2015-07-29 13:25:00

Askofu mkuu Kivuva anachambua dhana ya Upatanisho Barani Afrika


Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI katika Waraka wake wa kitume Dhamana ya Afrika, “Africae Munus analitaka Kanisa Barani Afrika kuwa ni mhudumu a upatanisho, haki na amani, kwa kuwataka waamini kuwa kweli ni chumvi ya dunia na mwanga wa mataifa katika kukuza na kudumisha mchakato wa upatanisho, haki na amani Barani Afrika.Mwaka huu unaadhimishwa na Familia ya Mungu Barani Afrika sanjari na Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu.

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagscar, SECAM, tarehe 29 Julai 2015 limeazindua rasmi maadhimisho ya Mwaka wa Upatanisho Barani Afrika kama sehemu ya maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka 47 tangu kuanzishwa kwa SECAM. Huu ni utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI kwa Kanisa Barani Afrika ili kuwa na siku maalum kwa ajili ya kuadhimisha mchakato wa upatanisho.

Katika mahojiano maalum na Radio Vatican, Askofu mkuu Martin Kivuva Musonde wa Jimbo kuu la Mombasa, Kenya anakazia umuhimu wa haki, amani na upatanisho Barani Afrika kama sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu kiroho na kimwili. Waamini wanakumbushwa kwamba upatanisho unapata chimbuko lake katika Fumbo la Pasaka, yaani katika mateso, kifo na ufufuko wa Kristo. Upatanisho ni sehemu kuu ya mafundisho ya Kristo kwa wafuasi wake, ili kukoleza zawadi ya amani na utulivu, chimbuko la maisha mapya.

Kwa namna ya pekee, waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanahamasishwa kuwa kweli ni wajumbe na vyombo vya upatanisho katika maisha yao, ili kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano. Ni mwaliko wa kujikita pia katika mchakato wa majadiliano ya kidini na kikabila ili amani na maridhiano yaweze kutawala katika maisha na vipaumbele vya watu. Kwa ufupi Askofu mkuu Kivuva anakaza kusema, Yesu Kristo ni kielelezo cha haki, amani na upatanisho. Upatanisho ni chimbuko la maisha mapya na kwamba, kamwe waamini wasitawaliwe na chuki wala kutaka kulipiza kisasi, daima watafute fursa za kujipatanisha, ili amani iweze kutawala.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.