2015-08-02 09:44:00

Jiandaeni kufanya hija wakati wa maadhimisho wa Mwaka Mtakatifu


Mpendwa msikilizaji wa kipindi cha hazina yetu, tumsifu Yesu Kristo.  Tunaendelea kuupitia waraka wa Kichungaji wa baba Mtakatifu Francisko, Misericordiae vultus yaani uso wa huruma, tunapojiandaa kuuzindua mwaka wa mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu, hapo tarehe 08.12.2015.  Tusisahau kwamba, Jubilei yoyote ile hupambwa na matendo pamoja na matukio maalumu kama vile, sala za pekee, mafundisho maalumu, safari za hija na matendo ya kumbukumbu pia.

Tutakumbuka kwamba, pamoja na mambo mengine mengi ambayo Baba Mtakatifu ameyaangazia katika waraka huu, amegusia pia suala la kufanya hija; kwa kupita katika malango matakatifu kama ulivyo utamaduni wa hija katika Kanisa katoliki. Lakini si hivyo tu, bali pia kwa njia ya kushiriki katika hija katika vituo ambavyo vitakuwa vimeelekezwa na Mabaraza ya maaskofu au na Maaskofu Jimbo.

Ieleweke kwamba, hija ni safari takatifu, safari ya kiroho yenye kuonesha hamu ya kuuambata uongofu na kukuza utii wetu kwa Mungu. Hapa tunaitatakari hija katika sura ile ya Ibrahimu, babu wa Imani. Alifanya hija, huku akimtii Mwenyezi Mungu. Hadi hapo tunaweza kuelewa kuwa kuna hija kama tendo binafsi; ambapo mtu mwenye kumwamini Mungu, kwa kusukumwa na upendo kwa Mungu na hamu ya kuuambata uongofu zaidi, ananafanya safari takatifu kutoka nyumbani kwake kuelekea katika sehemu ya kiroho kadiri inavyoelekezwa. Hivyo hija, hudai kupanga, kujiandaa na kuondoka kutoka sehemu mmoja hadi nyingine. Lazima iwe safari.

Katika hija hiyo, mwamini anafanya safari ya sala, sadaka, toba na majitoleo, huku akitafakati safari yake ya maisha ya hapa duniani; ambapo mwisho wake anatarajia kukutana na Mungu uso kwa uso. Hivyo hija yetu ambayo ni safari ya kiroho, safari ya uongofu, inachangia kwa namna ya pekee sana katika hija/safari yetu ya hapa duniani.

Pamoja na hija binafsi, yaani kama tendo la mtu binafsi kwa mwangwi wa hija ile ya Babu yetu Ibrahimu, kuna hija pia kama tendo la kijamii, kwa mfano wa Taifa la Israeli, lililotoka kwa mkono wa Musa na uongozi wa Mungu, kutoka katika nchi ya Misri na kuelekea katika Nchi ya Ahadi yaani Kanaan. Misri ni ishara ya utumwa na dhambi na Kanaan ni ishaara ya uhuru na utakatifu. Waana wa Israeli, miaka arobaini walikuwa katika safari hii, kurudi katika nchi waliyoahidiwa Abrahamu Isaka na Yakobo. Njiani walipata magumu mengi, hata kuna nyakati walikata tama, lakini kwa njia ya viongozi wao Mungu aliwaongoza hata wakafika salama katika nchi ya ahadi.

Katika magumu yao walisaidiana, walitegemezana, waliinuana; na kwa njia hiyo walijenga zaidi umoja kati yao, na wakajijenga kama taifa mmoja, chini ya Mkono wa Mungu ambaye daima alitenda kati yao kwa njia ya moja kwa moja na kwa njia ya manabii wake.

Na sisi pia, katika Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu, tunaalikwa na Baba Mtakatifu Francisko kufanya hija. Hija hizo zaweza kuwa za mtu binafsi au za kijumuia, yaani makundi ya watu kadiri ya taratibu zitakazopangwa. Mafundisho ya imani yetu yanatuelekeza kwamba, Kanisa letu lililo Moja Takatifu Katoliki na la Mitume, lipo katika sehemu tatu yaani, Kanisa la Mbinguni yaani jumuiya ya Watakatifu, Kanisa la toharani yaani wale wanaotakaswa, na Kanisa linalohiji au Kanisa linalosafiri hapa duniani, ambao ni sisi.

Kwa mantiki hiyo, hija katika makundi ni mfano wa Kanisa linalohiji, ambamo waamini wanasafiri kuelekea ukomo wao yaani kukutana na Mungu. Katika hija hii waamini wanalishwa kwa neno na Sakramenti; wanapatiwa misaada mbalimbali ya kiroho na kimwili, huku wao wenyewe wakijibidisha kujenga umoja kati yao, wakisaidiana na kufarijiana, wakitiana moyo na kuinuana ili wasafiri salama na wakafike katika bandari salama ya uzima mpya. Hivyo, hija katika makundi ikatukumbushe mantiki hii; na ndiyo maana tunaalikwa kufanya maandalizi, na kutimiza vema masharti yote ya hija kadiri tunavyoelekezwa na mama Kanisa.

Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya Huruma ya Mungu ni mwaka wa hija. Lakini ikumbukwe kwamba, maisha mazima ya Mkristo, ni hija. Mkristo hapa duniani ni mhaji, anayesafiri kwenda kwa Baba. Na katika mwaka huo wa Jubilei yule atakayetimiza vema masharti yatakayowekwa na Kanisa mintarafu hija, atajaaliwa rehema Kamili.

Mpendwa msikilizaji, usikose kusikiliza na kusoma makala hizi kutoka kwenye tovuti ya Radio Vatican kipindi kijacho muda Kama huu, ambapo tutaangazia suala la Rehema Kamili katika mwaka wa Jubilei. Kutoka katika Studio za Radio Vatican, ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.