2015-07-26 13:19:00

Papa Francisko azindua mchakato wa kujiandikisha kwa Siku ya Vijana Duniani 2016


Mara baada ya sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 26 Julai 2015 Baba Mtakatifu Francisko amezindua rasmi mchakato wa vijana kujiandikisha katika maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, itakayoadhimishwa Jimbo kuu la Cracovia, Julai 2016 na kuoongozwa na kauli mbiu “heri wenye huruma maana watahurumia”. Baba Mtakatifu anasema amejiandikisha kama hujaji katika siku hii.

Maadhimisho haya yanakwenda sanjari na Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu anawaalika vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia kujiandikisha kuanzia sasa ili kuweza kushiriki katika tukio hili la kihistoria katika maisha ya Jumuiya zao.

Baba Mtakatifu amemkumbuka pia Padre Paolo Dall’Oglio ambaye alitekwa sasa yapata miaka miwili! Anawaalika watekaji nyara wake kumwachilia huru mtawa huyu ili aweze kuendelea na maisha pamoja na utume wake. Baba Mtakatifu pia anawakumbuka Maaskofu wa Kanisa la Kiorthodox waliotekwa kutoka Syria pamoja na wote ambao wametekwa nyara katika maeneo ya vita, ili waweze kuachiliwa huru. Baba Mtakatifu anawaalika viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kuongeza bidii ili watu hawa waweze kupata tena uhuru wao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.