2015-07-26 13:08:00

Jitahidini kuishi mantiki ya Yesu, kwa kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa jirani


Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 26 Julai 2015 wakati wa tafakari ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican amezungumzia kuhusu muujiza wa Yesu kuwalisha watu elfu tano kwa kugeuza mikate mitano na samaki wawili. Huu ni muujiza ambayo Yesu aliutenda baada ya kuzungukwa na umati mkubwa watu na baada ya kuwaponya wagonjwa wao. Yesu anatenda yote haya kwa nguvu ya huruma ya Mungu, ili kuwaponya wagonjwa kiroho na kimwili.

Baba Mtakatifu anasema Yesu pia anaonesha kwamba, ni mwalimu anayewafundisha watu, kwa kupanda mlimani, mahali ambapo pameandaliwa na Baba yake wa mbinguni. Akiwa katika mazingira haya, Yesu anawaweka Mitume wake majaribuni, hali akijua lile ambalo alipaswa kulitenda. Mitume wanajiuliza, itawezekanaje kuwalisha watu wote hawa anahoji Mtume Filippo ambaye anataka kuwahamasisha watu kuchangia ili kununua mkate kwa ajili ya kuwalisha watu, lakini idadi ya watu ni wengi na mchango utakaotolewa hauwezi kufua dafu!

Mitume wanazungumzia suala hili katika dhana ya soko yaani kununua, lakini Yesu anawataka watoe. Andrea anaonesha kwamba, kuna mtoto ambaye ana mikate mitano na samaki wawili na Yesu ana amrisha watu waketekishwe. Baba Mtakatifu anasema, Yesu alikuwa anasubiri wazo hili na hapo anachukua mikate na wale samaki wawili na kuwabariki na hatimaye, watu wanagawiwa. Matukio haya yanapata mwelekeo wake kwenye Karamu ya Mwisho, Yesu Mkate ulioshuka kutoka mbinguni anatoa maana ya kina zaidi kuhusu Fumbo la Ekaristi Takatifu.

Yesu ni mkate wa Mungu, kwa kuungana naye, waamini wanapokea maisha mapya na hivyo kuwa kweli ni watoto wapendwa wa Mungu sanjari na kujenga udugu kati yao. Ili kuwa na ushiriki mkamilifu wa Fumbo la Ekaristi Takatifu, waamini wanachangamotishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanaishi kweli mantiki ya Yesu, yaani sadaka na kujitoa bila ya kujibakiza, ili kushirikiana na wengine. Hata katika umaskini, kila mtu anaweza kuchangia kitu fulani kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya binadamu.

Kujenga umoja na Yesu kuna maanisha kuchota kutoka kwa Kristo neema inayowawezesha waamini kushirikiana na wengine kwa kile ambacho wamekirimiwa na Mwenyezi Mungu na katika maisha yao kama walivyo!

Umati mkubwa unapigwa na bumbuwazi kutokana na muujiza uliotendwa na Yesu! Lakini ikumbukwe kwamba, Yesu anawajalia watu wenye njaa utimilifu wa maisha; anazima njaa ya mwili, lakini pia njaa ya maana ya maisha, njaa na kiu ya Mungu. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wanaweza kuchangia kadiri ya uwezo wao ili kukabiliana na mateso, mahangaiko na upweke unaomsibu mwanadamu; katika kukabiliana na umaskini, kila mtu anaweza kutenda badala ya kukaa na kulalama tu.

Kila mtu amekirimiwa zawadi na karama katika maisha; mambo yanayoweza kutolewa kwa ajili ya kujenga mshikamano wa upendo, haki, amani, ili kuwashirikisha wengine ile furaha inayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ambaye ana uwezo wa kuongeza mambo maradufu kutokana na ukarimu na mshikamano wa watu wake, kama kielelezo cha kushiriki katika sadaka yake. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuonesha moyo wa upendo, ukarimu na mshikamano ili kila mtu aweze kupata walau mahitaji yake msingi kwa njia ya mshikamano na upendo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.