2015-07-30 15:26:00

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 18 ya Mwaka B wa Kanisa


Ni siku nyingine tena tunakutana kushirikishana kwa furaha Habari Njema ya wokovu. Ni Dominika ya 18 ya mwaka B. Mama Kanisa kama kawaida ametutayarishia chakula kizuri tukialikwa kumtambua Kristo aliye Mkate wa uzima, aliye mkate ushukao toka mbinguni ambao wote waulao hawataona njaa kamwe na badala yake watauona utukufu wa Mungu milele.

Katika somo la kwanza Wana wa Israeli wako njiani kuelekea katika nchi ya ahadi na kwa sababu ya kukata tamaa wanaanza kumnung’unikia Mungu wakisema kwanini mmetutoa huko Misri ambapo tuliketi karibu na masufuria ya nyama na kutuleta katika balaa hili la njaa? Swali hili au lalamiko hili ni alama ya ukosefu wa kumbukumbu ya shida zote walizokuwa wakizipata huko Misri na badala yake wanakumbuka tu nyama! Wanasahau kuwa walikuwa watumwa na hivi wanakosa shukrani na uvumilivu mbele ya Mungu. Pamoja na lalamiko hili bado mwenyezi Mungu ni huruma isiyopimika anawahaidi kuwapatia chakula, na hivi anamwambia Musa, nitawanyeshea mvua ya mkate kutoka mbinguni na hivi watapata kushiba kwa chakula hicho.

Mpendwa, tabia hii inayojitokeza kwa Wana wa Israeli hujitokeza kwetu katika siku zetu hizi. Wakati tulipopokea sakramenti ya ubatizo tulishangilia na kuanza safari yetu ya wokovu kwa furaha, lakini katikati ya maisha yetu ya imani wakati fulani tunajikuta katika kulalamika dhidi ya Kanisa na pengine dhidi ya Mungu. Utasikia watu wakisema oh mara Kanisa halifanyi hiki, oh mbona Kanisa limeweka sheria ngumu juu ya maisha ya ndoa! Haya yote ni malalamiko ambayo daima hayana tafakari ndani mwake bali usahaulifu juu ya wajibu wangu kama Mkristu. Ningependa kusema kuwa, ukristo si tu ubatizo bali kuishi ubatizo na kujua kuwa Kristu hakutukomboa kwa kazi lelemama bali kazi ya kujipinda mgongo mpaka kufa msalabani. Ndiyo kusema alifundisha kwa ujasiri, akadharauliwa lakini alikaza uso gumegume na kuelekea Yerusalemu kwa ajili yangu mimi ninayelalamika!

Mpendwa unayefuatilia na kutafakari nami, mwishoni tukumbuke kuwa, pamoja na malalamiko yangu dhidi ya Mungu, bado Mungu anipenda na kunikirimia chakula, maisha ya mbinguni kwa njia ya Kitubio na Ekaristi Takatifu, kama alivyowagawia manna wana wa Israeli kule jangwani. Hata hivyo ananidai kuwa na tumaini thabiti katika yeye kila kunapokucha akitaka niishi tumaini la ubatizo kila siku, kumbuka alipowapa chakula kule jangwani ilikuwa ni kwa ajili ya siku mojamoja, yaani isingewezekana kuokota kwa ajili ya siku inayofuata.

Katika barua ya Mtume Paulo kwa Waefeso, Mtume Paulo anawaalika Waefeso waenende katika maisha mapya na kuacha mambo ya zamani. Mtume Paulo anasema hili kwa sababu kuna kishawishi cha kutaka kurudia mambo ya zamani waliyoyaacha wakati walipopokea ubatizo. Rafiki yangu mpendwa, Mtume Paulo anatambua kuwa mtu akibatizwa anabadilika na kuwa kiumbe kipya na hivi anaunganika na Yesu Kristu, kumbe utendaji wake lazima uenende kadri ya mapenzi ya Bwana, ndiyo kusema kuachana na maisha ya dhambi na kuishi kitakatifu.

Katika sehemu ya Injili ya Mtataktifu Yohane tunapata kujifunza jinsi mwanadamu alivyo dhaifu, baada ya kuwa Bwana amewalisha wale watu 5000 kwa mikate 5 na  na samaki 2 watu wanamwona Bwana kama mtu wa miujiza na hivi wanataka kumfanya awe mfalme wa dunia! Kwa jinsi hiyo wanamtafuta na kumfuata. Yesu akigundua nia yao chafu anawaambia yafaa mkanitafute si kwa ajili ya chakula kishibishacho tumbo bali chakula chenye kudumu milele. Kumbe mwaliko ni kutambua kuwa Neno la Mungu yaani mafundisho ya Bwana ndiyo uzima tunaopaswa kuutafuta daima na si kumfanya Bwana mfalme wa dunia.

Mpendwa mwana wa Mungu, katika zama zetu hizi kuna hatari nyingi yaani kuna baadhi ya wenzetu ambao husali kwa ajili ya kuona matukio, maajabu na kama hayatokei basi hukimbia na kuhamia kwenye vijisinagogi vinavyosadikika kuwa maarufu katika kuondolea pepo!

Mpendwa Ukristo si dini ya miujiza na wala si dini ya raha na vionjo bari dini ya hekima na furaha iliyozama katika moyo wa mapendo ya Mungu. Ni dini inayotudai daima kutafakari kila tukio kwa furaha na kwa kina bila kukurupuka. Kumbuka Gamalieli alisema kama kweli yatoka kwa Mungu itadumu. Inatudai kutafakari tukiangalia historia ya wokovu na si vionjo vya sasa au kadiri ya maisha yangu mimi tu bali pia tukitazama Jumuiya ya Waamini.

Mpendwa unayenisikiliza, Bwana anatudai tumaini na kujiaminisha katika yeye pasipo kutafuta uhakika wa mambo yaani miujiza, ndiyo kusema imani katika Mwana wa Mungu tukiongozwa na Mama Kanisa ambaye amekabidhiwa wajibu wa kutunza na kuhakiki mapendo na imani ya waamini, kumbuka Bwana anamwambia Petro, Je, Petro wanipenda? Chunga kondoo wangu. Mwitiko wetu hivi leo uko katika Injili, tukisema Bwana siku zote utupe chakula hiki, Bwana siku zote utufundishe kuyashika mafundisho na mausia yako.

Mpendwa, nikuombee heri na neema za Mungu ili ukashike vema mwaliko wa Bwana kwa njia ya mafundisho yake na mwisho ukaurithi uzima wa milele.Tumsifu Yesu Kristo.

Tafakari hii imeletwa kwako na Pd Richard Tiganya C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.