2015-07-27 16:01:00

JK aanza ziara ya kikazi nchini Australia!


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete aliondoka nchini Tanzania usiku wa Jumamosi, Julai 25, 2015, kwenda Australia ambako anaanza ziara rasmi ya Kiserikali, Jumatatu, Julai 27, 2015. Rais Kikwete anafanya ziara hiyo rasmi ya Kiserikali katika Jumuia ya Madola ya Australia (The Commonwealth of Australia) kwa mwaliko wa Mheshimiwa Jenerali Sir Peter Cosgrove AK MC (Mstaafu), Gavana Jenerali wa Jumuia ya Madola ya Australia.

Wakati wa ziara yake, Rais Kikwete ambaye mara ya mwisho alitembelea Australia kuhudhuria Mkutano wa Wakuu wa Serikali wa Nchi za Jumuia ya Madola mjini Perth mwaka 2011, atatembelea mji mkuu wa Australia wa Canberra na miji ya Newcastle na Sydney. Mara baada ya kuwasili mjini Canberra, Rais Kikwete atapanda Mti wa Kumbukumbu katika Bustani ya Taifa ya Miti ya Australia na kutembelea Makumbusho ya Taifa ya Vita ya nchi hiyo kabla ya kukutana na Watanzania wanaoishi katika Australia.

Jumanne, Julai 28, 2015, Rais Kikwete atafanya mazungumzo rasmi ya Kiserikali na Waziri Mkuu wa Australia, Mheshimiwa Tony Abbot (MB) na pia kukutana kwa mazungumzo na mwenyeji wake Gavana Jenerali Sir Peter Cosgrove ambaye alipata pia kuwa Mkuu wa Majeshi ya Australia.

Aidha, Rais Kikwete atakutana na kufanya mazungumzo na Mheshimiwa GaiBrodtmann (MB), Waziri Kivuli wa Ulinzi wa Australia. Maeneo makuu ambako mazungumzo kati ya Rais Kikwete na viongozi hao wa Australia yanatarajiwa kujikita ni katika eneo la madini na uchimbaji wake, fursa za elimu ya juu na mafunzo ya ufundi, masuala yanayohusu Bahari ya Hindi (The Indian Ocean Rim) na usalama wa Bahari hiyo, ugaidi na masuala ya usalama wa nchi za Afrika Mashariki.

 Rais Kikwete pia atatumia nafasi hiyo kuwashukuru na kuagana na viongozi wa Australia, nchi ambayo kwa miongoni mitano iliyopita imekuwa na uhusiano wa karibu na Tanzania katika maeneo ya uchumi, ulinzi, siasa, jamii na masuala ya usalama. Jioni ya siku hiyo, Rais Kikwete atahudhuria dhifa ya kitaifa ambayo itaandaliwa kwa heshima yake na mwenyeji wake, Gavana Jenerali Sir Peter Cosgrove na baada ya dhifa hiyo, Rais Kikwete na ujumbe wake wataondoka mjini Canberra kwenda Sydney, mji mkuu wa kibiashara wa Australia.

Jumatano, Julai 29, 2015, Rais Kikwete atakwenda mjini Newcastle ambako atatunukiwa Digriii ya Uzamivu ya Heshima ya Sheria (Degree of Doctors of Laws Honoriscausa – honorary LLD) na Chuo Kikuu cha Newcastle. Rais atatunukiwa digrii hiyo ya heshima kwa kutambua uongozi wake uliotukuka na mchango wake katika maendeleo ya Tanzania na Afrika na jitihada zake za kuleta amani.

Chuo Kikuu cha Newcastle ni moja ya vyuo ambavyo vimekuwa vinatoa nafasi za masomo kwa wanafunzi wa Tanzania, chini ya sera ya miaka mingi ya Australia kusaidia elimu katika Tanzania. Wanafunzi 26 wa Tanzania tayari wamemaliza masomo katika chuo hicho na kurejea nyumbani katika maeneo ya madini, elimu ya juu, vyombo vya habari, masuala ya fedha na masuala ya serikali. Wanafunzi 45 bado wanaendelea na masomo yao katika chuo hicho. Rais Kikwete na ujumbe wake wataondoka Australia asubuhi ya Alhamisi, Julai 30, 2015 kurejea nchini Tanzania.

Na mwandishi maalum.








All the contents on this site are copyrighted ©.