifu Yesu Kristo. Mama Kanisa anakuletea ujumbe kuhusu huruma ya Mungu. Tunapojiandaa kuupokea na kuuadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya Huruma ya Mungu, Baba Mtakatifu Francisko amependa kutupatia mafundisho rasmi katika Waraka wa kichungaji ujulikanao kwa jina la Misericordiae vultus yaani "Uso wa huruma.

Ndani ya  waraka huu tunapata dira kamili ya yale tutakayoyatenda katika mwaka huo Mtakatifu wa Jubilei. Ni mwaliko kwetu sote kufanya kila liwezekanao tuusome na tuuelewe waraka huu vema. Katika kipindi hiki cha hazina yetu, tunakumegea baadhi ya mambo ambayo Baba Mtakatifu  ameyaainisha mintarafu Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya Huruma ya Mungu.

Katika kipindi kilichopita, Baba Mtakatifu kwa undani na uzito wa pekee sana aligusia juu ya Sakramenti ya Upatanisho, huku akitualika waamini wote kukimbilia kiti cha huruma ya Mungu, tuweze kuguswa kwa neema zake za utakaso. Kwa namna ya pekee aliwaalika mapadre pia  (hasa kipindi cha kwaresma), kujibidisha sana kuwatafuta kondoo waliopotea au “wale waliosimama nje” mfano wa yule mwana mkubwa aliyebaki nyumbani yaani “kaka ya mwana mpotevu”. Kwa kukataa kuingia ndani kusherehekea kurudi kwa mdogo wake aliyepotea, naye pia alijionesha kuwa ni mpotevu zaidi. Hivyo alihitaji kufuatwa na huruma ya yuleyule Baba mwema, huruma yenye kumsihi aingie ndani, akafurahi pamoja na mwenzake.

Hali kadhalika, anabainisha Baba Mtakatifu, katika maisha ya waamini, wapo wale ambao kwa sababu ya ubinafsi, ugumu wa mioyo na kukosa kuguswa na mahangaiko ya wengine, huwa hawafurahii wenzao wanapoinuliwa kwa huruma ya Mungu. Hao nao wanapaswa kufuatwa, na kuonjeshwa huruma ya Mungu, ili waguswe na furaha za jirani zao, na pia wajali na kuguswa na vilio na mahangaiko ya jirani zao. Zaidi, anakaza kusema Baba Mtakatifu, mapadre wajibidishe kuhubiri huruma ya Mungu, na wawavute kwa ushawishi wa huruma, kondoo wale wanaotangatanga.

Baba Mtakatifu anaendelea kusema “ujumbe wa huruma umfikie kila mmoja, na pasiwepo mtu mwenye kuipatia kisogo huruma ya Mungu”.  Anasema tena “ninaelekeza ujumbe huu wa wongofu hata kwa wale ambao tabia zao zinawaweka mbali na neema ya Mungu. Ninawatazama haswa waume kwa wake ambao wanajihusisha na vikundi vya kigaidi. Kwa ajili ya usitawi wao wenyewe, ninawaomba wabadili mwenendo wao. Ninawaomba hili kwa Jina la Mwana wa Mungu ambaye pamoja na kuikataa dhambi, kamwe hakumkataa mdhambi”

Baba Mtakatifu anaendelea kutuasa kwamba tusidondoke katika mtego wa kufikiri kwamba  maisha hutegemea pesa na kwamba bila pesa hakuna chenye thamani. Dhana hiyo si mali kitu, bali ni uzushi mtupu! Hatutakwenda na fedha katika maisha yajayo. Fedha haituletei furaha. Ugaidi unaoendeshwa huko na huko kwa lengo la kujipatia utajiri ulioloweshwa damu, haumfanyi mtu yeyote kuwa mwenye nguvu zaidi wala kuwa ni wa milele. Kila mmoja,  leo au kesho atawajibika mbele ya hukumu ya Mungu ambayo hakuna awezaye kuikwepa.

Mwaliko huohuo uwaendee pia wale wote ambao wanaendekeza au wanajihusisha na ufisadi na rushwa. Donda hili katika jamii  ni dhambi kubwa inayolia mbinguni, kwa sababu inatishia maisha binafsi na yale ya kijamii. Rushwa inatuzuia tusiutazame wakati ujao kwa matumaini kwa sababu mfumo wake kandamizi unazima mipango ya wanyonge na unawakandamiza zaidi masikini wa masikini.

Ni uovu unaojifumbata katika matendo ya kila siku, na unasambaa na kusababisha kashfa ya hadhara. Rushwa ni dhambi ya kugumisha mioyo ambayo inaweka pesa mbele badala ya Mungu. Inaifanya pesa kuwa ina nguvu zaidi kuliko Mungu. Ni kazi ya giza hiyo, iliyojaa mashaka tele na udhalimu. Mtakatifu Gregory kwa sababu halali alisema, hakuna hata mmoja anayeweza kudhani kwamba  yuko salama na amekingwa na kishawishi hiki. Kama tunataka kukiondoa kutoka katika maisha yetu binafsi au yale ya kijamii, tunahitaji busara, uangalifu, uwazi, pamoja na ujasiri wa kuacha matendo maovu.

Kama rushwa na ufisadi haupigwi vita waziwazi, punde si punde kila mtu atakuwa mtekelezaji wa dhambi hii, na tutaishia kuangamiza hata uwepo wetu sisi wenyewe. Baba Mtakatifu anakaza kusema “huu ni wakati mwafaka wa kubadili maisha yetu! Huu ni wakati wa kuruhusu mioyo yetu iguswe! Tunapokabiliwa na matendo mabaya, hata mbele ya makosa makubwa zaidi, ni wakati wa kusikiliza kilio cha wanyonge wanaodhulumiwa mali zao, thamani yao kama binadamu, hisia zao, na hata maisha yao pia. Kung’angania tu maisha ya dhambi kutatuacha tukiwa tumedhalilishwa na tutabaki na huzuni.

Baba Mtakatifu anasema, “Maisha ya kweli ni kitu tofauti kabisa. Mungu hachoki kutufikia sisi. Daima yu tayari kutusikiliza, kama nifanyavyo mimi, pamoja na maaskofu wenzangu na mapadre”. Kinachompasa kila mmoja ni kukubali mwaliko wa wongofu na kuwa tayari kujiweka chini ya haki katika kipindi hiki cha huruma tunachopewa na Kanisa”.

Mpendwa Msikilizaji, hadi hapo tunatia nanga kwa tafakari yetu kwa siku ya leo. Tusikilizane tena kipindi kijacho. Kutoka katika Studio za Radio Vatican ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.