2015-07-29 13:45:00

Familia imara ni msingi wa maadili na utu wema, Kanisa dogo la nyumbani!


Wazazi na walezi wamechangia kwa kiasi kikubwa katika mchakato wa watoto wao kuwa watu mashuhuri, wema, lakini zaidi watakatifu na mfano wa kuigwa na Jamii hata kwa nyakati hizi. Hivi ndivyo ilivyokuwa hata kwa Watakatifu Joakim na Anna wazazi wa Bikira Maria. Wao walisaidia sana kumfunda Maria, kiasi hata cha kupata upendeleo mbele ya Mwenyezi Mungu na hivyo kuteuliwa kuwa ni Mama wa Mungu na Kanisa.

Haya yamesemwa na Kardinali Joao Braz de Avis, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, wakati wa maadhimisho ya Siku kuu ya Mtakatifu Anna, Msimamizi wa Parokia ya Mtakatifu Anna iliyoko mjini Vatican, iliyoadhimishwa Kiparokia, Jumapili iliyopita, sanjari na Kumbu kumbu ya Watakatifu Joakim na Anna, wazazi wake Bikira Maria.

Ilikuwa ni fursa ya kuwaunganisha watawa mbali mbali wanaotoa huduma zao mjini Vatican, kama nafasi ya kumshukuru Mungu kwa ajili ya maadhimisho pia ya Mwaka wa Watawa Duniani pamoja na kuombea maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia itakayofanyika mjini Vatican kuanzia tarehe 4 hadi tarehe 25 Oktoba 2015 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Wito na utume wa familia ndani ya Kanisa na Ulimwengu mamboleo”.

Kardinali Braz de Avis anawataka watawa na waamini katika ujumla wao kurejea na kuambata mambo msingi katika maisha na utume wao; yaani Injili na Karama za waanzilishi wa Mashirika yao, tayari kujisadaka kwa ajili ya kushiriki kikamilifu katika mchakato wa Uinjilishaji mpya, unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko; watu wamechoka kusikia “longo longo kibao”.

Kwa upande wake, Kardinali Angelo Comastri, amepembua umuhimu wa dhamana na utume wa familia katika mchakato wa kuwafunda watoto malezi mema mintarafu tunu msingi za maisha ya Kikristo, kiutu na kijamii. Watoto wakibahatika kuambata utakatifu wa maisha, wazazi wanaweza kufaidika sana kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Teresa wa Lisieux, Mtakatifu Yohane Bosco na Mtakatifu Yohane XIII.

Padre Bruno Silvestrini, Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Anna amekazia kuhusu umuhimu wa Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani, kwa kujikita katika changamoto iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko anayewataka watawa kutafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini. Watawa wawe na ushuhuda wa kusimulia historia ya maisha yao pasi na ukakasi pamoja na kutoa utambulisho wenye mvuto na mashiko, kama ilivyo pia kwenye familia.

Watawa wanapoangalia yaliyopita, wanapaswa kuonesha moyo wa shukrani kwa Mwenyezi Mungu kutokana na yale aliyowakirimia na kuungama kwa moyo wa unyenyekevu mapungufu yao ya kibinadamu, ili kukimbilia wema na huruma ya Mungu katika hija ya maisha yao. Haya ni mambo msingi katika kumwilisha changamoto za maisha ya kitawa kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko: Watawa wawe ni mashuhuda wa furaha, wanaopaswa kuwaamsha walimwengu na kwamba, wajikite katika umoja na mshikamano, tayari kujifunga kibwebwe kwenda pembezoni mwa jamii kwa ajili ya kuwatangazia Watu wa Mataifa Injili ya furaha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.