2015-08-02 08:09:00

Katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu nitawatumieni Wamissionari wa huruma!


Mpendwa Msikilizaji wa Kipindi hiki cha Hazina yetu, Tumsifu Yesu Kristo. Kutoka katika Hazina ya Mama Kanisa kwa wakati huu tunakuletea uchambuzi wa barua ya Kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko inayotuandaa kuipokea na kuiishi Jubilei kuu ya Mwaka Mtakatifu wa Huruma ya Mungu. Ndani ya Waraka huu ya Kichungaji, pamoja na mambo mengine mengi, Baba Mtakatifu analialika Kanisa lote kurudi katika misingi yaani, kufundisha na kuuishi huruma ya Mungu. Sambamba na hilo kila mwamini na wote wenye mapenzi mema, wanaalikwa kujibidisha katika kuyamwilisha matendo ya huruma ya kiroho na kimwili.

Baba Mtakatifu ameelekeza jicho la pekee katika kipindi cha Kwaresma cha Mwaka 2016 ambapo tutakuwa ndani ya Mwaka mtakatifu wa Jubilei hiyo kuu ya Huruma ya Mungu. Pamoja na kuwaalika waamini wote katika unyofu wa kweli kuikimbilia Sakramenti ya Kitubio kwa mfano wa mwana yule mpotevu, anayesimuliwa katika Injili ya Mtakatifu Luka, aliyetambua udhaifu wake, na akayazingatia mahangaiko yake ambayo ni matokeo ya dhambi; na mwishoni kwa ujasiri mkubwa akafanya maamuzi ya kuondoka, kurudi kwa baba yake, na kwa unyoofu wote, kutubu yale yote aliyoyatenda. Hatua hii, ni kielelezo cha kilio cha kuomba huruma kutoka kwa huyu mwana mdhambi.

Na sisi, kila mmoja wetu, kwa kutambua udhaifu wetu mbele ya Mungu na mbele ya binadamu wenzetu, tunaalikwa kuzingatia moyoni, kuuvaa ujasiri, kurudi kutubu kwa Mungu wetu kwa njia ya Sakramenti ya Kitubio, ili Mungu nasi kisha kuguswa na unyoofu wetu na kilio cha nafsi yetu, atukimbilie, tendo linaloonesha anatutafuta, atukumbatie, tendo linaloonesha anatujali kama tulivyo, atubusu, tendo linaloonesha, anatupenda hata kama tu wakosefu; na hasa kama ni wakosefu tunaotubu, na atuvishe pete, tendo linaloonesha anaturudishia tena umoja na muungano naye na Kanisa,   na atuvike vazi, tendo linaloonesha kurudishiwa neema ya utakaso na atufanyie sherehe; tendo linalodhihirisha furaha kuu iliyopo Mbinguni pale ambapo tunatubu dhambi zetu kwa unyoofu.

Kwa mantiki fulani, Sakramenti ya Kitubio kwa namna yake huleta furaha, shangwe, hali njema, enzi mpya, amani na utulivu ndani ya Kanisa. Ndiyo maana Baba Mtakatifu anasema, katika mwaka huo Mtakatifu wa Jubilei kuu ya Huruma ya Mungu, anapenda Kanisa zima, tuiweke Sakramenti hii ya Upatanisho kuwa kama Nguzo msingi kabisa kwani ni kutoka humo twachota neema tele za huruma ya Mungu.

Katika Mwaka huo Mtakatifu wa Huruma ya Mungu, Baba Mtakatifu anadhamiria kuwatuma Wamisionari wa Huruma kila kona ya dunia. Hao watakuwa ishara ya Upendo wa Kimama wa Kanisa kwa watu wote wa Mungu, ambao watawasadia na kuwawezesha watu kuzama katika utajiri wa fumbo hili msingi la Imani yetu.

Anasema Baba Mtaktifu “Nina dhamiria kuwatuma Wamisionari wa Huruma. Kutakuwa na Mapadre ambao nitawapa ruhusa na mamlaka ya kuondolea dhambi hata zile zinazoondolewa na  Kiti Kitakatifu peke yake”.  Mapadre hawa watakuwa Ishara hai ya utayari wa Baba wa kuwapokea wale wote wanaotafuta msamaha na huruma yake. Mapadre hawa watakuwa ni wamisionari wa hurma kwa sababu watakuwa wawezeshaji wa binadamu kukutana; mapadre hawa watakuwa pia chanzo cha ukombozi wenye kuwawezesha waamini kuvuka vikwazo vya maisha ya kiroho ili waweze kutwaa tena maisha mapya ya ubatizo.

Katika umisionari wao mapadre hao wataongozwa na maneno ya Mtume Paulo asemapo “Maana Mungu amewafunga wote pamoja katika kuasi ili awarehemu wote (Rum 11:32).Na kutoka katika Waraka kwa Waebrania anasema: hivyo ilimpasa kufananishwa na ndugu zake katika mambo yote, apate kuwa kuhani mkuu mwenye rehema, mwaminifu katika mambo ya Mungu, ili afanye suluhu kwa dhambi za watu wake (Ebr 2:17).

Anendelea kusema Baba Mtakatifu “Ninawaomba Kaka zangu Maaskofu, kuwaalika na kuwapokea wamisionari hao ili zaidi ya yote wawe wahubiri-washawishi wa huruma. Kila Jimbo liandae  utume maalumu kwa ajili ya watu, ili wamisionari hawa wawe watangazaji wa furaha na msamaha. Maaskofu wanaombwa kuadhimisha sakramenti ya Upatanisho pamoja na watu wao ili wakati wa neema unaotolewa na Mwaka wa Jubilei, uwawezeshe watoto wengi zaidi wa Mungu, kuchota nguvu ya kusonga mbele katika safari yao ya kumwendea Mungu”.

Anaendelea kusema Baba Mtakatifu Francisko, Mapadre nao hasa kwa kipindi cha Kwaresma, wajibidishe sana kuwaita waamini, kwenye kiti cha neema, ili wapokee huruma ya Mungu na wapokee neema kama tunavyoalikwa na neno la Mungu katika Kitabu cha Waebrania asemapo  “Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji” (Ebr. 4:16).

Mpendwa Msikilizaji Mwaka Mtakatifu wa Jubilei Kuu ya Huruma ya Mungu, umesheheni mambo kemkem. Kuendelea kufahamu zaidi, endelea kuitegea sikio Radio Vatican. Kukuletea makala hizi, ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.