2015-07-30 07:24:00

Wazee wa Kanisa wanavyo chakarika kutumia njia za mawasiliano ya jamii!


 

Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 26 Julai 2015 mara baada ya tafakari ya Sala ya Malaika wa Bwana, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican alizindua rasmi mchakato wa vijana kujiandikisha katika maadhimisho ya Siku ya 31 ya Vijana Duniani, inayoongozwa na kauli mbiu “Heri wenye rehema maana hao wapata rehema”.

Maadhimisho haya yanakwenda sanjari na Mwaka mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Kumbe, hii itakuwa ni Jubilei ya Vijana Duniani itakayowasha moto wa huruma ya Mungu kuanzia tarehe 26 hadi tarehe 31 Julai 2016.

Saa chache tu baada ya Baba Mtakatifu kujiandikisha kwa njia mtandao kama hujaji kwenye maadhimisho haya, takwimu zinaonesha kwamba, zaidi ya vijana 45, 000 tayari wamekwisha kuchangamkia tukio hili kwa kujiandikisha. Haya ndiyo mambo ya maendeleo ya teknolojia ya habari na mawasiliano jamii. Ilikuwa ni tarehe 19 Novemba 2001, Mtakatifu Yohane Paulo II alipowatumia Maaskofu kutoka Oceania, Waraka wake wa kichungaji mara baada ya Sinodi ya Maaskofu wa Oceania, “Ecclesia in Oceania”, “Kanisa Oceania”.

Papa Yohane Paulo II wakati huo alianza pia kutumia Computer ya mkononi. Kwa Mapapa, huu ukawa pia ni mwanzo wa matumizi ya maendeleo ya sayansi ya teknolojia ya habari na mawasiliano, ili kuweza kuwafikia watu wengi zaidi kwa wakati muafaka. Tarehe 24 Machi 1997, Papa Yohane Paulo II alizindua tovuti ya Vatican inayokwenda kwa anuani ya: www.vaticana.va na baada ya muda si mrefu, tayari ikawa imetembelewa na mamillioni ya watu.

Tangu wakati huo, wachunguzi wa masuala ya maendeleo ya sayansi na teknolojia ya habari wanakiri kwamba, kumekuwepo na mabadiliko makubwa hadi wakati huu, tunapozungumzia teknolojia ya mawasiliano kwa mfumo wa digitali unaoweza kutumiwa na watu wengi zaidi hata kwa njia ya simu za viganjani. Hapa kwa hakika, njia za mawasiliano ya jamii zimeuwezesha ulimwengu kuwa kama kijiji; lakini bado kuna changamoto zake.

Baba Mtakatifu Francisko amezindua mchakato wa kujiandikisha kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, mwaka mmoja kuanzia sasa, maadhimisho ambayo yatafanyika Jimbo kuu la Cracovia, Poland. Ni tukio litakalowakusanya vijana wa kizazi kipya kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Baba Mtakatifu licha ya kuwa amezaliwa “enzi ya mawe” kama anavyokiri mwenyewe, lakini anapenda kuonesha uwepo wake wa karibu na vijana wa kizazi kipya.

Baba Mtakatifu ana upenda na kuuheshimu utamaduni wa digitali, ndiyo maana hana makuu anapoombwa na vijana kufanya “Selfies”. Hapa Baba Mtakatifu anaonesha umahiri wake katika medani ya mawasiliano ya jamii, si tu kwa kujadiliana na wasikilizaji wake, lakini hata kwa njia ya mawasiliano ya kisasa. Itakumbukwa kwamba, siku chache tu baada ya kuchaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki, kunako mwaka 2013, Baba Mtakatifu Francisko alizawadiwa “Tablet” wengine wanauita eti ubao wa kuandikia!

Baba Mtakatifu alifundishwa na vijana wawili namna ya kuutumia ubao huu wakati wa kuwasiliana na watu, kama ilivyo kwa tamaduni nyingi zinazojikita katika fasihi simulizi kuona wajukuu wanamzunguka Babu yao ili kupata simulizi mbali mbali. Hata leo hii vijana wa zamani wanapotaka kutumia computer au simu za kisasa wanalazimika kuomba ushauri kutoka kwa wajuu wao.

Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI alikuwa ni Papa wa kwanza kuanza kutumia “Tablet”, tarehe 12 Desemba 2012, akiwa amezungukwa na vijana wawili, mahiri katika matumizi ya mitandao ya kijamii, akazindua akaunti ya Papa inayojulikana kwa jina la @Pontifex. Leo hii akaunti hii ina wafuasi zaidi millioni 22, matendo makuu ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.