2015-08-02 07:49:00

Kimbilieni Sakramenti ya Upatanisho ili kuonja huruma na upendo wa Mungu!


Mpendwa Msikilizaji wa kipindi cha Hazina yetu, tumsifu Yesu Kristo. Tunakukaribisha tuendelee kuupitia Waraka wa Kichungaji wa Baba Mtakatifu Francisko Misericordiae vultus, maalumu kwa ajili  ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Kwa njia ya waraka huu, tunaandaliwa na tunaalikwa sisi wenyewe kujiandaa kiroho na kimwili katika kuuadhimisha mwaka huo Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu.

Ni mwaliko kwetu sisi sote kushiriki kikamilifu katika kuelewa maana, na kushishiriki katika maadhimisho yatakayopangwa kwa ngazi mbalimbali; huku tukijibidisha kutimiza kwa uwezo wetu wote yale ambayo Baba Mtakatifu anatuagiza yaani, kuyatekeleza matendo ya huruma ya kimwili na kiroho, kufanya toba, kusamehe, kuyasoma na kuyajifunza Maandiko Matakatifu na mambo mengi kama hayo.

Katika Kipindi Kilichopita tulimsikia Baba Mtakatifu, akituelekeza namna ya kuiishi Kwaresma ya mwaka ujao kwa ukamilifu wote ambapo pia twaalikwa kumwilisha matendo ya huruma, pamoja na Sakramenti ya Kitubio. Akitumia Mfano wa hadithi ya mwana mpotevu, anatualika sisi sote kuikimbilia Sakramanti ya Upatanisho, kwani kwa njia ya hiyo ndimo haswa tunarudishiwa neema za utakaso, uhuru, amani, furaha, na mfungamano wa kiimani na Kanisa, na zaidi pia mfungamano wa kijamii. Kwani kwa njia ya Sakramenti hii, hatujipatanishi na Mungu peke yake, bali pia twajipatanisha na binadamu wenzetu waliotukosea.

Itakumbukwa kwamba tafanusi ya Sakramenti ya upatanisho inatuelekeza kuelewa kwamba “ni mmoja kati ya Sakramenti saba  za Kanisa, ambapo waamini wadhambi, hutubu dhambi zao kwa Mungu, mbele ya mhudumu halali wa Sakramenti hiyo, nao kwa kuziungama dhambi zao kwa udhahiri na unyoofu wa moyo, husamehewa dhambi zao, na hivyo hapatanishwa na Mungu, na Kanisa ambalo wamelijeruhi kwa dhambi zao, na tena hupatanishwa na nafsi zao kwa kujaliwa amani ya kweli moyoni” (Rej. Kan. 959 – 969, CIC).

Tafanusi hiyo inatupatia mafaa ya Sakramenti ya Kitubio, ambayo Baba Mtakatifu anatuhimiza kuikimbilia kwa ujasiri, imani na matumaini kama alivyofanya yule mwana mpotevu. Baba Mtakatifu Francisko, akiielezea Sakramenti ya Upatanisho kwa mfumo wa Katekesi kamili; pamoja na neema zinazopatikana katika kuadhimisha Sakramenti hii, anaelekeza unadhifu wa kuiadhimisha kwa iwe kwa upande wa Muungamaji au kwa Muungamishi pia.

Anasisitiza zaidi Baba Mtakatifu “Kwa mara nyingine tena, na tuiweke Sakramenti ya Upatanisho kama kiini cha Maisha yetu, na hiyo itawasaidia watu kugusa ukuu wa Huruma ya Mungu kwa mikono yao wenyewe. Na kwa kila anayetubu, Sakramenti ya Upatanisho itakuwa kwake ni chemchemi ya amani ya kweli moyoni”.

Ndiyo maana kwa uzito huo Baba Mtakatifu Fransisko anawasisitiza waungamishi wawe ishara  halisi ya huruma ya  Baba; kwani kuwa waungamishi maana yake ni kushiriki katika utume wa Yesu mwenyewe wa kuwa Ishara wazi ya upendo wa daima wa kimungu, upendo wenye kusamehe na kuokoa.

Bado, anaendelea kusisitiza Baba Mtakatifu “katika kiti cha Kitubio, waungamishi wasiwe wanauliza maswali-maswali yasiyo na maana, wawe kama baba mwenye huruma katika mfano ule; aliyeikatikiza litania ya maelezo aliyoiandaa yule mwana mpotevu”. Hilo linaelekezwa pia na Taratibu Kanuni za Kanisa letu namba 979 CIC. Ni kwa njia hiyo waungamishaji watajifunza kupokea kilio cha msaada na toba kinachotoka katika moyo wa muungamaji. Kwa kifupi, Baba Mtakatitu anasema tena “hata iweje, waungamishi wameitwa kuwa ishara ya ukuu wa huruma ya Mungu daima na popote na katika hali zote,”!

Tusisahau pia kwamba, pamoja na unadhifu wa uadhimishaji wa Sakramenti hii, kuna wajibu pia wa kushika siri ya Kitubio. Hata iweje, Muungamishaji haruhusiwi kutoa siri ya kitubio, wala kutumia ufahamu wa jambo alilolisikia katika kitubio kwa namna yoyote ile iwe katika kuwafundishia, au kutolea ushahidi au kumpatiliza muungamaji (rej, Kan, 983 – 984 CIC). Sakramenti ya Kitubio ni Kiti cha Huruma ya Mungu, mahali ambapo moyo mnyonge na uliopondeka wa muumini mdhambi anayetubu anajipatanisha na Moyo wa Baba mwema mwingi wa Huruma. Mahali hapo Muungamaji anakutana ana kwa ana na Mungu, anajishitaki katika unyofu wa ndani, na hivyo kuiangukia na kuililia huruma ya Mungu.

Pamoja na kuelekezwa kuikimbilia Sakramenti hii, unyoofu wa muungamaji ndio unaofungua zaidi huruma ya Mungu. Yule mwana mpotevu ni unyoofu wake ulioonekana toka ndani hadi nje, ndio iliomfanya Baba mwema atoke, amkimbilie, amkumbatie, ambusu, amvike vazi safi, na viatu, na pete, na kumfanyia sherehe kuu, kwani kwa kurudi nyumbani kutubu, amefufuka, amekuwa mtu mpya, mwenye furaha na amani.

Sisi nasi waamini tujue kwamba, kwa unyoofu tunapaswa kuungama dhambi zetu. Tukificha dhambi zetum tunajidanganya wenyewe! Tukiungama kwa kupurukusha, tunajidanganya wenyewe! Tusipotimiza maelekezo tunayopewa kabla na baada ya kuungama, tunajidanganya wenyewe! Tusipoweka nia thabiti ya kubadili mwenendo wetu, tunajidanganya wenyewe! Zaidi ya hayo hata sisi waungamaji pia tunaalikwa kushika siri ya Kitubio. Yale tuliyoyaungama, na tuliyoelekezwa katika kiti cha Kitubio, sio adili kuyatangaza nje.

Mpendwa Msikilizaji, Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya Huruma ya Mungu huo, uko mbele yako. Tuwe tayari kuupokea, huku sisi wenyewe kwa unyofu tukiwa tayari kuguswa, kutakaswa, kufarijiwa na kukumbatiwa na huruma ya Mungu yenye nguvu ya kutufanya watu wapya rohoni na mwilini, na hivyo kuwezeshwa kuipeleka huruma hiyo kwa watu wengine.

Tusikilizane tena Kipindi kijacho. Kutoka katika Studio za Radio Vatican, ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.