2015-07-31 10:25:00

Lisaidieni Bara la Afrika kujikita katika mchakato wa haki, amani na upatanisho


Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM limezindua rasmi maadhimisho ya Mwaka wa Upatanisho Barani Afrika kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Padre Yves- Lucien Evaga Ndjana, Mkurugenzi wa utume wa Biblia Afrika na Madagascar, BICAM. Maadhimisho haya ni sehemu ya utekelezaji wa mchakato wa changamoto iliyotolewa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI, Dhamana ya Afrika, ili kuiwezesha Familia ya Mungu Barani Afrika kujikita katika mchakato wa haki, Amani na upatanisho.

Katika mahubiri yake, Padre Ndjana amekiri kukua na kukomaa kwa Kanisa Barani Afrika na kwamba, maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka 46 tangu kuanzishwa kwa SECAM ni fursa kwa Familia ya Mungu Barani Afrika kufanya tafakari ya kina kuhusu dhana ya Kanisa kama Familia ya Mungu inayowajibika. Huu ni mwaliko wa kutunza na kuiendeleza familia hii Barani Afrika.

Akizungumza na waamini waliohudhuria katika Ibada hii ya Misa Takatifu, Askofu mkuu Charles Palmer- Buckler wa Jimbo kuu la Accra, Ghana ambaye pia ni mtunza hazina wa SECAM, amewashukuru wajumbe wote walioitikia na hatimaye, kuhudhuria uzinduzi wa Maadhimisho ya Mwaka wa Upatanisho Barani Afrika. Hili limekuwa ni tukio la kumbu kumbu ya miaka 46 tangu kuzaliwa kwa SECAM. Amegusia kuhusu mchakato wa SECAM kuwa na mwakilishi wa kudumu kwenye Umoja wa Afrika.

Maadhimisho ya Mwaka wa Upatanisho Barani Afrika ni sehemu ya utekelezaji wa maazimio yaliyotolewa na Mababa wa Sinodi maalum ya Afrika, yakapewa kipaumbele cha pekee na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI katika Waraka wake wa Kichungaji, Dhamana ya Afrika na hatimaye, kuridhiwa na Baba Mtakatifu Francisko alipokutana na wajumbe wa SECAM, mwezi Februari, 2015.

Katika maadhimisho haya, SECAM itaendesha semina, warsha na makongamano maalum ili kukazia dhana ya haki, Amani na upatanisho; sanjari na majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kweli misingi ya haki, amani na upatanisho iwezi kusimikwa katika maisha na vipaumbele vya waamini. SECAM inawaalika viongozi wa Serikali na wadau mbali mbali kuhakikisha kwamba wanasaidia mchakato wa upatanisho na maridhiano Barani Afrika.

SECAM pia inaendea kujiandaa kikamilifu ili kushiriki katika maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia, itakayofanyika mjini Vatican kuanzia tarehe 4 hadi tarehe 25 Oktoba 2015, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Wito na utume wa familia ndani ya Kanisa na ulimwengu mamboleo”. SECAM inataka kushirikisha mchango wake, mintarafu changamoto za maisha na utume wa Familia Barani Afrika.

SECAM inawataka waamini Barani Afrika kujifunga kibwebwe ili kuiwezesha kutekeleza dhamana na wajibu wake, ili hatimaye, iweze kujitegemea kwa rasimali fedha na watu. Waamini waendelea kuwa kweli ni chumvi ya dunia na mwanga wa mataifa. Waamini wanasema, ikiwa kama kuna usimamizi wa kutosha, SECAM inaweza kuchangiwa sana, lakini lazima wawepe wahamasishaji watakaolisaidia Kanisa Barani Afrika kuweza kujitemea.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican kwa msaada wa CANAA.








All the contents on this site are copyrighted ©.