2015-07-28 11:44:00

Upendo, haki na upatanisho ni mambo yanayoleta tofauti katika maisha!


Patriaki Louis Raphael Sako wa kwanza wa Baghdad ya Wacaldei, tarehe 27 Julai 2015 amepokea tuzo ya kimataifa kwa kutambua mchango wake katika kulinda na kutetea: tamaduni, mazingira na haki msingi za binadamu. Tuzo hii ya kimataifa hutolewa kila mwaka kwa mtu ambaye amejipambanua katika maeneo hayo kama ambayo imekuwa kwa Patriaki Louis Sako wa Baghdad.

Tuzo hii anasema anaipokea kwa heshima ya wananchi wa Iraq katika ujumla wao, watu wanaoendelea kuteseka na kunyanyasika; ni tuzo kwa heshima ya watu wanaosimama kidete kutafuta amani ya kudumu na maisha bora, ustawi na mafanikio ya wengi. Tukio hili limehudhuriwa na viongozi mbali mbali wa Kanisa na Serikali ya Italia, mabalozi pamoja na watu mashuhuri.

Patriaki Louis Sako anasema kunako mwaka 2003, Makanisa 62 yalishambuliwa na Wakristo 1264 wakauwawa kikatili. Hii ni Njia ya Msalaba ambayo imekuwa ni sehemu ya maisha yao ya kila siku. Kumekuwepo na utawala wa mabavu, litania ya vita na mauaji ya watu wasiokuwa na hatia; misimamo mikali ya kiimani ambayo kwa sasa imegeuka kuwa ni vitendo vya kigaidi, vinavyotishia usalama, maisha, maendeleo ya wengi na mafungamano ya kijamii.

Ni mauaji yanayofanywa kwa misingi ya kidini, jambo ambalo ni hatari sana na linapaswa kushughulikiwa kikamilifu na Jumuiya ya Kimataifa, ili watu waweze kujifunza kuheshimiana na kuthaminiana hata katika tofauti zao. Misimamo mikali ya kidini ni matokeo ya watu kutofahamu kwa kina imani na mafundisho ya dini zao, hapa kuna haja ya kuendeleza majadiliano ya kidini pamoja na kuwataka viongozi wa dini ya Kiislam kuhakikisha kwamba, wanawawezesha waamini wao kufahamu kweli na misingi ya dini ya Kiislam. Wananchi wote wawe na haki sawa pasi na upendeleo unaoweza kusababisha mpasuko wa kijamii na hali yakudhaniana vibaya.

Patriaki Louis Sako anakaza kusema, haki inakwenda sanjari na wajibu. Kwa Wakristo huko Mashariki ya Kati, kifodini ni sehemu ya vinasaba na karama ya Kanisa. Hii inatokana na ukweli kwamba, Wakristo wanakabiliwa na matatizo na changamoto nyingi zinazowataka kuwa kweli ni mashuhuda amini wa Kristo na Kanisa lake. Hapa imani na ushuhuda ni chanda na pete kama wanavyosema kwa Kiarabu “Shahidi wa shahadi”.

Wakristo wanauwawa kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, ushuhuda kwamba, imani kwa Wakristo si jambo linaloning’ia kifuani kama tai, bali ni sehemu ya maisha ya mwamini yanayojikita katika upendo unaobubujika kutoka katika undani wa mwamini aliyekutana na Yesu katika hija ya maisha yake. Hapa waamini wanahamasishwa kuonesha upendo wao kwa Kristo, hata ikiwa kama watatakiwa kutoa ushuhuda kwa njia ya maisha yao!

Wakristo wa Iraq wanatambua kwamba, Yesu anawapenda na anawapigania, kumbe wanapaswa kumwambata hata kama itawabidi kujisadaka. Wanapenda kubaki katika nchi yao, kwani hapa ni kiini cha historia na maisha yao. Wanatambua kwamba, wana wito, dhamana na utambulisho wanaopaswa kuutolea ushuhuda wa maisha kwa kuambata Injili ya furaha kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko.

Katika mapambano ya maisha, Wakristo wanatambua kwamba, nyuma yao kuna kundi kubwa la Wakristo wenzao kutoka sehemu mbali mbali za dunia, linalowasindikiza kwa njia ya sala na sadaka; kuna marafiki na watu wenye mapenzi mema wanaowatia shime kusonga mbele kwa imani na matumaini pasi na kukata tamaa, ili kujenga misingi ya maridhiano, haki, amani, upendo na mshikamano na waamini wa dini ya Kiislam, ambao daima wanakiri kwamba, Wakristo kweli ni tofauti kabisa na waamini wa dini nyingine, kwani wanaweza kupenda, kusamehe, kuwapokea wengine katika ukweli na uwazi na kuishi kwa amani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.