2015-08-02 12:15:00

Leo Yesu anatembeza mkwara mzito! Amua! Kusuka au kunyoa!


Katika tafakari ya Jumapili ya 21 ya Mwaka B wa Kanisa tunaongozwa na Injili kama ilivyoandikwa na Mtakatifu Yohane. Yoh. 6: 60-69. Waswahili wanasema unaposhikwa, shikamana hadi kieleweke! Maamuzi magumu ni hali ambayo mtu analazimika kuchagua au kuacha au kufanya tendo fulani. Mathalani, kuacha dini moja uliyozaliwa nayo na kuingia dini nyingine, yatakiwa kufanya maamuzi magumu. Wengine yawabidi kutoa maamuzi magumu katika siasa, katika kazi fulani, katika wito wa ndoa, upadre, utawa nk. “Ni hiari yako kusuka au kunyoa.” Waswahili wanasema hapo wewe utajiju!

Leo tutakutana na wanafunzi wa Yesu wanaotakiwa kutoa uamuzi mgumu wa maisha. “Watu wengi miongoni mwa wanafunzi wa Yesu waliposikia, walisema, Neno hili ni gumu, ni nani awezaye kulisikia?” (Yoh. 6:60). Hadi sasa wahusika wamekuwa Wayahudi wakinung’unika, halafu wakipishana mawazo kutokana na ujumbe wa Yesu. Kumbe wahusika wakuu wa leo ni wanafunzi wa Yesu. Hoja ya kubadili wahusika ni ya kichungaji. Mwinjili anaonesha mtazamo wa wale walioshuhudia ishara ile ya mkate, kuwa ni kiini cha mgogoro wa uwajibikaji wa wanafunzi kwa mwalimu wao.

Huo ni mwaliko pia kwa waamini wengine wanapotakiwa kutoa maamuzi magumu ya uwajibikaji juu ya wanachokiamini na kukifuata katika maisha. Ama kweli kazi nzito katika maisha ni kufanya maamuzi. Wanafunzi wa Yesu walishuhudia ishara ya mikate na waliyafuatilia mahubiri yote ya Yesu. Kwa vyovyote mwanzoni kulikuwa na sintofahamu, kwa sababu walidhani Yesu anamaanisha kula kweli nyama ya mtu. Lakini baadaye wakatambua alimaanisha: “kuunganisha maisha yao na ya Yesu,” yaani kutoa maamuzi ya kuendelea kujiaminisha kwa Yesu au kuhama chama chake. Huo ni uchaguzi wa akili unaodai kuelewa na wa moyo unaodai kupenda. Yesu alishajua ugumu huo wanaouona wanafunzi wake.

Hivi kabla ya kulijibu sisi swali lao, tuangalie kwanza Yesu mwenyewe anavyolikabili: “Naye Yesu akafahamu nafsini mwake ya kuwa wanafunzi wake wanalinung’unikia neno hilo. Akawauliza: Je, neno hili linawakwaza?” (Yoh. 6:61). Hapa kukwaza kuna maana ya kushangaa au kushtuka. Halafu anaendelea kuwakatisha tamaa anaposema: “Itakuwaje basi, mmwonapo Mwana wa Adamu akipaa huko alikokuwako kwanza?” (Yoh. 6:62) kwa maneno mengine: ‘Endapo sasa mnaona ugumu kupokea mapendekezo yangu pindi niko pamoja nanyi, je, mambo yatakuwaje nitakapokuwa nimerudi kwa Baba nilikotoka?”

