2015-07-27 09:33:00

Ng'oeni ndago za: uhalifu, rushwa, umaskini, ujinga na ukosefu wa usawa!


Familia ya Mungu nchini Perù inawajibika kuhakikisha kwamba, inang’oa maadui na vikwazo vya uhuru wa kweli vinavyofumbatwa katika uhalifu, rushwa na ufisadi wa mali ya umma; umaskini wa hali na kipato; ukosefu wa misingi ya usawa na haki jamii pamoja na ujinga. Haya ni mambo msingi ambayo yanabainishwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Perù wakati wa maadhimisho ya Siku kuu ya kitaifa, tarehe 28 na tarehe 29 Julai 2015.

Maadhimisho haya yawe ni mwanzo wa matumaini mapya kwa Familia ya Mungu nchini Perù, lakini kwa bahati mbaya bado kuna giza kubwa inayogubika mchakato wa umoja wa kitaifa; kanuni maadili na uongozi bora na matokeo yake wananchi wengi wametopea na kumezwa na malimwengu. Kumbe, kuna haja ya kujikita katika utawala bora na wa sheria, unaongozwa na fadhila ya unyenyekevu kwa kutambua kwamba, cheo ni dhamana na uongozi ni huduma ya upendo na kamwe si kwa ajili ya mafao ya mtu binafsi. Uongozi ujielekeze katika kutafuta na kudumisha utu, heshima, ustawi na mafao ya wengi.

Kwa namna ya pekee, Baraza la Maaskofu Katoliki Perù linaitaka familia ya Mungu nchini humo, kusimama kidete, kulinda, kutetea na kushuhudia Injili ya Uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, ili kuwajengea wananchi matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Wananchi wajenge utamaduni na ari ya kuchapa kazi kwa ufanisi, ukweli, uwazi, ugunduzi na mshikamano, huku wakishuhudia tunu msingi za maisha ya kiroho na kimwili, kama kielelezo cha imani tendaji inayopania kuyatakatifuza malimwengu.

Familia ya Mungu nchini Perù inapaswa kuwa ni matunda ya tunu msingi za maisha ya kifamilia na kijamii walizorithishwa kama zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Tunu hizi zilindwe, ziendelezwe na kurithishwa kwa vijana wa kizazi kipya kama sehemu ya mang’amuzi ya kijamii.

Maaskofu wanakaza kusema, kati ya changamoto kubwa zinazowakabili wananchi wa Perù ni: mwingiliano wa mawazo; maendeleo ya sayansi na teknolojia; ulinzi na usalama pamoja na utunzaji bora wa mazingira. Changamoto zote hizi zinapaswa kushughulikiwa kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu; kwa kuthamini maisha tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumbaoni mwa mama yake hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Wananchi wajifunze kuheshimu na kutunza mazingira nyumba ya wote kama anavyo kaza kusema Baba Mtakatifu Francisko.

Maaskofu wanasema kwamba, kumbu kumbu ya maadhimisho ya Miaka 194 ya uhuru wa Perù ni changamoto na mwaliko wa kusimama kidete kulinda na kudumisha uhuru ambao kimsingi ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Uhuru ukipata chapa katika imani na Neno la Mungu, unawasaidia wananchi kuwajibika barabara, tayari kushiriki katika mchakato wa ujenzi na maboresho ya nchi yao katika misingi ya ukweli na haki.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.