2015-08-02 11:28:00

Amewatibua nyongo, wanaunda kambi ya upinzani, ili kumwonesha cha mtema kuni!


Jumapili ya kumi na tisa ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa tunaongozwa na Injili kama ilivyoandikwa na Yohane. Yoh. 6:41-51: kabla ya kuendelea na mchapo ufuatao, ingekuwa vyema kama ungevipitia vifungu hivi vya Maandiko Matakatifu, ili uweze kufaidika na mdundo ufuatao!

Katika moja ya hotuba za Musisi na Baba wa Taifa la Tanzania, Mtumishi wa Mungu Mwalimu Julius Nyerere, aliwahi kusema: “Makaburu wa Afrika kusini walikuwa wanapingwa siyo sababu ya rangi yao, bali kutokana na ubaguzi wao. Makaburu wa Tanzania ni wale wanaojiita wazawa na wanabagua wengine. Hao ni makaburu tu, mimi siwaonei haya hata kidogo! Kwa sababu kama una mawazo yaleyale kama makaburu wa Afrika kusini ila tofauti yake wewe ni mweusi, wewe ni kaburu tu!” Katika Biblia kulikuwa na watu wenye tabia ya ubaguzi kama makaburu wa Afrika kusini, walijisikia kuwa bora na waliotosheka, hivi hawakutaka kabisa kupokea mabadiliko toka nje. Kabla ya kuwaona watu hao hebu tuangalie kwanza mazingira ya fasuli ya leo.

Jumapili iliyopita Yesu alihitimisha hotuba yake kwa kujitambulisha na kusema: “Mimi ndimi chakula cha uzima.” Tamko hilo liliwachefua nyongo Wayahudi. Gharama anayoanza kuilipa Yesu kwa lugha hiyo ni hii kwamba: “Wayahudi walimnung’unikia, kwa vile Yesu alisema: ‘Mimi ni chakula kilichoshuka kutoka mbinguni.’” (Yoh. 6:41). Neno hili “kunung’unika” kwa kigiriki egongyzon linamaanisha kukasirika, kuchukia, kutia mgomo, kupinga, kubagua, kutofautiana, kuhitilafiana nk. Katika kitabu cha Kutoka na cha Hesabu kumaanisha chuki na mgomo wa Wayahudi dhidi ya Mungu, Musa na Aroni. Kunung’unika huko maana yake ni kutafuta mashabiki wa kutengeneza kambi ya kumkataa Yesu ili kuendelea na fikra zako.

Yesu anajitambulisha kuwa ni mkate wa uzima ulioshuka kutoka mbinguni. Kwa Wayahudi mkate na maji ni alama ya Neno na Hekima (Torah), waliyofunuliwa moja kwa moja na Mungu toka mbinguni. Zawadi hiyo waliisherekea katika sikukuu iliyoitwa Sinkhata Tora yaani “Furaha ya Torah.” Siku hiyo Wayahudi walimshukuru Mungu wakisoma “Baraka ya Musa” (Walawi 23), kisha wanaume kwa wanawake walicheza na kubusu gombo la Torah. Namna hii ya kuisherehekea Torah kama chakula (mkate) unaiona pia kwa manabii. Mungu anamwambia nabii Ezekieli: “Mwanadamu, kula gombo hili, kisha enenda ukaseme na wana wa Israeli.” Basi nikafunua kinywa changu, naye akanilisha lile gombo. Akaniambia, “Mwanadamu, ulijaze tumbo lako kwa hili gombo nikupalo.” Ndipo nikalila, nalo kinywani mwangu lilikuwa tamu, kama utamu wa asali.” Akaniambia, “Mwanadamu, haya! Waendee wana wa Israeli, ukawaambie maneno yangu” (Ezekiel 3:1-4).

Bwana anamwalika nabii alicheue Neno hilo hadi libadilishe maisha yake  kisha akawaelezee watu wake. Nabii Yeremia anasema: “Maneno yako yalionekana, nami nikayala; na maneno yako yalikuwa ni furaha kwangu, na shangwe ya moyo wangu, maana nimeitwa kwa jina lako, Ee Bwana, Mungu wa majeshi.” (Yeremia 15:16). Neno na Hekima ya Mungu (Torah) ilibadili maisha ya Wayahudi na hawakuhitaji tena aina nyingine ya Neno. Kumbe Yesu anasema kuwa Neno (Torah) na Hekima hiyo ya Mungu imejimwilisha katika yeye, kiasi kwamba anayetaka kubadilika na kuwa mtu kweli, hahitaji kujilisha tena na kitabu cha Torah. Hapo Wayahudi wakamgomea na kumsanifu: “Huyu siye Yesu mwana wa Yusufu, ambaye twamjua babaye na mamaye? Anawezaje kusema “Nimeshuka kutoka mbinguni?”

Ndugu zangu dini mbalimbali zina mtazamo tofauti juu ya Neno na Hekima ya Mungu iliyofunuliwa kwa binadamu. Usipojua tofauti hizo utagombana na watu wa dini nyingine bila sababu. Mathalani, kuna tofauti kubwa ya kulitazama Neno hilo kati ya Wayahudi, Waislamu na Wakristu. Kwa Wayahudi Hekima ya Mungu imejimwilisha katika gombo la Torah. Kwa Waislamu Neno la Mungu limejimwilisha na kujikita katika kitabu cha Koran Tukufu. Katika Koran Tukufu neno hili “Kitabu” limeandikwa mara 230 likiwa na maana ya Neno Tukufu lililofunuliwa moja kwa moja na Allah mwenyewe. Kumbe kwa Wakristu Neno hilo limejimwilisha katika nafsi ya Yesu wa Nazareti na siyo katika kitabu (Biblia au Injili). Wakristu wanamwiga mtu Yesu na siyo kitabu cha Biblia Takatifu.

