2015-08-02 09:04:00

Huruma ya Mungu inampatia mwamini nafasi ya kuanza upya!


Mpendwa Msikilizaji wa kipindi cha hazina yetu, tunakusalimu kutoka Studio za Radio Vatican, huku tukikutakia usilikizaji mwema wa makala hizi kutoka katika Hazina ya Mama Kanisa, ambapo kwa wakati huu tunaupitia waraka wa  kichungaji wa Baba Mtakatifu Francisko maarufu kwa jina la Misericordiae vultus, maalumu kwa ajili ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu.

Katika kipindi kilichopita Baba Mtakatifu alitutafakarisha juu ya kuoanisha Haki  na huruma. Mshairi mmoja aliwahi kusema ‘haki bila huruma yaweza kuzaa ukatiri wa hali ya juu’. Leo kwa mwangwi wa mafundisho ya Kristo tunasema, haki na huruma huzaa upendo wa kweli. Mara nyingi katika jamii zetu za leo, kumekuwa na mkazo mkubwa juu ya haki ambayo inajengwa katika ufuatajiwa sheria, tena hata sheria kandamizi ambazo kamwe haziheshimu wala kujali utu na thamani ya Binadamu.

Akiweka msingi katika mafundisho na matendo ya Kristo Mwenye, Baba Mtakatifu anatualika sana kuishi haki katika huruma. Ni kwa njia hiyo tu, tutaweza kumwilisha upendo, ambao ni amri kuu. Si mara chache katika mahusiano jamii, iwe ndani ya familia au katika makundi jamii, tumefukuza upendo, kwa sababu tu ya kulazimisha haki pasipokuwa na hata chembe ya huruma yenye kumtazama mtu katika uhalisia wake. Hakika kwa njia ya haki yenye huruma, tutaweza kuusistawisha upendo wa kweli. Haki ikisimama peke yake tu, huwa ni nyenzo dhalimu kwa mafaa ya wachache na uangamizi wa wengi.

Mtume Paulo, kwa kutekeleza haki, alipita katika mapito yayo hayo. Kabla ya kukutana na Yesu akiwa njiani kuelekea Damasko, alijitoa mhanga kulinda na kutetea haki ya Sheria kwa nguvu zake zote (rej, Fil. 3:6). Kwa tendo la kumwongokea Kristo kulimfanya ageuze kabisa aina hii ya mtazamo, kiasi kwamba akaweza kuwaandikia Wagalatia “Tumemsadiki Yesu Kristo ili tuweze kuhesabiwa haki kwa imani katika Kristo, na siyo kwa kazi za sheria, kwa sababu kwa nguvu ya sheria, hakuna atakayeweza kuhesabiwa haki (2:6).

Hapa tunaona wazi kuwa, uelewa wa Paulo kuhusu haki umebadilika mara kabisa.  Sasa anaweka imani kwanza, na siyo haki. Wokovu hupatikana sio kwa njia ya kufuata sheria, bali kwa imani katika Yesu Kristo, ambaye kwa kifo chake na ufufuko wake, analeta wokovu  pamoja na huruma inayohesabia haki. Haki ya Mungu sasa inakuwa ni nguvu ya ukombozi kwa wale wanaoonewa na kongwa la utumwa wa dhambi na matokeo ya dhambi. Haki ya Mungu ni huruma yake (Zab 51:11-16).

Huruma haipingani na haki, bali inaonesha namna Mungu anavyomfikia mdhambi, akimjaalia nafasi nyingine tena ya kujiangalia mwenyewe, kuongoka na kuamini. Mang’amuzi ya nabii Hosea yanaweza kutusaidia kuona namna ambavyo huruma huizidi haki. Kipindi ambapo Nabii Hosea aliishi, kilikuwa ni mmoja ya nyakati tete sana katika historia ya Wayahudi.

Ufalme ulilegalega kiasi cha kuangamia kabisa; watu hawakuwa waaminifu kwa agano; walimwasi Mungu na wakaipoteza imani ya baba zao. Kadiri ya mantiki ya kibinadamu, ni halali kwa Mungu kufikiria kuwaachilia mbalia watu hawa ambao hawajawa waaminifu. Hawajalishika agano lake na hivyo wanastahili adhabu: kwa maneno mengine kuchukuliwa mateka na kutupwa utumwani. Maneno ya nabii yanathibitisha hilo asemapo “ Hawatarudi katika nchi ya Misri na Ashuri atakuwa mfalme wao, kwa sababu wamekataa kunirudia mimi” (Hos 11).

Na zaidi, baada ya sala yake ya haki, Nabii anabadilisha kabisa mafundisho yake na anadhihirisha taswira halisi ya Mungu, akisema “Nawezaje kukutupa ee Ephraim! Nitawezaje kukuacha ee Israeli! Nitawezaje kukufanya kama Edama! Nitawezaje kukutendea kama Zeboiim! Moyo wangu unaugua ndani yangu, huruma yangu inazidi kuwa nyingi na karimu. Sitatekeleza hasira yangu, sitamwangamiza tena Ephraim, kwa maana  mimi ni Mungu na wala si Mwanadamu, mtakatifu kati yenu, na sitakuja kuangamiza (Hos. 11:8-9).

Mtakatifu Augustino, akiyafafanua maandiko haya anasema “Ni rahisi zaidi kwa Mungu kuzuia hasira yake kuliko huruma” Yaani Mungu hawezi kuizuia huruma yake, bali anaweza kuizuia hasira yake. Na ndivyo ilivyo.  Hasira ya Mungu hudumu kitambo kidogo, lakini huruma yake ni ya milele.

Endapo Mungu angejali tu haki yake, hapo angeacha kuwa Mungu, na badala yake angekuwa tu kama wanadamu wanaopenda tu kuheshimu sheria. Lakini haki tu, haitoshi. Mang’amuzi yanaonesha kwamba, kuikimbilia haki peke yake hutupeleka katika uangamizi. Ndiyo maana Mungu anakwenda ng’ambo zaidi ya haki kwa njia ya huruma yake na msamaha wake.

Mpendwa msikilizaji, mwaliko endelevu hapa ni uleule, yaani, kuoanisha  haki na huruma. Haki bila huruma anakaza kusema Baba Mtakatifu, huzaa uharibifu. Haki yenye huruma ndiyo huzaa upendo, wenye kujenga, upendo wenye kumjali jirani, upendo wenye kupenda kutimiza wajibu, upendo unaofariji, unaoleta furaha na kujenga amani ya kweli. Huruma ni dawa kiboko kwa magonjwa yote na hasira, chuki, fitina, mifarakano na kila aina ya kinzani. Huruma ya Mungu inatupatia nafasi na muda wa kuanza upya, ili tuwe watu wema zaidi.

Tunakutakia usikilizaji na usomaji mwema wa makala zetu kutoka Studio za Radio Vatican. Kukuletea makala hizi ni Mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.