2015-07-27 08:47:00

Jumuiya ya Kimataifa ikiungana kwa pamoja, UKIMWI unaweza kupewa kisogo!


Mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi duniani ni changamoto inayohitaji mshikamano wa kimataifa, ikiwa kama kweli dunia inataka kuupatia Ukimwi kisogo. Ni mwaliko ambao umetolewa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa washiriki wa mkutano wa tisa wa Chama cha Ukimwi Duniani, uliokuwa unafanyika huko Vancouver, Canada.

Baba Mtakatifu anasema, umoja ni nguvu na kwamba anapenda kuwatia shime wale wote wanaojitaabisha kwa ajili ya kuokoa na kuendeleza maisha ya mwanadamu, kwa kuwapatia waathirika wa Ukimwi dawa za kurefusha maisha sanjari na kuzuia maambukizi ya Virusi vya Ukimwi kutoka kwa mama mjamzito kwenda kwa mtoto. Baba Mtakatifu anapenda kuwahakikishia wote hawa sala na sadaka yake katika mchakato huu wa kudumisha Injili ya uhai, kwa ajili ya mafao ya wengi.

Papa anapenda kuwatia moyo waendelee kuchakarika katika tafiti na tiba, ili kufanikisha mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi ambao umekuwa ni janga kubwa kwa maisha ya familia nyingi duniani. Lengo ni kumhudumia mtu mzima: kiroho na kimwili kwani ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Ugonjwa wa Ukimwi umekuwa na madhara makubwa katika ustawi na maendeleo ya wengi kwani unaendelea kupukutisha nguvu kazi ndani ya jamii.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu umepelekwa kwa Dr. Julio Montaner, Rais mwenza wa mkutano huo ambaye pia ni Mkurugenzi mkuu wa Kituo cha Ukimwi, Hospitali ya Mt. Paulo iliyoko mjini Vancouver, Canada. Hiki ni kituo kinachomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki na kimekuwa mstari wa mbele katika kutoa tiba ya kurefusha maisha kwa wagonjwa walioathirika kwa virusi vya Ukimwi pamoja na tafiti kuhusiana na ugonjwa huu usiokuwa na tiba wala chanjo hadi sasa.

Tafiti zimeiwezesha Jumuiya ya Kimataifa kuzuia maambukizi ya virusi vya Ukimwi kutoka kwa mama mjamzito kwenda kwa mtoto, jambo ambalo linaendelea kuleta matumaini makubwa kwa watoto wanaozaliwa na wazazi ambao wana virusi vya Ukimwi. Kauli mbiu ambayo imeongoza maadhimisho ya mkutano huu ambao umewashirikisha wadau mbali mbali ni “Tiba kama njia ya kuzuia maambukizi ya Virusi vya Ukimwi. Matumaini ya kisayansi yanaonesha kwamba, ifikapo mwaka 2030 gonjwa la Ukimwi duniani litakuwa limepewa ufumbuzi wa kudumu.

Hii inatokana na ukweli kwamba, ikiwa kama  asilimia 90% ya wagonjwa walioambukizwa na virusi vya Ukimwi watafanyiwa utafiti wa kutosha, wanaweza kupewa tiba ya kurefusha maisha. Mchakato huu hauna budi kuelekezwa hata kwenye nchi changa zaidi duniani ambako wagonjwa wengi wa Ukimwi bado hawajafanikiwa kupata dawa ya kurefusha maisha.

Takwimu zinaonesha kwamba, jumla ya wagonjwa millioni 15 walioathirika kwa virusi vya Ukimwi wanapata tiba ya kurefusha maisha, lakini kuna zaidi ya watu millioni 22 ambao hawafahamu kwamba wameambukizwa kwa virusi vya Ukimwi na wala hawapati tiba muafaka.

Kwa upande wake, Monsinyo Robert Vitillo, mshauri maalum wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis, amewasilisha mchakato wa huduma inayotolewa na Kanisa Katoliki pamoja na Mashirika yake ya misaada kitaifa na kimataifa kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa na waathirika wa Ukimwi sehemu mbali mbali za dunia, hususan Kusini mwa Jangwa la Sahara, ambako maambukizi ya virusi vya Ukimwi bado yako katika kiwango cha juu. Zaidi ya Dolla millioni 740 zimetumika katika kipindi cha miaka tisa kwa ajili ya kusaidia na kuwahudumia wagonjwa wa Ukimwi.

Monsinyo Vitillo ameridhishwa na mafanikio yaliyokwisha kupatikana kutokana na utekelezaji wa mradi wa “The Dream” unaosimamiwa na kuendeshwa na Jumuiya ya Mtakatifu Egidio katika baadhi ya nchi za kiafrika, ili kuzuia maambukizi ya virusi vya Ukimwi kutoka kwa mama mjamzito kwenda kwa mtoto wakati wa kujifungua. Asilimia 25% ya miundo mbinu inayotumika kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa wa Ukimwi, inamilikiwa na Kanisa Katoliki. Hii inaonesha kwamba, Kanisa ni mdau mkubwa wa Serikali nyingi duniani katika  mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.