2015-07-27 10:03:00

Wafundeni barabara majandokasisi ili kukabiliana na changamoto za maisha!


Kutokana na vitimbwi vya maisha vinavyoendelea kujitokeza katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, kuna haja ya kuhakikisha kwamba, majandokasisi wanafundwa barabara: kiakili, kiroho, kimaadili, kiutu na kichungaji, ili kuwawezesha kuwa tayari kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Majiundo makini ni kati ya vipaumbele vya Kanisa kwa sasa ili kuwa na wakleri wema na watakatifu watakaosaidia mchakato wa Uinjilishaji mpya.

Chuo kikuu cha Kipapa cha “Regina Apostolorum” kilichoko mjini Roma, wakati wa likizo ya kiangazi kinaendesha kozi maalum kwa ajili ya walezi wa majandokasisi kutoka sehemu mbali mbali za dunia, ili wawe kujifunza kutoka kwa Yesu mwenyewe Injili ya furaha, tayari kuwashirikisha majandokasisi katika hija ya maisha na malezi yao ya kikuhani.

Monsinyo Patròn Wong, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Wakleri akizungumza na washiriki wa kozi hii fupi amewataka kuwa makini katika utume wao, ili kuwasaidia Maaskofu mahalia katika maandalizi ya viongozi wa Kanisa. Ili kutekeleza dhamana hii nyeti katika maisha na utume wa Kanisa walezi wenyewe hawana budi kuhakikisha kwamba, wanafundwa barabara katika mambo msingi ya maisha na utume wa Kanisa, tayari kuwarithisha majandokasisi wao, utajiri unaofumbatwa katika maisha na utume wa kipadre.

Uelewa wa mwanadamu mintarafu mafundisho ya Kanisa ni msingi thabiti katika majiundo ya Wakleri kadiri ya hali ya maisha na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu mamboleo. Leo hii kuna changamoto nyingi katika maisha na utume wa Kipadre anasema Monsinyo Wong. Majandokasisi hawana budi kufundwa katika misingi ya kiutu, kichungaji, kiakili na katika maisha ya kiroho, ili kweli waweze kuwa ni wachungaji wema na watakatifu mintarafu Kristo mchungaji mwema, daima wakionesha wema na huruma kwa watu wao.

Wakleri wanahamasishwa kushuhudia kwa maneno na matendo zile tunu msingi zinazofumbatwa katika undani wa maisha yao ya kiroho, ili watu waguswe na kuvutika na huduma inayotolewa kama kielelezo cha imani inayomwilishwa katika matendo. Waoneshe kweli kwamba, wameitwa na kuchaguliwa na Kristo kwa ajili ya huduma ya mambo matakatifu.

Mapadre wawe ni watu wa sala, wanaojibidisha kujenga utamaduni wa kusikiliza kwa makini na kujadiliana na wengine, tayari kushiriki katika mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Mapadre waoneshe wema na huruma ya Mungu katika maisha na utume wao. Licha ya Mapadre wanaoshiriki kozi hii maalum inayohitimishwa hapo tarehe 30 Julai 2015, lakini inaonekana kana kwamba, wote wanakabiliana na changamoto zile zile, pengine kwa viwango tofauti. Majiundo haya endelevu yamewakumbusha Mapadre hawa kwamba, wanahudumia Kanisa moja, takatifu katoliki na la mitume.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.