Kwa vyovyote mtahitajika kuwa na imani kali zaidi, yaani mtahitaji imani ile isiyotegemea kuniona mimi kimwili, bali inayotegemea alama za kisakramenti. Kwa hiyo anawahimiza na kuwatia nguvu. Ili kuwa na imani hiyo kubwa zaidi, wanafunzi wanaalikwa kuachana na ulimwengu huu wa mwili, (mali) na kuingia katika ulimwengu wa kiroho. “Roho ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu. Maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena ni uzima” kwa yule anayetaka kuelewa ujumbe wa Kiinjili. Hekima ya kibinadamu na ya duniani haisaidii kukuelewesha mafumbo ya Mungu: “Basi mwanadamu wa tabia ya asili hayapokei mambo ya Roho wa Mungu; maana kwake huyo ni upuzi, wala hawezi kuyafahamu, kwa kuwa yatambulikana kwa jinsi ya rohoni” (IKor. 2:14). Kwa hiyo ukitegemea hekima ya kibinadamu utashindwa kutoa maamuzi magumu: “Kwa ajili ya hayo wengi miongoni mwa wanafunzi wake wakarejea nyuma, wasiandamane naye tena.” (Yoh. 6: 66).

Lakini wanafunzi waliomkacha Yesu haina maana ni wabaya, wasaliti au wahaini, la hasha bali siyo wadumifu watu wanaoweza kuvumilia patashika nguo kuchanika katika maisha!. Wameona Bwana kuwa anawadai zaidi ya uwezo wao. Kumbe, Yesu anaheshimu uhuru wao, hamlazimishi yeyote kuafikiana naye, hamlazimishi yeyote “kula nyama yake”. Migomo haimjalishi Yesu kwani ameshakuwa na mang’amuzi ya wengi wanaoshindwa kutoa maamuzi magumu na wameachana njia kutokana na misimamo na kauli zake nzito. Kwa mfano, kauli aliyotoa kwa yule kijana tajiri: “Nenda kauze kila ulicho nacho na uwape maskini” (Mt. 19:21). Kijana aliondoka bila kuaga, amekunja ndita!. Halafu kauli ya Mlimani: “mgeuzie adui wako shavu la pili, mpende adui yako” (Mt. 5:39-44); Usamehe saba mara sabini (Mt. 18:22).  Ama kweli hata sisi tunaweza kusema kama wanafunzi: “Neno hili ni gumu!”

Lakini anachotuelekeza Yesu sasa, siyo mambo ya maadili yaliyo magumu kuyafuata, la hasha! Bali anatupa mtazamo wa kimapinduzi zaidi katika maisha, yaani imani iliyo ngumu zaidi kuielewa na kuifuata: “Mimi ni mkate wa Mungu, mimi ninatoa maisha ya Mungu, nyama yangu inaleta uzima na maisha ya milele duniani.” Hapa ieleweke kwamba, hadi sasa hajawahi kutokea na hatatokea kamwe  mtu kusema kwa mkazo na kwa uhakika na mamlaka, “Mimi natoka mbinguni” na kuongea hivyo juu ya Mungu kama alivyofanya Yesu. Kwamba Yesu ni Mungu asiyemwaga damu ya wengine, bali yeye anamwaga damu yake, ni Mungu anayeenda kufa kwa ajili ya upendo; Mungu anayekuwa mdogo kama mkate na kujifanya chakula kwa ajili ya binadamu.

Ndugu zangu, dini ya Yesu siyo ya madhehebu, yenye madai magumu, la hasha bali ni dini ya muungano wa binadamu na Mungu, yaani wewe na yeye mnaungana na mnakuwa kitu kimoja hadi kieleweke. Kwa vyovyote yaonekana Yesu amehadaika na kudanganyika kidogo kutokana na umati ule mkubwa uliomshabikia mwanzoni na sasa wengi wamemkacha. Hata hivyo anatambua wazi kuwa imani haitegemei ushabiki na kushangiliwa bali kumfuata unayempenda. Aidha hashangai kuona kwamba kufuata huko hata kama ni wachache, kunaweza kuwa kwa mashaka, manung’uniko, mshangao na kusitasita.

