2015-07-27 12:00:00

Mwaka Mtakatifu wa huruma ya Mungu utakuwa ni Jubilei ya Vijana Duniani!


Maadhimisho ya Siku ya 31 ya Vijana Duniani yataanza kutimua vumbi tarehe 26 hadi tarehe 31 Julai 2016, Jimbo kuu la Cracovia, Poland. Bado vijana wengi wanakumbuka maadhimisho ya Siku ya Vijana yalioadhimishwa Jimboni Czestochowa kunako mwaka 1991. Kwa mwaka 2016 maadhimisho haya yanaongozwa na Heri za Mlimani, muhtasari wa mafundisho makuu ya Yesu; tema ambayo iko moyoni mwa Baba Mtakatifu Francisko.

Baba Mtakatifu anawahamasisha vijana kusoma na kutafakari Heri za Mlimani kama sehemu ya majiundo yao ya maisha ya kiroho. “Heri wenye rehema maana hao watapata rehema” ni dira na mwongozo wa maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko kwa wakati huu. Huu ni muhtasari wa Injili na Maisha ya Kikristo. Huruma ni chemchemi inayoweza kuwaponya walimwengu kutoka katika saratani ya dhambi; mmong’onyoko wa kimaadili na mapungufu ya maisha ya kiroho.

Upendo unasaidia kujaza mioyo ya watu kwa mambo mema na matakatifu; kwa kufungua mioyo na historia. Hii inatokana na ukweli kwamba, Yesu ni chemchemi ya huruma na upendo. Hapa waamini wanahamasishwa kuwa watu wenye rehema ili waweze kupata pia rehema; mambo yanayopewa kipaumbele cha pekee katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu uliotangazwa na Baba Mtakatifu Francisko. Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, kwa mwaka 2016 yatakuwa ni Jubilei ya Vijana Duniani.

Haya yamo kwenye ujumbe wa Kardinali Stanislaw Rylko, Rais wa Baraza la Kipapa la walei wakati huu Mama Kanisa anapojiandaa kuadhimisha Siku ya Vijana Duniani, mwaka mmoja kuanzia sasa. Vijana watahamasishwa kwa namna ya pekee kufanya tafakari ya kina kuhusu huruma kama kielelezo makini cha imani inayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kufumbwa katika sura, maisha na utume wa Yesu Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai. Vijana wanahamasishwa kuwa ni wajumbe na watangazaji wa huruma ya Mungu duniani. Wawe tayari kushibisha majangwa ya maisha ya mwanadamu kwa huruma na upendo wa Mungu.

Kardinali Rylko anakaza kusema, Madhabahu ya Huruma ya Mungu na ya Mtakatifu Faustina Kowalska, mtume wa huruma ya Mungu yaliyozinduliwa rasmi kunako mwaka 2002 na Mtakatifu Yohane Paulo II yatakuwa ni chimbuko la tafakari kwa vijana wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2016. Vijana wataweza pia kupata nafasi ya kupita katika malango ya Jubilei ili kujipatia rehema zinazotolewa na Mama Kanisa wakati wa maadhimisho haya.

Itakuwa ni nafasi kwa waamini kukimbilia huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho katika lugha mbali mbali. Katika tukio  hili, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa pia kukaa katika kiti cha maungamo, ili kuwapatia baadhi ya vijana huruma na upendo wa Mungu. Uzoefu unaonesha kwamba, vijana wengi wanatumia fursa hii kwa ajili ya kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zao. Maadhimisho ya Sakramenti ya Upatanisho ni muhimu sana wakati wa Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Baba Mtakatifu na Vijana watapitia lango la Jubilei ya huruma ya Mungu wakati wa Mkesha wa Sala, tarehe 30 Julai 2016, mkesha huu utahitimishwa kwa Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu. Tarehe 31 Julai 2016, wakati wa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, Papa Francisko anatarajiwa kuwapatia wawakilishi wa Mabara yote taa inayowaka, kielelezo cha moto wa huruma ya Mungu ulioletwa na Yesu Kristo.

Baba Mtakatifu atawatuma vijana kwenda sehemu mbali mbali za dunia kushuhudia na kuwa kweli ni Wamissionari wa huruma ya Mungu. Tangu wakati huu, Mama Kanisa anaendelea kuiweka hija ya maisha ya kiroho inayofanywa na vijana sehemu mbali mbali za dunia chini ya huruma na upendo wa Mungu, ili kweli waweze kuwa ni mashuhuda wa huruma ya Mungu kwa watu wa nyakati hizi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.