Kwa hiyo, ili kuupata vizuri zaidi ujumbe wa leo, ni budi pia kuwajua ni nani hawa ambao Yesu anawaita Wayahudi. Ndugu zangu tuko Kafarnaumu Galilea. Wakazi wake ni Wagalilea, lakini Yesu anawaita kuwa ni: “Wayahudi” akimaanisha wale wote wanaomchukia Yesu na sera zake. Kumbe Wayahudi wanaotajwa hapa wanaweza kuwa ni sisi yaani mimi na wewe. Yesu anatuonesha jinsi ya kumpambanua huyu Myahudi aliye ndani mwetu, kuwa ni wale wanaoukataa mkate wa uzima ambao ni Yesu na kung’ang’ania kujilisha na mkate usio na uzima. Yesu hawaonei haya, anawaita kuwa ni “Wayahudi tu!”

Kisha anasema: “Hakuna mtu awezaje kuja kwangu asipovutwa na Baba aliyenipeleka: nami nitamfufua siku ya mwisho.” akimaanisha kwamba, hali hiyo ya kuupokea mkate wa uzima ni zawadi itokayo kwa Mungu. Halafu anasema tena: “Na wote watakuwa wamefundishwa na Mungu,” yaani Mungu atakujaza nguvu ya Roho Mtakatifu ndani ya moyo wako uweze kupokea ujumbe wa  Yesu. Nguvu hiyo ya ndani (dhamiri) itakuonesha ukweli wa mafundisho ya Yesu. Mathalani unapoona mtu anaonewa, toka ndani ya moyo wako utatambua kuwa kweli mtu anaonewa na utamhurumia. Kadhalika utakapoambiwa usiwe mbinafsi bali fungua moyo wako kwa maskini, hapo toka ndani itafahamu kuwa huo ni ukweli. Wanapopiga kampeni juu ya ndoa ya jinsia moja, hapo sauti ya ndani itakuambia, “binadamu tumechemsha.”

Hadi hapa Yesu ameongea juu ya mkate wa uzima utokao mbinguni (Neno na Hekima) uliojimwilisha katika Yesu. Kama umemfuatilia vyema utagundua kwamba, toka mwanzo wa sura hii hadi hapa Yesu hajazungumza kabisa juu ya Ekaristi. Lakini sasa kutoka hapa Yesu anadokeza wazo kuu atakololipembua kinagaubaga wiki ijayo nalo ni: “Baba zenu waliila mana jangwani; wakafa. Hiki ni chakula kishukacho kutoka mbinguni, kwamba mtu akila wala asife.” Yesu anajilinganisha na mana ya jangwani ambayo iliwalisha Wayahudi kimwili (kibaolojia), hata hivyo wote wakafa, kumbe anayekula nafsi ya Kristu aliyeshuka toka mbinguni, huyo anao uzima udumuo (Zoé orion). 

Kutokana na maneno hayo Yesu anaanza kulidokeza wazo la Ekaristi kwa maneno yafuatayo atakayoanza nayo wiki ijayo: “Mimi ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni mtu akila chakula hiki, ataishi milele. Na chakula nitakachotoa mimi ni mwili wangu, kwa ajili ya uzima wa ulimwengu.” Kwa hiyo kutoka sasa neno “kuamini” lililokuwa linatamba katika fasuli hii linafifia, badala yake maneno yafuatayo ndiyo yanachukua ulingo: “kula” linatumika mara kumi na moja. “Kutafuna” mara nne, na “kunywa” mara tatu.

Maana yake, ukishaliamini Neno na Hekima iliyojimwilisha katika nafsi ya Yesu sasa huna budi kumla, kumtafuna na kumnywa kama alivyofanya kwenye karamu ya mwisho: “Alichukua mkate akawapa wafuasi wake akisema: twaeni mle nyote, huu ndiyo mwili wangu.” Yohane hasemi mwili bali anataja “nyama” kwa wababu nyama tunatafuna. Naye Neno alifanyika Nyama, akakaa kwetu” (Yoh 1:14). Kadiri ya watu wa Mashariki, “nyama” ni nafsi nzima ya mtu, uhai wake, udhaifu wake na hali yake ya kufa kama asemavyo mzaburi “mtu ni nini hata umwangalie, ni upepo tu unaofika na kutoka.”

Kula au kutafuna  nyama na kunywa damu ya Kristu siyo suala la kufanya madhehebu ya misa peke yake bali ni muunganiko unaodumu na unaoendelea, unaohusu kumpumua Kristu ndani yangu daima. Paulo anasema: “Katika yeye tumo, tunatembea na kupumua” (Mdo 17:28).

Ukiulisha ovyo mwili unapata utapiamlo na kudhoofika au utachika hadi kuwashangaza watu! Kadhalika mioyo na akili zetu yabidi zilishwe vizuri kwa upendo, ukarimu, haki na siyo kuulisha ovyo kwa ubinafsi, kutovumilia, woga, unafiki nk huo ndiyo utapiamlo wa kiroho na mbaya zaidi unaweza ukapata hata Ukimwi wa kiroho! Tusipompokea na kumwamini Kristo hapo tunakuwa Wayahudi tu. Tukimpokea bila kulingana naye tutapata utapio mlo. Lakini tukipokea mawazo ya Kiinjili, na kumfuata tutakuwa na afya ya mwili na roho na utachanua kama Mwerezi wa Lebanon. Tukijilisha na Kristo aliye Neno na Hekima tutabadilika fikra zetu, mioyo yetu, vionjo vyetu, na kuwa na upendo kama yeye.

Na Padre Alcuin Nyirenda OSB.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.