2015-08-01 16:13:00

Changamoto za malezi na makuzi ya watoto katika ulimwengu mamboleo!


Familia ni tabernakulo ya uhai wa mwanadamu ni mahali ambapo watoto wanaritishwa tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni. Ni shule ya malezi na makuzi bora; mahali pa kujifunza kusamehe na kusamehewa, kupenda na kupendwa. Familia ni kitalu cha haki, amani na upatanisho wa kweli; mahali ambapo watu wanajifunza kutaabikiana na kusumbukiana kwa hali na mali. Ni mahali muafaka pa kujifunza maisha ya Kisakramenti, Tafakari na Neno la Mungu na kuhakikisha kwamba, kweli imani inamwilishwa katika matendo.

Katika familia za Kikristo, baba na mama wanapaswa kuonesha upendo wa dhati, kwa kutangaza na kushuhudia Injili ya Familia inayoambata Injili ya uhai, zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, inayokwenda sanjari na malezi pamoja na makuzi ya watoto. Ni wajibu wa wazazi na walezi kuhakikisha kwamba, wanawafunda watoto wao katika maisha ya sala, kwa njia ya mifano na ushuhuda wa maisha yenye mvuto na mashiko, ili waweze kuvuta neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu katika maisha yao.

Katika mahojiano maalum na Radio Vatican, Ndugu Severini Kalonga mwamini mlei kutoka Jimbo kuu la Dodoma anakaza kusema, dhamana na utume wa familia ya Kikristo unajikita katika malezi, ambayo kimsingi ni shule ya kumfuasa Yesu Kristo. Familia ni kikolezo cha Uinjilishaji kwani kwa kujiinjilisha yenyewe inashiriki kikamilifu katika mchakato wa Uinjilishaji. Wazazi ni mashuhuda wa kwanza wa Injili ya Kristo.

Ndugu Kalonga anasema, watoto wanapaswa kusaidiwa kukua na kuimarika katika fadhila mbali mbali za Kikristo kwa njia ya mshikamano wa umoja, upendo na msamaha unaojikita katika maisha ya wazazi wenyewe. Watoto wajengewe utamaduni wa kushiriki katika sala, tafakari na maisha ya Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo ili kuwasaidia kumwilisha imani katika matendo tangu wakiwa wadogo.

Anasema, changamoto kubwa inayowakabili wazazi na walezi ni kutokana na pilika pilika za malimwengu kiasi kwamba, wakati mwingine wazazi hawana nafasi hata kidogo ya kukaa na watoto wao. Watoto nao kutokana na majukumu mbali mbali wanajikuta kwamba, wanapata muda kidogo sana wa kukutana na kuzungumza na wazazi wao. Kumbe, hapa kuna haja ya kuweka uhusiano mwema kati ya maisha ya kiroho na maisha ya kijamii, ili watoto waweze kuwa na malezi pamoja na makuzi bora: kiroho, kiutu, kijamii na kimataduni. Mambo yote haya ni muhimu katika ukuaji wa mtu mzima.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.