Kimebaki kikundi kidogo hata kama hakielewi kinahitaji nini kutoka kwa Yesu lakini kinamfuata tu kimamuma. Ingawaje Yesu anahuzunika, lakini anatambua mgogoro na changamoto nyingi katika kutoa maamuzi ya kumfuata, lakini ameacha pia mwanya wa uhuru. Kwa vyovyote Yesu hakulazimishi kufanya unachotaka, wala hakuchagulii unavyotakiwa kuwa, bali anakutaka ujiangalie na kujihoji mwenyewe ndani mwako, kama vile angesema: “Mpo huru, nendeni mchague kadiri ya dhamiri yenu inavyowasukuma.” Hivi ndivyo anavyowahoji mitume: “Je, ninyi nanyi mwataka kuondoka?” Hata mimi nimeitwa kutoa “uamuzi mgumu,” kubaki na Kristo au kumwacha.

Jibu la Petro ndiyo uamuzi magumu anaofanya kwa niaba ya mitume na wafuasi wote wa Kristo: “Bwana, twende kwa nani? Wewe peke yako  una maneno ya uzima.” Katika Kristo kuna umaana wa imani. “Wewe peke yako.” Sina mwingine bora zaidi yako. Kwa sababu “Wewe peke yako una maneno ya uzima”. Kumbe Mungu anaongea, mbingu siyo kitu tupu na siyo bubu. Mbinguni kuna Neno sufufu linaloumba, kuna Neno linaloviringisha jiwe la kaburini na kufufua. Hii ni imani ambayo Kristu anaisubiri toka kwetu. “Wewe peke yako una neno la uzima.” Maneno yanayoleta uhai na uzima kila sehemu ya mimi, hutoa uhai katika moyo, hupanua, husafisha moyo na kulainisha ugumu wa moyo.

Maneno yanayoleta uhai akilini, kwa vile akili huishi katika uhuru. Maneno yanaleta maisha kwenye roho, sehemu ya kimungu iliyo katika mimi. Maneno yanayoleta uhai hata kwenye mwili, kwa vile katika yeye tumo, tunaishi na kupumua (Mdo 17:28); akiondoa pumzi mara moja tunakuwa mavumbi (Zab. 146:4). Maneno ya uzima wa milele, hayo huumba vitu vinavyotufanya tusife, hutengeneza umilele na kila kitu chema kilicho moyoni. Ama kweli “Neno la Mungu hufanya kazi kwenu mnaosadiki.” (I Tess 2:13). Mimi ninauchukua uamuzi mgumu wa Petro na kuugeuza kuwa wangu tena uamuzi wa upendo: “Mimi ninakuchagua wewe, kwa vile wewe peke yako una maneno yaletayo uzima na maisha yangu.”

Baada ya kutoa uamuzi huo mgumu nabakiwa na swali moja la msingi: “Ni nani anayestahili kuingia kwenye tafrija ya Ekaristi yaani ni nani basi anayeweza kupokea komunio?” Kama Ekaristi ni tuzo na mshahara kwa wenye haki, basi kwa vyovyote hakuna anayestahili kumpokea. Kumbe, Yesu siyo mkate wa Malaika bali ni chakula kilichotolewa kwa wanadamu tulio wasafiri hapa duniani, kwa sisi tulio wadhambi, wadhaifu, waliochoka, wahitaji na walalahoi kama Yesu alivyosema siku ya karamu ya mwisho: “Kunyweni nyote, kwa maana hii ndiyo damu yangu ya Agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi (Mt. 26:27-28). Kwa hiyo Ekaristi siyo kwa ajili wasafi na watakatifu, bali ni kwa ajili ya wakosefu ili wapate msamaha  na maondoleo ya dhambi toka kwa Mungu.

Anayepokea Ekaristi Takatifu haulizwi maadili yake, bali hali yake ya kifukara, yule anayejitambua kutokufaa kwake, uovu wake, na amkaribie yeye anayeweza kumponya. Toa uamuzi mgumu wa kupokea Ekaristi Takatifu kwa imani hii nyenyekevu, unyofu na toba ya ndani. Hapo Ekaristi takatifu itakuwa kwako dawa, uponyaji wa magonjwa ya kimaadili, uponyaji wa majeraha na madonda yote na utashinda kila dhambi, tayari kutoka kifua mbele kushuhudia utakatifu wa maisha!

Na Padre Alcuin Nyirenda.








All the contents on this site are copyrighted ©.