2015-07-26 13:50:00

Siku ya Vijana Duniani 2016 Kumekucha! Asiye na mwana aeleke jiwe!


Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2016 huko Cracovia, Poland, yataanza kutimua vumbi hapo tarehe 26 Julai 2016. Baba Mtakatifu Francisko baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 26 Julai 2015 amezindua mchakato wa vijana kuanza kujiandikisha, tayari kushiriki katika maadhimisho haya. Hili ni tukio la maisha ya kiroho linalokwenda sanjari na maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa huruma ya Mungu uliotangazwa na Baba Mtakatifu Francisko.

Ni kipindi muafaka cha kuganga na kutibu majereha ya kinzani, migogoro na vita, tayari kuambata na kushuhudia upendo na huruma ya Mungu katika maisha ya mwanadamu. Familia ya Mungu inasubiri kwa hamu kubwa kuona ushuhuda wa matendo ya huruma: kiroho na kimwili yakilimwilishwa katika uhalisia wa maisha ya binadamu, ili kweli watu wengi zaidi waweze kuguswa na Injili ya Kristo. Ni fursa kwa Watoto wa Kanisa kufanya toba na wongofu wa ndani kwa kujikita katika msamaha na upatanisho katika ngazi mbali mbali za maisha ya mwanadamu.

Padre Gregorio Suchodolski, Katibu mkuu wa Kamati ya Siku ya Vijana Duniani Jimbo kuu la Cracovia 2016 anakaza kusema, huu utakuwa ni mwendelezo wa maadhimisho ya Jubilei ya huruma ya Mungu inayomwilishwa katika maisha ya vijana, moto wa kuotea mbali. Matukio makuu ni pamoja na mapokezi makubwa yanayoandaliwa na vijana kwa Baba Mtakatifu Francisko, Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya uzinduzi wa Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani; Maadhimisho ya Ibada ya Njia ya Msalaba.

Maadhimisho haya ni nafasi kwa vijana kupata katekesi ya kina kuhusu: Neno la Mungu, Mafundisho Jamii ya Kanisa na Kanuni maadili na utu wema, tayari kuyamwilisha katika maisha yao kama kielelezo cha imani tendaji. Vijana wote watakaoshiriki katika maadhimisho haya watatembelea maeneo ya kihistoria na yale ambayo tayari yamepangwa kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Itakuwa ni nafasi kwa vijana pia kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zao kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho; ibada ambayo itafanyika kwenye Uwanja wa Huruma ya Mungu, mahali ambapo pia kutafanyika mkesha na Ibada ya Misa takatifu ili kufunga maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani.

Katika maandalizi, Kanisa nchini Poland linaendelea kuwahimiza vijana kujikita katika maisha ya kiroho, kiutu na kimaadili kwa kujisomea na kutafakari Neno la Mungu; kwa kushiriki kikamilifu katika Sakramenti za Kanisa, lakini kwa namna ya pekee kabisa, Sakramenti ya Upatanisho na Ekaristi Takatifu zinazowakirimia waamini huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao, tayari kuhjisadaka kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa na jamii inayowazunguka. Kanisa linaendelea kujenga Jumuihya za vijana, ili ziweze kuonesha jeuri kwa kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa.

Maadhimisha ya Siku ya Vijana Duniani yanafanyika nchini Poland, miaka michache tu baada ya Baba Mtakatifu Francisko kumtangaza Papa Yohane Paulo II kuwa Mtakatifu na msimamizi wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani. Maadhimisho haya nchini Poland yanapania kuwapatia vijana changamoto ya kuwa kweli ni vyombo na wajenzi wa huruma kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Faustina Kowalska. Waamini wanaendelea kuhamasishwa kutambua na kuthamini umuhimu wa huruma ya Mungu katika maisha yao, tayari kuimwilisha kwa wale wote wanaowazunguka.

Padre Gregorio Suchodolski anasema, vijana wana matumaini makubwa na uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko miongoni mwao, ili kuwapatia imani, matumaini na mapendo katika safari ya maisha ya ujana wao, licha ya ukosefu wa fursa za ajira na “majanga” yanayotokana na udhaifu wa maisha ya ujana. Huruma ni tema inayopewa kipaumbele cha pekee katika maadhimisho ya Siku ya vijana duniani itakayoadhimishwa Jimbo kuu la Cracovia, Poland.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.