2015-07-28 11:12:00

Serikali ya umoja wa kitaifa inaweza kuwa ni suluhu ya mgogoro wa Burundi!


Bwana Agathon Rwasa mpinzani mkuu wa Serikali ya Burundi inayoongozwa na Rais Pierr Nkurunziza amekataa kukubali matokeo ya ushindi wa Rais Pierr Nkurunziza na kwamba, kuna haja ya kuendeleza majadiliano katika msingi ya ukweli na uwazi, ili kutafuta muafaka wa mgogoro wa kisiasa unaoendelea kufuka moshi nchini Burundi hata baada ya uchaguzi mkuu kuhitimishwa na matokeo kutangazwa hivi karibuni.

Bwana Rwasa anasema lingekuwa ni jambo la busara ikiwa kama Rais Nkurunziza angeanza mchakato wa kuunda Serikali ya umoja wa kitaifa, itakayowawezesha wananchi wa Burundi kujiandaa kwa ajili ya kufanya uchaguzi mkuu utakaokuwa huru na wa haki. Katika uchaguzi huu, Rais Nkurunziza alipata kura asilimia 69.41% na mpinzani 18.99 %.

Tangu awali Jumuiya ya Kimataifa ilionesha kwamba, uchaguzi mkuu nchini Burundi haukuwa wa kweli na haki kutokana na mauaji na vurugu zilizoandamana na mchakato mzima wa uchaguzi. Rais Barack Obama wakati wa ziara yake ya kikazi nchini Kenya, amelijadili suala la uchaguzi mkuu nchini Burundi pamoja na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya. Ameitaka Serikali na wapinzani kuanza majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kutafuta suluhu ya kudumu ya mgogoro huu unaotishia ustawi na maendeleo ya wananchi wa Burundi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.