2015-07-31 08:16:00

Majandokasisi Seminarini wafundishwe matumizi ya njia za mawasiliano ya kijamii


Seminari ni kipindi cha malezi na majiundo makini ya maisha na wito wa kipadre. Huu ni muda wa kufanya maamuzi, malezi na maendeleo ya kiutu, kiroho na kimwili. Majandokasisi wanapaswa kutumia kwa busara muda huu ambao unatolewa kwa ajili yao kujijengea uwezo wa maisha ya kiroho na kiutu, ili wakitoka humo waweze baadaye kuchota kwa njia ya maisha ya kipadre. Huu ni mkazo unaotolewa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI katika Waraka wake wa kitume, Dhamana ya Afrika, Africae munus.

Mtakatifu Yohane Paulo II katika Waraka wake wa kitume, Kanisa Barani Afrika, “Ecclesia in Africa” anapenda kuihamasisha Familia ya Mungu Barani Afrika kuhakikisha kwamba, inatumia vyema njia za mawasiliano ya kijamii kama nyenzo ya kueneza Habari Njema ya wokovu. Njia za mawasiliano zinawaunganisha watu wengi, kiasi cha kuufanya ulimwengu kuwa kama kijiji. Familia ya Mungu Barani Afrika inakumbushwa kwamba, Kanisa linatumwa kutangaza na kushuhudia Injili inayookoa na kuponya.

Kwa kutambua umuhimu wa mawasiliano katika maisha na utume wa Kanisa, Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Kusini mwa Afrika, IMBISA, liliandaa semina maalum ya matumizi ya vyombo vya mawasiliano ya jamii. Mwezeshaji mkuu alikuwa ni Askofu Bernadin Mfumbusa wa Jimbo Katoliki Kondoa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Idara ya habari, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Semina hii iliongozwa na kauli mbiu “ Uinjilishaji katika ulimwengu wa digitali”.

Askofu Mfumbusa anakaza kusema, matumizi ya mawasiliano kwa njia ya digitali ni muhimu sana katika mapambazuko ya millenia ya tatu ya Ukristo na kwamba, Kanisa Barani Afrika linahamasishwa kuhakikisha kwamba, linatumia maendeleo ya sayansi na teknolojia ya habari kwa ajili ya kutangaza Habari Njema ya wokovu. Ili kufanikisha azma hii kuna haja kwa majandno kasisi kufundwa barabara, kama walivyokazia wajumbe wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Afrika Mashariki ya Kati, AMECEA katika mkutano wake wa kumi na nane uliofanyika nchini Malawi.

Kanisa halina budi kuendelea kushiriki katika mchakato wa Uinjilishaji kama sehemu ya utekelezaji wa agizo la Yesu Kristo kwenda duniani kote ilikutangaza Habari Njema ya wokovu, lakini kwa sasa Kanisa Barani Afrika halina budi kusoma alama za nyakati kwa kutumia nyenzo zinazokwenda na wakati. Kanisa halina budi kuhakikisha kwamba, linawapatia watu chakula cha uzima wa milele, vinginevyo mitandao mingi inaweza kujikita ikielea katika utupu, utakaojazwa na watumiaji wengine wa mitandao ya kijamii.

Askofu Mfumbusa anawaalika wasomi na wanazuoni Wakatoliki kuhakikisha kwamba, wanatumia vyema mitandao ya kijamii ili kuzima kiu na njaa ya watu wanaoishi kwenye ulimwengu wa mitandao ya kijamii. Mkazo huu pia umetolewa na Askofu mkuu William Slatter wa Jimbo kuu la Pretoria ambaye amewataka viongozi na walezi Seminarini kuhakikisha kwamba wanawafunda majandokasisi kutumia vyema njia za mawasiliano ya kijamii, tayari kushiriki katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Matumizi ya njia mpya za mawasiliano ya kijamii yataliwezesha Kanisa kusonga mbele katika maisha na utume wake, kwa kuwatangazia watu wa mataifa Injili ya furaha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.