2015-07-31 11:55:00

Watanzania jengeni umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa!


Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam anawataka watanzania wakati huu wanapojiandaa kwa ajili ya mchakato wa uchaguzi mkuu, kuhakikisha kwamba, wanajenga na kudumisha misingi ya haki, amani, umoja na mshikamano wa kitaifa. Watanzania wajenge na kudumisha utamaduni wa majadiliano na kusikilizana hata katika tofauti zao za kidini, kiimani na kikabila, daima watoe kipaumbele cha kwanza kwa ustawi na maendeleo ya watanzania wengi.

Haki, amani na utulivu vikitawala katika mchakato mzima wa uchaguzi mkuu, Tanzania itaweza kupata kiongozi atakaliongoza taifa na kwamba, huyu atapaswa kupewa ushirikiano na watanzania wote. Watanzania wakati wa kupiga kura, wasiangalie sura ya mtu au chama chake; bali sifa na vigezo muhimu katika maisha yaani: watu wanaowajibika, waaminifu, waadilifu, wakweli na wachamungu. Watanzania wakiendekeza ukabila, udini, uchama na umajimbo, watatumbukia mahali pabaya.

Kardinali Pengo ameyasema haya wakati wa mahojiano maalum na “Tumaini Media” wakati huu anapojiandaa kuadhimisha miaka 71 tangu alipozaliwa, yaani hapo tarehe 5 Agosti 2015. Amekwishalihudumia Jimbo kuu la Dar es Salaam kwa miaka 23. Alipokea Jimbo kuu la Dar es Salaam likiwa na Parokia 20 tu, lakini leo hii kuna Parokia 89 na lengo katika maisha na utume wake kama Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam ni kuwa na Parokia 100 ili kuweza kusogeza huduma za maisha ya kiroho kwa Familia ya Mungu Jimbo kuu la Dar es Salaam, tayari kutoka kimasomaso kutangaza na kushuhudia Injili ya furaha.

Kardinali Pengo anaendelea kuwahamasisha waamini wa Jimbo kuu la Dar es Salaam kujifunga kibwebwe ili kuweza kulitegemeza Jimbo lao kwa kuwa na rasilimali watu, yaani mihimili ya Uinjilishaji; rasilimali fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundo mbinu ya Uinjilishaji, kama vile Makanisa na nyumba za Mapadre pamoja na rasilimali vitu kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Jimbo.

Hizi ni juhudi zinazoonesha moyo wa kimissionari na uzalendo kwa kulipenda na kulisaidia Kanisa kutekeleza dhamana na wajibu wake wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Umefika wakati wa Familia ya Mungu Barani Afrika kulitegemeza Kanisa na kuachana na kasumba ya kuendelea kutegemea misaada kutoka ng’ambo, waamini wakiamua inawezekana kabisa kulitegemeza Kanisa. Kardinali anawapongeza sana waamini wa Jimbo kuu la Dar es Salaam ambao daima wamekuwa mstari wa mbele katika kulitegemeza Jimbo kuu kwa hali na mali.

Kardinali Pengo anasema, anapojiandaa kuadhimisha kumbu kumbu ya miaka 71 tangu alipozaliwa anamshukuru Mwenyezi Mungu pamoja na wazazi wake bila kuwasahau watu wote wenye mapenzi mema waliomsindikiza kwa sala, sadaka na majitoleo yao, hadi leo hii amefikia mahali hapa. Tangu akiwa kijana, alitamani kuwa Mhudumu wa Neno la Mungu, akawa na shauku ya kufuata na kuiga mfano wa maisha ya Mtakatifu Polycarp, Askofu na shahidi. Akasindikizwa kwa malezi na mifano bora ya maisha ya wazazi wake. Akabahatika kupata majiundo makini Seminari ndogo ya Kaengesa, Jimbo Katoliki la Sumbawanga na baadaye kwa masomo ya falsafa na taalimungu Seminari kuu ya Kipalapala, Jimbo kuu la Tabora, akapadrishwa kunako mwaka 1971 na baadaye kutumwa Roma kuendelea na masomo ya juu ya uzamivu katika maadili.

Kardinali Pengo anasema alipangiwa kufundisha Kipalapala na baadaye akautumwa kuanzisha Seminari kuu ya Segerea, iliyoko Jimbo kuu la Dar es Salaam. Kati ya wanafunzi wake ni Askofu mkuu Juda Thaddeus Ruwaichi wa Jimbo kuu la Mwanza, Askofu Almachius Rweyengeza wa Jimbo Katoliki la Kayanga, Askofu mkuu Beatus Kinyaiya wa Jimbo kuu la Dodoma, Askofu Ludovick Minde wa Jimbo Katoliki Kahama na Askofu msaidizi Titus Mdoe wa Jimbo kuu la Dar es Salaam.

Kardinali Pengo anapenda kuishukuru Familia ya Mungu Jimbo kuu la Dar es Salaam kwa juhudi wanazozifanya katika kukuza na kutegemeza miito mbali mbali ndani ya Kanisa. Miito ya Kipadre inaendelea kuongezeka siku hadi siku, jambo linalotia moyo na hamasa kubwa. Anawashukuru WAWATA kwa kuwalea na kuwaenzi waseminari kule Visiga. Ujenzi wa kidato cha tano na sita, unatarajiwa kuanza wakati wowote kuanzia sasa.

Kardinali Pengo anawashukuru na kuwapongeza Wanaume Wakatoliki Jimbo kuu la Dar es Salaam kwa kuwatunza na kuwaenzi watawa wa Shirika la Dada Wadogo, ili liendelee kutoa huduma kwa Familia ya Mungu, Jimbo kuu la Dar es Salaam. Kardinali Pengo anasema, kwa sasa anajivua kuona matunda ya Seminari ndogo ya visiga yakiendelea kukua na kushamiri.

Kati ya Mapadre kutoka Visiga anawakumbuka Padre Arister Makubi na Padre Joseph Peter Mosha ambao kwa sasa wako Roma kwa masomo ya juu, tayari kuchakarika katika mchakato wa Uinjilishaji wa Familia ya Mungu, Jimbo kuu la Dar es Salaam. Anasema, kuna idadi kubwa ya Mapadre wazalendo ambao wako na wanaendelea na masomo katika taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu ndani na nje ya Tanzania, lengo ni kuwaandaa wahudumu wa Injilitayari kukabiliana na changamoto za Uinjilishaji ndani na nje ya Tanzania.

Kardinali Pengo anawashukuru na kuwapongeza majandokasisi waliko kwenye Seminari kuu za Falsafa na Taalimungu na kuwataka kuwa na ari na moyo mkuu pasi na kukata wala kutatishwa tamaa, ingawa maisha na wito wa Upadre una changamoto zake.

Na John Liveti,

Jimbo kuu la Dar es Salaam.








All the contents on this site are copyrighted ©.